Monday, February 16, 2015

MWALIMU NAMABENGO AJINYONGA NA KUPOTEZA MAISHA



Na Mwandishi wetu,
Songea.

MWALIMU mmoja ambaye anafundisha shule ya msingi Kaijere, kijiji cha Namabengo wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Shaibu Niali (30) amekutwa akiwa amefariki dunia na mwili wake ukining’inia chumbani kwake, baada ya kujinyonga kwa kutumia khanga.

Habari zilizopatikana mjini hapa, na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoa huo, Mihayo Msikhela alisema kuwa tukio hilo lilitokea Februari 14 mwaka huu, majira ya usiku kwenye chumba chake alichokuwa analala.

Msikhela alifafanua kuwa mnamo majira ya saa moja usiku, Niali kabla hajajinyonga alimpigia simu dada yake aitwaye, Asia Niali mkazi wa Majengo Manispaa ya Songea, kwa kumjulisha kuwa anaumwa sana akimuomba aende haraka kijijini Namabengo, akamuone na ampeleke nyumbani kwa mama yake mzazi kijijini Lusewa wilayani humo.

Alifafanua kuwa marehemu huyo, kwa muda mrefu alikuwa ana ugomvi mkubwa na mke wake ambaye baadaye walilazimika kutengana, lakini alionekana kutokubali kukaa na watoto, jambo ambalo lilikuwa linaleta ugomvi mara kwa mara kati ya wandani hao wawili.


Niali wakati anampigia simu huyo dada yake akimtaka aende kumuona, tayari alikuwa ameandaa Khanga ya kujinyongea, na panga kwa lengo la kutaka kwenda kumcharanga kwanza mke wake, ambaye anaishi mbali kidogo na nyumba yake ndipo arudi na kuchukua maamuzi hayo magumu.

Msikhela aliongeza kuwa dada yake baada ya kupigiwa simu ambaye ni Asia, alichukua uamuzi wa kuwasiliana na majirani, ambao walikuwa wanaishi na mwalimu huyo kwa lengo la kujua kipi kilichomkuta kaka yake, ndipo majirani hao wakaenda nyumbani kwa Niali, na kumkuta akiwa amejinyonga.

Baada ya kuona hali hiyo majirani waliwasiliana na uongozi wa serikali ya kijiji cha Namabengo, na kutoa taarifa kituo cha Polisi wilaya ya Namtumbo, ndugu na jamaa wa marehemu huyo.

Hata hivyo Kamanda huyo wa polisi mkoani Ruvuma, alieleza kuwa polisi walipopata taarifa juu ya tukio hilo, walikwenda haraka huku wakiwa wameongozana na daktari kwa ajili ya uchunguzi wa mwili wa marehemu huyo, ili kuweza kuthibitisha juu ya kifo chake.

No comments: