Sunday, February 22, 2015

KIKONGWE ALIYEKATWA NYETI TUNDURU APATIWA MATIBABU HOSPITALI

Na Steven Augustino,

Tunduru.

KIKONGWE mwenye umri wa miaka 70, ambaye ni mkazi wa kijiji cha Majimaji wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Patrick Vitus amelazwa katika hospitali ya wilaya hiyo, akiwa amepoteza fahamu (hajitambui) baada ya kukatwa sehemu zake za siri.

Taarifa za tukio hilo zinaeleza kuwa, babu huyo alifanyiwa kitendo hicho na mkwe wake aliyefahamika kwa jina la Zainabu Said.

Mjomba wa majeruhi huyo, Mussa Said akizungumzia juu ya kitendo hicho alisema, kilitokea majira ya usiku wa kuamkia Februari 20 mwaka huu.

Alisema wakati linafanyika hilo, yeye alikuwa akitokea katika mazingira ya msitu ambao upo jirani na mashamba yaliyopo katika kitongoji kipya cha Lukumbule, kilichopo kata mpya ya Majimaji wilayani humo.


Said alieleza kuwa kutokana na yeye hakuwepo shambani huko, bado alikuwa akijiuliza maswali mengi na kubaki anashangaa, baada ya kupata taarifa juu ya tukio hilo.

“Bado najiuliza maswali mengi ambayo majibu yake siyapati, maana nilipo mhoji mke wangu, alinieleza kuwa alichukua uamuzi huo baada ya mjomba wangu kutaka kumbaka”, alisema Said.

Alisema wakati anafuatilia mkasa huo, mjomba huyo alimjibu kuwa alikatwa na kisu na mkwe wake huyo wakati akijaribu kumlazimisha afanye naye tendo la ndoa, sasa wakati wakiwa wanaelekea katika nyumba ya mke mdogo wa Mussa Said,  ndipo mkasa huo ulitokea ambako mwanamke Siwema Mustapha alidai kutaka kupeleka dawa ya kienyeji ambayo ingeweza kuifarakanisha ndoa yao. 

“Majibu haya yananifanya niendelee kuumiza kichwa na ninaona kuna kilicho jificha kati yao, kwani kama mjomba wake huyo alikuwa na nia ya kumbaka mkwe wake, angeweza kweli kufanya tukio kama hili ndani ya nyumba hii”, alisema.

Mganga mfawidhi wa Hospitali ya wilaya Tunduru, Dokta Mmary Zabron alithibitisha kumpokea majeruhi huyo na kuongeza kuwa, hali yake inahitaji uangalizi wa muda mrefu wa maafisa tabibu.

Katika tukio hilo majeruhi, alikatwa na kuumizwa vibaya sehemu za korodani pamoja na sehemu za maoteo ya uume wake, maeneo ambayo yameshonwa kwa lengo la kuangalia uwezekano wa kurudisha viungo vyake ambavyo viliharibiwa, kuwa katika hali yake ya kawaida.

Mihayo Msikhela ambaye ni Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, alisema Polisi wanamshikilia Zainabu Said, ambaye anahusika na tukio hilo kwa mahojiano zaidi.

Hata hivyo aliongeza kuwa, baada ya uchunguzi kukamilika mtuhumiwa huyo atafikishwa Mahakamani, ili aweze kukijibu kosa hilo ambalo  linamkabili.

No comments: