Tuesday, February 24, 2015

SISTA WA KANISA KATOLIKI JIMBO LA IRINGA AFARIKI DUNIA, SITA WAJERUHIWA VIBAYA



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

SISTA Innocensia Kisaka (33) wa kanisa Katoliki, Jimbo la Iringa mkoani Iringa amefariki dunia na wenzake sita kujeruhiwa vibaya baada ya gari walilokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso na gari jingine, ambalo lilikuwa mbele yao katika kijiji cha Sanangura, Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.

Ajali hiyo ilitokea kwenye barabara ya kutoka Njombe kwenda Songea, ambapo Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Mihayo Msikhela alisema tukio hilo lilitokea Februari 20 mwaka huu majira ya usiku, huku akimtaja aliyefariki dunia kuwa ni Sista huyo wa kanisa Katoliki.

Kadhalika Msikhela aliwataja waliojeruhiwa ambao hivi sasa, wamelazwa katika Hospitali ya misheni Peramiho mkoani humo kuwa ni; Padre Jastine Sapila (70), Sista Christine Banda (63) Sista Karomere Mfuse (48) Erasto (20) Karo Mhagama (21) na Thadei Charles (20) wote wakazi wa Seminari kuu Peramiho.


Alifafanua kuwa siku hiyo ya tukio gari lenye namba za usajili T 94 DDC aina ya Land Cruiser, ambalo ilikuwa linaendeshwa na Fadher Kastori Goriama (52) wa Seminari kuu Peramiho, lilikuwa linatoka Iringa kwenda Peramiho na kwamba liligongana uso kwa uso na gari lenye namba za usajili T 926 CDB aina ya Suzuki Carry, lililokuwa likiendeshwa na dereva  ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja baada ya kukimbia kusikojulikana, mara baada ya ajali hiyo kutokea.

Baada ya magari hayo kugongana, majeruhi hao walikimbizwa katika hospital hiyo kwa ajili ya matibabu zaidi, na kwamba hali zao zinaendelea vizuri na chanzo cha ajali hiyo kinaendelea kuchunguzwa ikiwemo polisi, wanamsaka dereva aliyekimbia ili hatua za kisheria ziweze kuchukua mkondo wake.

No comments: