Sunday, February 1, 2015

HOTUBA YA RAIS KIKWETE KATIKA MAADHIMISHO YA SHEREHE ZA CCM SONGEA MKOANI RUVUMA HII HAPA

Rais Jakaya Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa (CCM), akiwasili katika uwanja wa Majimaji leo mjini Songea mkoani Ruvuma, katika sherehe za maadhimisho ya kitaifa miaka 38 ya kuzaliwa kwa CCM.
Hotuba ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Kikwete:

Mheshimiwa Makamu mwenyekikiti wa CCM, Philip Mangula Mwenyekiti wa NRM. Huyu ni rafiki yangu mkubwa, ni rubani pia. Alishawahi kunisafirisha na ndege akiwa kama rubani.

Nawashukuru wahusika wote na waheshimiwa mbalimbali mliopo hapa katika maadhimisho ya sherehe hizi.

Anammwagia sifa Mhe. Nchimbi kwa maandalizi mazuri na kuwashukuru viongozi mbalimbali wa CCM kwa kazi nzuri, akiwemo Katibu mkuu, AbdulRahman Kinana.

Nchi yetu imepiga hatua, kuna amani, utulivu na maendeleo yanayoonekana. CCM imeendelea kuaminiwa katika awamu zote. Hata mwaka huu itakuwa hivyo hivyo. Nalisema hili bila wasiwasi kabisa, roho baridiiiii.

Dalili ya mvua ni mawingu, ushindi tulioupata kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa Oktoba 2014 ni ushahidi tosha, ndugu zetu wapinzani hawana chao.

Tusikate tamaa, tunaweza kuwa na changamoto nyingi mwaka huu ila tunapaswa kuwa na ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi. Lazima tuhakikishe tuwe wamoja. Umoja ni ushindi.

Anaendelea.....


Komba nakushukuru sana kwa wimbo mzuri, huishiwi nyimbo (vichekooo).

Huu ni mwaka ambao tunapaswa kuwa na rasilimali za kutosha kuweza kuwapatia ushindi wagombea wetu, ni mwaka wa kuhakikisha tunafanikisha kwa kiwango kikubwa.

Nafurahishwa na wale waliofanya kazi kubwa. Nawapongeza sana!

Nasikitishwa na viongozi wetu ambao hawajafanya kazi ipasavyo, hawa wanavunja moyo, wanazorotesha chama chetu. Kuna msemo unasema ''Jasho jingi wakati wa amani, damu kidogo wakati wa vita''.

Maana yake maandalizi yakiwa ya kutosha, kazi inakuwa rahisi, kinyume chake unapunguza nguvu ya ushindi. Naomba kila mmoja ajipime yupo fungu gani.

Kila wilaya na mkoa kuwe na mfuko wa uchaguzi, na wakati ndio huu mfuko unatakiwa kufanya kazi. Sina budi kuwatahadharisha, msichukue fedha ambazo zitaleta matatizo!

Lazima tujiandae kama chama na kuwa na nyenzo zote kwa ajili ya kukiwezesha chama na wagombea wetu kushinda.

Katika jitihada za kutafuta pesa za kutunisha mifuko ya uchaguzi, Msichukue tu kila pesa, nyingine moto. Mi ushauri wangu ni huo tu!

Huu ni mwaka wa kutambua ahadi zipi zimetimizwa na zipi bado. zipo ahadi za Rais na za chama kuanzia mkoa, wilaya na kata. Mwaka wa kuulizwa ndio huu!

Waswahili husema, ''mla kunde husahau, mtupa maganda hasahau''. Kwahiyo watupiwa maganda hawajasahau. Lazima tuwe makini.

Sio tukiulizwa, tuanze kuwanyooshea vidole na kuwaita wapinzani. Kwa hiyo nasisitiza kila mmoja akumbuke ahadi zake. Mimi nayakumbuka maana naandika na wasaidizi wangu hunisaidia kunikumbusha, ila kusema kweli mengi tumetekeleza sana. Japo yapo machache bado.

Huu ni mwaka wa kuulizwa, si vizuri tuumalize mwaka huu huku tunaenda na madeni lukuki ya ahadi. Kushinda tutashinda, ila yatatupunguzia ushindi kwa machache ambayo bado hutuja yatekeleza. Huu ni mwaka wa kuongeza jeshi letu la ushindi, nalo ni wanachama wapya.

Jambo lingine kubwa na la muhimu ni kuwatembelea wanachama na wananchi kuzungumza nao. Jambo hili huwa hatulifanyi vizuri sana. Kila nikipata taarifa nina watu wengi wa kunipa taarifa, wengine hamuwajui nawajua mie.

Wananiambia, “Chama chako hakifanyi mikutano mingi kama wapinzani”. Japo ukiwauliza watajitetea. Ndugu zangu hili ni jambo kubwa, huwezi kupata ushindi kwa watu wasio kujua.

Tuache kukaa ofisini, tutoke tuwashawishi watu wajiunge na CCM. Kila ofisi ya mkoa na wilaya inayo gari la kuwawezesha kufanya kazi hiyo lakini hamtembei. Tulipokuwa hatujawapa magari ajenda ilikuwa ni magari. Mpaka mzee Mkapa akawa anakasirika, sasa tumewapa hayatumiwi inavyotakiwa.

Jambo la msingi ni kuwapata wapiga kura ili tushinde. Chama chetu kama vilivyo vyama vingine kinapaswa kuhimiza wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura.

Asiyekuwa na kadi mpya ya kupiga kura, hatoruhusiwa kupiga kura unaanza utaratibu mpya wa BVR, kadi za zamani hazitotumika.

Tume ikitangaza nenda usije ukasema unacho chako, wewe nenda kwa kuwa hicho cha zamani hakitotumika.

Asiyejiandikisha hatopata fursa ya kupiga kura ya maoni na ya uchaguzi mkuu. Hakuna kujiandikisha tena hii ndio ya mwisho! Asiyejiandikisha kala hasara.

Nawasihi wanachama wetu ambao ni zaidi ya milioni 8 wajiandikishe, ikiwa wote hawa watajiandikisha na kupiga kura, tutapata ushindi kwa kishindo!

Ndugu wananchi, tunajua jambo kubwa ni kura ya maoni ya Katiba pendekezwa ya hapo Machi, uandikishaji wa kupiga kura ndio lipo mbioni. Lingine ni uchapishaji na usambazaji wa katiba pendekezwa ili wananchi waisome.

Tuwasaidie wananchi kuwapatia elimu kuhusu katiba inayopendekezwa na kuhamasisha wananchi wapige kura ya ndio. Wenzetu watatoa elimu hasi sisi tutoe chanya. Wao watahimiza isipite, sisi tuhimize ipite..

Katiba iliyopendekezwa imebeba maslahi mapana ya nchi yetu, nadiriki kusema hakuna katiba bora kama hii ya sasa. Inatambua maslahi ya makundi maalum na namna ya kuyatimiza. Wakulima, wafugaji, wasanii, wanawake na mengine mengi.

Katiba imeshughulikia kero za muungano vizuri. Yale mambo yaliyokuwa yanaukwaza muungano, yamepatiwa suluhisho. Sioni sababu ya kukataa katiba inayopendekezwa.

Niwakumbushe tukiikataa hii, maana yake iliyopo itaendelea kutumika, maana hakuna nyingine. Na itakuja kuchukua miaka mingi ijayo. Labda rais ajaye apate hamu. Maana mimi nilipata hamu!

Wapinzani wamesikika wakisema hawatoshiriki na kuwataka wananchi wasishiriki, hii imenisikitisha. Mimi nawasishi washiriki na nawasihi wananchi washiriki, wao wakitaka kususia wasusie, ila nyie pigeni kura.

Nawasihi, msiache kupiga kura eti kisa tu serikali tatu haimo, maana hawana hoja nyingine. Sasa hivi bado hawa watu hawana muamko nalo, ila muda ukifika muamko utakuja. Serikali tatu haina muhemko kwa sasa.

Lakini jambo ni moja tu, kama kweli wananchi wanataka serikali tatu na humu haimo itathibitika kwenye kura. Wasiposhiriki tutashiriki sisi na tutashinda.

Msibabaishwe na wala msirudishwe nyuma.

Wananchi Mwezi Oktoba tutafanya uchaguzi mkuu. Utakuwa wa kihistoria kwani tunachagua Rais wa awamu ya tano. Mimi mwakani nitakuwa nafanya “handover” tu, lakini pembeni yangu atakaa MKUU WA NCHI. Mimi nataka rais ajae awe ni wa CCM.

Maelezo ni rais, namnukuu Mwalimu aliwahi kusema, “Rais wa nchi yetu anaweza kutoka chama chochote, lakini rais bora atatoka CCM”. Tuuenzi wosia huu mzuri.

Mgombea ambaye wananchi wakisikia jina lake tutakapomtangaza katika ukumbi wetu, wananchi watanzania waseme, “hapo barabara”.

Kushinda chaguzi za dola, ndiyo madhumuni makuu ya chama cha mapinduzi.

Tusipoipigia CCM tutakuwa tumemuangusha muasisi wetu. Aliwahi kusema bila CCM imara nchi itayumba. Tuhakikishe tusifanye vitendo vitakavyokiuka laana na hasara kwa taifa ni kubwa, na ni msiba mkubwa kwa CCM na nchi itayumba! Lazima tuhakikishe hatufiki huko. Watu wazuri wapo CCM wa kutosha, naamini mnawajua.

Mnaowaona wanafaa, washawishini wachukue fomu sio dhambi, hata mimi nilishawishiwa.

Ngoja nitoe siri moja, japo sio nyeti. Kinana aliniulizaga kipindi hicho “umemuona mzee fulani”? nikamjibu “sijamwona”, akaniambia ''uwe umemwona au hujamwona, we zingatia''.

Kwahiyo, Sio dhambi mnayemuona anafaa mpendekezeni hata kama anasita sita na kusema hajajiandaa kisaikolojia, mwambieni “wewe ndiye unayetufaa”.

Nina imani tunao watu wazuri sana ambao watatuvusha (Makofiii).

Msanii wetu Diamond yuko hapa, atatumbuiza ni msanii bora Afrika nzima na dunia, anapendwa sana. Ile nyimbo yake ya My Number One ikipigwa ile hata mimi nishawahi kuiimba kidogo. (Vicheko).

Nikizungumzia kwa mkoa wa Ruvuma, hali si mbaya sana. Maana kwa takwimu za ushindi wa kura za serikali za mtaa mwaka huu ni ushindi mzito. Tuimarishe zaidi. Kuhusu maendeleo yaa Ruvuma, yanaridhisha japo kasi zaidi inahitajika.

Kwa ufupi, Ruvuma ya miaka 10 iliyopita, si sawa na ya leo. Mwenye macho haambiwi tazama.

Jambo la mwisho nitazungumzia kuhusu mazao ya wakulima. Niliwahi kuelezea kutofurahishwa kwangu na deni lisilolipwa. Nimeagiza walipwe kwanza wakulima wale wadogo, nasikia wanatangulia kulipwa mawakala halafu wakulima wanacheleweshewa. Hili liangaliwe, walipwe kwanza wakulima wadogo.

Hivi karibuni tutapata pesa nyingi, bilioni 36 Waziri mkuu anasema bilioni zaidi ya 10 zishaletwa, zipo tutawapa. Safari hii hatutopenda kusikia tena malalamiko.

Sasa hebu tuanze safari, Wizara ya kilimo na wizara ya viwanda na biashara washirikiane na mikoa ya kilimo kama hii.

Namalizia, mafanikio ya kuongoza miaka 38 isitufanye tubweteke. Tuzidi kuongeza juhudi. Tuwe tayari kubadilika na kwenda na wakati. Itawezekana ikiwa tutaendelea kukuza demokrasia ndani ya chama. Na tukoseane bila chuki ndani ya chama.

Hatuna budi kuondoa utegemezi wa kifedha, kutegemea misaada na hata ruzuku na michango ya wafanyabiashara. Ipo siku watoa misaada na wafanyabiashara watapungua.

Tuwekeze nguvu zaidi kwenye kuzalisha kwa kutumia vizuri rasilimali zetu, lazima tuwe wabunifu. Hii yote ni ili kuwezesha chama chetu kijitegemee.

Nihitimishe kwa kusema leo ni siku ya furaha kwetu wote. Tuwakumbuke waasisi japo wawili, Mwalimu Julius K. Nyerere na Aboud Jumbe, kwani kwa busara zao, wao ndio walioanzisha chama cha CCM.

Kidumu chama cha mapinduzi !!

Baada ya Rais Kikwete kumaliza kutoa hotuba yake, msanii Diamond alipanda jukwaani na kuanza kutoa burudani.

No comments: