Sunday, February 1, 2015

CCM RUVUMA YALIA NA UJENZI WA BARABARA YA NAMTUMBO TUNDURU

Leo bendi mbalimbali mjini Songea mkoani Ruvuma, nazo hazikuwa mbali kutumbuiza wakati wa maadhimisho ya miaka 38 kitaifa, kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Na Steven Chindiye,
Songea.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Ruvuma, kimemuomba Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Dokta Jakaya Kikwete kusimamia kikamilifu ujenzi wa barabara kiwango cha lami kutoka wilaya ya Namtumbo kwenda Tunduru mkoani humo, ili iweze kukamilika kwa wakati na kuufanya mkoa huo, ufunguke na kutoa fursa mbalimbali za kimaendeleo kwa wananchi wake na taifa kwa ujumla.

Hayo yalisemwa leo kwa nyakati tofauti na Mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho na Mwenyekiti wa kamati ya  maandalizi ya sherehe za chama hicho Mbunge wa jimbo la Songea mjini Dokta Emmanuel Nchimbi, katika maadhimisho ya sherehe za kitaifa miaka 38 kuzaliwa kwa chama cha mapinduzi zilizofanyika kwenye uwanja wa Majimaji mjini Songea.

Pamoja na mambo mengine walimpongeza Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Dokta Kikwete kwa kuupatia mkoa huo, heshima ya kuandaa maadhimisho hayo.

Maagizo mengine yaliyotakiwa kutolewa maelekezo kwa watendaji wake ni pamoja na ahadi iliyotolewa na Rais huyo, mwezi Julai mwaka jana alipokuwa katika ziara yake ya kikazi mkoani humo, juu ya ujenzi wa barabara kilometa 2.4 ambao hadi leo hii haujatekelezwa. 


Ahadi nyingine ambayo utekelezaji wake ni kizungumkuti ni pamoja na agizo la serikali kuiingiza hospitali ya mkoa wa Ruvuma, katika mfumo wa bajeti pamoja na uendelezaji ujenzi wa mfumo wa maji safi na taka katika Manispaa ya Songea.

Pamoja na kuiomba serikali kufanya hivyo, viongozi hao hawakuwa wachoyo wa fadhila kwa kuishukuru serikali kwa kutekeleza miradi ya fedha za IPZ ambapo katika maadhimisho hayo, Dokta Kikwete alikabidhi cheki ya shilingi bilioni 2.

Aidha kwa niaba ya wakulima wa mkoa wa Ruvuma, pia Oddo Mwisho na Dokta Nchimbi waliishukuru serikali kwa kutoa shilingi bilioni 8 kwa ajili ya kuwalipa wakulima, walioikopesha serikali mahindi katika vituo vya kununulia zao hilo.

Mwentekiti Oddo Mwisho, alimhakikishia Mwenyekiti CCM taifa Dokta Kikwete kuwa majimbo saba ya uchaguzi yaliyopo mkoani humo, katika uchaguzi mkuu ujao chama hicho kitashinda bila matatizo yoyote yale.

Akijibu maombi hayo Dokta Kikwete alisema kuwa kilio cha muda mrefu cha wananchi wa mkoa huo, kimesikika na akawataka wananchi kuwa na subira wakati serikali inaendelea na utekelezaji wake.

Alisema taarifa alizokuwa nazo juu ya kusuasua kwa ujenzi wa barabara ya lami wilaya ya Namtumbo hadi Tunduru mkoani humo, kunatokana na msimu wa mvua kubwa zinazoendelea kunyesha hali ambayo alifafanua kuwa mara mvua hizo zitakapopungua kunyesha, ujenzi huo utaendelea.

Dokta Kikwete aliongeza pia, serikali inaendelea kutekeleza ahadi yake ya kujenga kivuko kwa kuanza na ujenzi wa chelezo, katika eneo la kivuko mto Ruhuhu wilaya ya Nyasa.

Kuhusu umeme vijijini, alisema mkoa wa Ruvuma unatarajia kunufaisha wananchi waishio katika vijiji 3000, huku sekta ya afya tayari amekwisha toa maelekezo ya kujengwa kwa Hospitali mpya ya mkoa wa Ruvuma ya rufaa, ili iliyopo ibakie kwa ajili ya matumizi ya wagonjwa wa Manispaa hiyo.

No comments: