Sunday, February 22, 2015

USHIRIKA NAMTUMBO YASAMBAZA WALIMU MASHULENI KUANZA MAZOEZI YA KUFUNDISHA



Na  Yeremias Ngerangera,
Namtumbo.

CHUO cha ualimu, Ushirika wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, kimesambaza wanachuo kutoka katika chuo hicho kwenda shule mbalimbali za msingi wilayani humo, ili waweze kuanza mazoezi ya kufundisha watoto shuleni.

Mwandishi wetu akizungumza na Mkuu wa chuo hicho, Awadh Nchimbi alisema kuwa tayari wanachuo 120 wamekwisha pelekwa katika shule hizo, wakiwemo wanaume 80 na wanawake 40.

Alifafanua kuwa, chuo kimedhamiria kufanya hivyo ili kuweza kujenga misingi imara ya kuwajengea uwezo wa kufundisha wanachuo hao pale wanapokuwa darasani, ili baadaye watakapohitimu masomo yao waweze kufanya vyema kwa vitendo na kufuata weledi wa kazi ya ualimu.


Nchimbi aliongeza kuwa kutokana na uhaba wa majengo waliyonayo chuoni hapo, pia wanampango wa kuhakikisha kuanzia sasa wanajenga majengo ya kutosha hususani, mabweni ya kulala wanafunzi ili kuweza kukidhi mahitaji husika kutokana na yaliyopo sasa kutojitosheleza.

Aidha imeelezwa kuwa kuanzishwa kwa chuo hicho, kunahamasisha wazazi wenye watoto kusomesha kwa bidii wakiwa na lengo la kuwataka kujiunga na chuo cha ualimu, Ushirika baada ya kuona vijana kutoka maeneo mbalimbali mkoani humo, kwenda kujiunga na masomo ya ualimu.

Pamoja na mambo mengine, chuo hicho kipo katika kijiji cha Nahoro kata ya Luegu wilaya ya Namtumbo, Ruvuma umbali wa kilometa 10 kutoka makao makuu ya wilaya hiyo, kuelekea Songea mjini.

No comments: