Monday, February 9, 2015

DED TUNDURU ATAKIWA KUONGEZA UZALISHAJI WA KOROSHO

Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Chande Nalicho akisisitiza jambo katika mikutano mbalimbali aliyokuwa akiifanya wilayani humo.


Na Steven Augustino,
Tunduru.

SERIKALI wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, imemtaka Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Tinna Sekambo kuongeza nguvu katika usimamiaji wa zoezi la upandaji wa mikorosho mipya kwa wakulima wa zao hilo wilayani humo, ili waweze kuondokana na hali ya kipato duni walichonayo sasa, na hatimaye waweze kusonga mbele kimaendeleo.

Mkuu wa wilaya ya Tunduru Chande Nalicho, alitoa agizo hilo wakati akimkabidhi miche ya mikorosho kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Chiza Marando ikiwa ni muda mfupi baada ya mkuu huyo wa wilaya, naye kukabidhiwa miche 30,000 yenye thamani ya shilingi milioni 85 kutoka kwa mwenyekiti wa mfuko wa kuendeleza zao la korosho Tanzania. (WAKUF) 

Aidha Nalicho alimweleza mkurugenzi huyo kuwa ili kufanikisha ugawaji wa miche hiyo kwenda kwa wakulima, maafisa ugani wanatakiwa kwenda katika vituo vyao vya kazi vijijini, na kuacha kukaa maofisini.

Mkuu huyo wa wilaya ya Tunduru, aliahidi kufanya ziara ya ufuatiliaji juu ya zoezi hilo, la upandaji wa mikorosho ambalo linaendelea wilayani humo kwa lengo la kujionea utekelezaji wake. 


Awali akimkabidhi miche ya mikorosho hiyo, Mwenyekiti wa mfuko wa kuendeleza korosho Tanzania, Athuman Nkinde alimweleza Nalicho kuwa mfuko huo umeazimia kutekeleza kwa vitendo, kauli mbiu ya Kilimo kwanza.

Nkinde alifafanua kuwa mikorosho hiyo ambayo inasambazwa na kugawiwa bure kwa wakulima wote hapa nchini, imegharimiwa na  mfuko huo ikiwa ni mpango wa kuendeleza na kuongeza uzalishaji wa zao hilo kila mwaka, ambapo matarajio yao ni kusambaza miche milioni 10 yenye thamani ya shilingi milioni 500 ifikapo  mwaka 2015 na 2016.

Alisema miche hiyo husambazwa kwa wakulima, baada ya kufanyiwa usanifu na wataalamu wa mimea kutoka kituo cha utafiti Naliendele, ambacho kimeweka matawi yake katika wilaya ya Tunduru, ambacho kinahudumia nyanda za juu kusini, Mpwapwa ambacho kinahudumia wakulima kanda ya ziwa na Mkuranga wakulima wa  kanda ya Mashariki na kaskazini.

Ili kwenda na ongezeko la uzalishaji, pia mfuko huo umeandaa utaratibu wa kugawa mashine maalum ambazo zitatumika kuwasaidia wakulima kupulizia mikorosho yao ili waweze kuongeza uzalishaji.

Sambamba na utekelezaji wa zoezi hilo WAKUF imeandaa utaratibu wa kujenga viwanda vitatu, ambavyo ujenzi wake utagharimu shilingi bilioni 6 kwa ajili ya Kubangulia korosho za wakulima, kwa lengo la kuziongezea thamani na kupata bei nzuri sokoni. 

Viwanda hivyo vitajengwa katika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Mtwara, na wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani ambapo ujenzi wake unatarajiwa kuanza mapema mwaka huu.
Katika makabidhiano hayo, kaimu mkurugezni wa halmashauri ya wilaya hiyo, Chiza Marando aliushukuru mfuko huo kwa msaada wake huku akimhakikishia mkuu wa wilaya hiyo, Nalicho kuwa halmashauri yake imejipanga katika kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa na kutekelezwa kwa wakati ili wakulima waweze kupiga hatua.

Marando alieleza kuwa mbali na zoezi hilo kuwa na changamoto ya wakulima wengi kutochangamkia fursa hiyo, kwa madai ya kutegemea mikorosho waliyorithi kutoka kwa babu zao, alisema miche hiyo ina faida nyingi ikiwemo ya kuzaa katika kipindi cha miaka miwili baada ya kupandwa, na huzaa mazao mengi kuliko mikorosho ya zamani.
  
Wakizungumza kwa niaba ya wakulima wenzao, Mussa Nasoro kutoka kijiji cha Namasakata, Mwajuma Nakayaya na Mussa Kaisi wote wa kijiji cha Mchoteka kwa nyakati tofauti waliipongeza serikali kwa kuwapelekea mradi huo, na kutoa wito kwa wakulima wenzao kuchangamkia miche hiyo, ili iweze kuwaletea faida ya kuvuna mikorosho mingi na hatimaye kusonga mbele kimaendeleo.
   
Meneja wa kituo cha utafiti wa zao hilo, katika kituo cha Nakayaya wilayani Tunduru, Said Mawanje aliwaomba viongozi wa mfuko huo kuandaa utaratibu na kupeleka oda iliyobakia ya uzalishaji wa mikorosho hiyo mapema, ili kuwawezesha kuandaa na kukabidhi miche hiyo kabla ya mwezi wa kwanza mwakani.

No comments: