Thursday, February 26, 2015

TASAF YAPINGA VITENDO VYA UPOTOSHWAJI JUU YA SHUGHULI ZAKE


Na Steven Augustino,

Njombe.

TAARIFA potofu kuhusu yale yanayofanywa katika awamu ya tatu, katika mpango wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) kwamba umezifanya baadhi ya kaya maskini hapa nchini, zinazokidhi vigezo vya kuwezeshwa kiuchumi kuwa zimekosa fursa ya kunufaika na mpango huo, imeelezwa kuwa sio kweli bali ni upotoshaji katika jamii.

Mkurugenzi mtendaji wa TASAF, Ladislaus Mwamanga alisema mpango huo ulizinduliwa Agosti 15 mwaka 2012 na Rais Jakaya Kikwete na kuanza kutekelezwa Februari 2013 ambapo unalenga kuzinusuru kaya masikini, kwa kuzisaidia fedha ili zipate huduma mbalimbali ikiwemo elimu, afya na maji.

Akifungua kikao cha kazi cha siku mbili mjini Njombe jana, ambacho kimewashirikisha waratibu wa mpango huo, wahasibu, maafisa ufuatiliaji na wanahabari, Mwamanga alisema baadhi ya kaya maskini zimekuwa zikidanganywa kwamba fedha zinazotolewa kupitia mpango huo ni za Freemasons.


Washiriki hao ambao wakakuja na mikakati ya pamoja ya kuelimisha jamii juu ya malengo na manufaa ya mpango huo, katika kupunguza umaskini nchini wanatoka katika Halmashauri za mikoa ya Mbeya, Ruvuma, Iringa na Njombe.

“Kwa wasio na elimu sahihi juu ya mpango huu wanaogopa kujiunga na mpango kwa sababu ya taarifa hizi potofu, na hivyo familia zao kukosa uwezeshaji huu ambao tunataraji kuutekeleza sasa,” alisema.

Ili kuondokana na upotoshaji huo, TASAF itahakikisha inawatumia wanahabari katika maeneo husika ili wasaidie kufikisha kwa umma taarifa sahihi za mpango huo, ambao ni mmoja kati ya mipango mingi inayolenga kufikia lengo namba moja la millennia katika kukabiliana na umasikini.

Mpangu huo ni wa miaka kumi, Mkurugenzi huyo alisema kaya milioni moja zinazoishi katika mazingira duni ya umaskini, zitafikiwa na kuwezeshwa hapa nchini.

Alisema mpango huo una sehemu kuu tano, ikiwemo ya uhawilishaji fedha kwa kutoa ruzuku kwa kaya hizo zenye watu wenye uwezo wa kufanya kazi, kujenga na kuboresha miundombinu inayolenga sekta ya elimu, afya na maji, na kujenga uwezo katika ngazi zote za utekelezaji.

Alisema utawezesha pia kaya maskini hususan watoto chini ya miaka mitano na wajawazito kupata lishe bora, huduma za afya, elimu na ajira kwa kupitia ruzuku za aina mbili, ya msingi na ya kutimiza masharti maalumu.

“Hizo ndio kazi zinazofanywa katika mpango huu, na fedha za kutekeleza hayo yote zinatolewa na serikali yenyewe kwa kushirikiana na wadau wake mbalimbali ikiwemo benki ya dunia, hapa hakuna Freemason kama ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakisema na kupotosha jamii,” alisema Mwamanga.

No comments: