Tuesday, February 3, 2015

JWTZ WATEGUA BOMU TUNDURU, WANANCHI WAKUMBWA NA TAHARUKI


Bomu lililookotwa wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, kisha kuteguliwa na JWTZ.

Na Steven Augustino,

Tunduru.

JESHI la Polisi wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, kwa kushirikiana na  Jeshi la wananchi JWTZ wametegua na kulipua bomu lenye ukubwa wa milimita 82 ikiwa ni lengo la kuzuia madhara yanayoweza kutokea baadae, kama vile usalama wananchi wa kijiji cha Wenje wilayani humo, ambako bomu hilo lilionekana.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Mihayo  Msikhela alisema kuwa bomu hilo lilionekana karibu na nyumba ya mkulima mmoja, aliyefahamika kwa jina la Ngaunje Sadick.

Alifafanua kuwa bomu hilo ni la kurushwa na bunduki yenye uwezo mkubwa, huenda lilitelekezwa katika maeneo hayo miaka ya 1960 wakati wa harakati za wapigania uhuru wa nchi jirani ya Msumbiji, na kuangukia upande wa Tanzania ambapo inaonesha halikulipuka kutokana na matatizo ya kutokuwa na nguvu.

Kamanda Msikhela alifafanua kuwa bomu liliteguliwa kwa kulipuliwa kwa kuunguzwa na moto mkubwa, uliowashwa kwa kutumia kuni nyingi huku akiongeza kuwa kutokana na kukosa nguvu na kushindwa kulipuka wakati liliporushwa, lilitoa mwanga mdogo ulioonesha kuwa tayari limekwisha haribika.

Kufuatia hali hiyo Wananchi wa mkoa wa Ruvuma, na maeneo mengine wameshauriwa pale wanapoona kitu cha ajabu mfano wa bomu, wasikiguse badala yake watoe taarifa haraka katika vyombo vya ulinzi na usalama, ambavyo vipo karibu nao.



Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi wa kijiji cha Wenje wilayani Tunduru mkoani humo, ambacho kipo mpakani mwa Tanzania na nchi jirani ya Msumbiji walikiri kupatwa nahofu ya kuwa katika taharuki kubwa, baada ya kupata taarifa kuwa mkulima mwenzao kijijini hapo kaleta bomu hilo, hadi nyumbani kwake akidhani kuwa kaokota kitu cha thamani.

Walisema Kufutia hali hiyo mamia ya wakanachi wa kijiji hicho wote walikimbia kijijini hapo na kutelekeza watoto, mali na vitu mbalimbali.

Kwamujibu wa taarifa za tukio hilo, zinaeleza kuwa mkulima huyo aliyefahamika kwa jina la Ngaunje Sadiki aliliokota bomu hilo wakati akilima shambani kwake katika eneo la mto Ruvuma, na kulazimika kulibeba hadi nyumbani kwake akiwa na matumaini kuwa kitu hicho kingemsaidia kujikwamua katika maisha magumu baada ya kukiuza.

Taarifa hizo zilifafanua kuwa Sadiki aliliokota Januari 24 mwaka huu na kulibeba hadi nyumbani kwake, na kukaa nalo ndani ya nyumba yake kwa zaidi ya siku 4 hadi alipokutana na mtu aliyefahamika kwa jina moja la Mandiko kwa madai kuwa ndiye aliyemtegemea kuwa na ujuzi wa kukitambua kitu hicho na kumkabidhi ili akakiuze Mjini Tunduru, na aweze kupata fedha.

Mashuhuda hao waliendelea kufafanua kuwa wakati Sadiki akiwa na matumaini hayo Januari 27, alikutana na mtu huyo aliyemlenga kumhusisha katika uuzaji wa dili hilo ambapo baada ya kuliona tu alihamaki na kumweleza kuwa kitu alichokuwa amekihifhadhi ndani ya nyumba yake ni bomu, na hatari kwa maisha yake, familia na majirani zake kijijini hapo.

Kwa mujibu wa mashuhuda hao baada ya maelezo hayo taarifa za kuwepo kwa bomu hilo, zilianza kusambaa kijijini hapo na kuwafikia watu wengi hali ambayo ilisababisha wananchi hao kutimua mbio na kuacha nyumba zao wakihofia kulipukiwa na kupoteza maisha.

Akizungumzia hali hiyo Ngaunje Sadiki pamoja na mambo mengine alikiri kukibeba kitu hicho na kukihifadhi ndani ya nyumba yake, huku akieleza kuwa chanzo chake kilijengwa katika matumaini ya kukiuza kitu hicho hata kama kwa kukipima kama chuma chakavu, lakini angeweza kupata kiasi kidogo cha fedha ambazo zingemsaidia kujikwamua na hali ngumu ya maisha ambayo imekuwa ikimkabili kwa kipindi kirefu.

Sadiki alisema kuwa baada ya matumaini yake kuyeyuka na kuonekana kitu hicho ni hatari hata kwa maisha yake, alipiga konde moyo na kulazimika kukibeba kwa siri na kwenda kukitupa porini katika eneo la mto Ruvuma, ikiwa ni matumaini yake ya kuondoa taharuki hiyo aliyonayo yeye na majirani wenzake kijijini hapo.

No comments: