Monday, February 16, 2015

AKAMATWA NA MENO YA TEMBO WAKATI ANAYASAFIRISHA KWA PIKIPIKI

Meno ya Tembo.


Na Mwandishi wetu,
Songea.

JANATI Haji (32) mkazi wa kijiji cha Rwinga wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, ametiwa mbaroni baada ya kukamatwa na meno sita ya Tembo, ambayo alikuwa anayasafirisha kwa kutumia pikipiki, akitokea katika kijiji hicho kwenda Songea mjini, mkoani humo.

Kamanda wa polisi wa mkoa huo, Mihayo Msikhela akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa alisema, tukio hilo lilitokea juzi katika katika kijiji hicho.

Msikhela alisema kuwa inadaiwa siku hiyo ya tukio askari ambao walikuwa doria, waliweza kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo, akiwa na meno hayo ambayo aliyabeba kwenye pikipiki yenye namba ya usajili, T 448 CZT aina ya Sanlg.


Alifafanua kuwa Haji alikuwa akiyasafirisha meno hayo ya Tembo, kwenda Songea ambako inadaiwa ndiko alikokuwa anatarajia kuyauza kwa mtu anayemjua yeye, ambapo upelelezi unaendelea kufanyika, ili kuweza kujua ni nani ambaye alikuwa akimpelekea kwa ajili  ya kumuuzia.

Polisi kwa kushirikiana na maafisa wa idara ya wanyama pori, wanafanya jitihada ili kupata thamani ya nyara hizo na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani wakati wowote, mara tu upelelezi utakapokamilika.

Kamanda Msikhela alisema kuwa jeshi la polisi mkoani Ruvuma, bado linaendelea na msako mkali ili kuwabaini watu wanaojihusisha na biashara hiyo, kwenye mbuga ya wanyama ya Selou iliyopo mkoani humo, ambapo tembo wengi huuawa.

No comments: