Saturday, February 7, 2015

TUME YA UCHAGUZI YAENDESHA MAFUNZO WILAYANI MBINGA JUU YA MFUMO WA MATUMIZI MASHINE ZA KISASA UANDIKISHAJI WAPIGA KURA

Afisa uchaguzi kutoka makao makuu ya Tume ya uchaguzi hapa nchini, Crecencia Mayalla upande wa kushoto, akitoa maelekezo kwa Waandikishaji wasaidizi ngazi ya kata wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, namna ya kutumia mashine za kisasa (BVR) ambazo zitatumika kwa ajili ya zoezi la uandikishaji wapiga kura, ambalo linatarajiwa kuanza hivi karibuni hapa nchini.


Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa makini na kufuatilia juu ya mfumo wa matumizi, mashine za kisasa (BVR) kwenye ukumbi wa Chuo cha maendeleo Mbinga mjini.

Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

TUME ya Taifa ya uchaguzi hapa nchini, imeendesha mafunzo kwa Waandikishaji wasaidizi ngazi ya kata wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, juu ya mfumo wa matumizi, mashine za kisasa (BVR) ambazo zitatumika kwa ajili ya uandikishaji wapiga kura, katika daftari la kudumu mapema mwaka huu.

Mafunzo hayo ambayo yameendeshwa kwa siku mbili, katika ukumbi wa chuo cha maendeleo ya jamii wilayani humo, yanalenga uboreshaji wa daftari hilo kwa lengo la kudhibiti mianya ya udanganyifu kwa baadhi ya watu, ambao hujiandikisha zaidi ya mara moja.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Afisa uchaguzi kutoka makao makuu ya tume hiyo, Crecencia Mayalla alisema mfumo huo unarahisisha pia utendaji kazi wakati wa zoezi hilo la uandikishaji wapiga kura, ambalo linatarajiwa kuanza hivi karibuni.

“Mashine hizi zinatengeneza kadi ya mpiga kura, ambayo inamwezesha mtu kufungua akaunti benki, kumdhamini polisi, kupata paspoti ya kusafiria na hata cheti cha kuzaliwa”, alisema Mayalla.



Awali akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga aliwataka washiriki kuzingatia taaluma waliyoipata na kuwa waangalifu juu ya matumizi ya mashine hizo, kutokana na umuhimu wa zoezi hilo katika jamii.

Mkuu huyo wa wilaya, aliwasisitiza washiriki wa mafunzo hayo kuwa waangalifu wakati wa matumizi wa mashine hizo, ili zisiharibiwe kwa kuwa serikali imezinunua kwa gharama kubwa.

Ngaga alisema, kwa mwandikishaji ambaye ataona hawezi kumudu namna ya kutumia mashine hizo, ni vyema akajiondoa mapema ili asiweze kuharibu mwenendo wa zoezi hilo.

“Napenda kutoa wito kwenu na wananchi kwa ujumla, wakati zoezi hili la uandikishaji litakapoanza washawishini wananchi wajitokeze kwa wingi, na huko muendako nendeni mkawahamasishe pia waweze kushiriki kikamilifu”, alisema Ngaga.

Hata hivyo, mmoja kati ya wakufunzi wa mafunzo hayo, Peter Mdaki alisema kuwa, washiriki wamekuwa wepesi kuelewa juu ya matumizi ya mashine hizo kutokana na wengi wao, kuwa na elimu ya matumizi ya kompyuta.




1 comment:

Unknown said...

thanks for good news.........!!!!