Tuesday, February 3, 2015

DOKTA NCHIMBI: CCM HAINA TATIZO LA KIMUUNDO WALA MFUMO


Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya sherehe za maadhimisho ya miaka 38 ya kuzaliwa CCM, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Songea, Dokta Emmanuel Nchimbi akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe katika maadhimisho hayo, yaliyofanyika kitaifa juzi kwenye uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma, katikati ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho.

Na Kassian Nyandindi,

Songea.

MWENYEKITI wa maandalizi ya sherehe za miaka 38 ya Chama Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Mbunge wa Songea mjini, Dokta Emmanuel Nchimbi amesema, chama chake kina kila sababu ya kushinda kwa kishindo kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, kwa kuwa kina mfumo na muundo imara.

Akizungumza muda mfupi baada ya maadhimisho hayo mjini Songea, Dokta Nchimbi alisema kuwa chama hicho, hakina tatizo la kimfumo wa muundo na kuongeza kuwa ushindi ni lazima.

“Chama hakina tatizo la muundo wala mfumo, tutakachofanya ni kubadilisha mikakati tu ili kujihakikishia ushindi katika uchaguzi ujao”, alisema.

Akizungumzia kuhusu kauli ya Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Rais Jakaya Kikwete kuwataka viongozi wa chama kuwatembelea wanachama na kushawishi wanachama wapya, alisema  CCM ni chama kikubwa na ndani yake wapo viongozi waliolala ambao mwenyekiti wa taifa aliwakumbusha kuamka na kufanya kazi.

“Chama hakiwezi kuwa na maisha marefu kama viongozi katika ngazi zote hawajitumi, katika jeshi kubwa kama hili la CCM wapo watu ambao lazima wasukumwe na ndiyo hawa mwenyekiti wetu wa taifa, aliwasukuma kupitia hotuba yake.

 Alifafanua kuwa wanatakiwa kuamka na kufanya kazi kwa bidii ili kukiwezesha chama kushinda kwa kishindo, kama ambavyo kimekuwa kikishinda tangu kuanza kwa siasa za vyama vingi.


Dokta Nchimbi aliishukuru Halmashauri kuu ya chama kwa kuweza kuuchagua mkoa wa Ruvuma, kuwa mwenyeji wa maazimisho ya miaka 38 ya chama hicho na kueleza kuwa miaka mingi mkoa huo umekuwa ngome imara ya chama cha mapinduzi.

Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho alisema chama chake kimeshaanza  kujipanga kwa ajili ya uchaguzi mkuu na kuweka mikakati ambayo itakipatia ushindi mnono.

“Nimeshawaagiza viongozi wa chama katika ngazi ya mkoa na wilaya kuanza vikao kwa ajili ya kuweka mikakati thabiti ya ushindi, katika uchaguzi mkuu ujao”, alisema.

Hata hivyo aliongeza kuwa, chama katika mkoa wake tayari kilishaanza mikakati ya kujitegemeza ikiwa ni kufuata agizo la Mwenyekiti huyo wa taifa, ambapo tayari kimejipanga vyema kuendeleza vyanzo vyake vya mapato pamoja na kuanzisha vyanzo vipya kwa ajili ya kukifanya kijitegemee.

No comments: