Friday, September 29, 2017

ONGEZEKO LA VIFO VYA UZAZI NCHINI LINASIKITISHA

Na Mwandishi wetu,

IMEELEZWA kuwa vifo vinavyotokana na uzazi vimeongezeka kutoka 432 kwa vizazi hadi laki moja katika kipindi cha mwaka 2012/2013 na kufikia 556 mwaka 2016/2017 sawa na akina mama 900 wanaopoteza maisha kila mwezi na 30 kila siku nchini wakati wanapojifungua.

Takwimu hizo zimetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa afya, Ummy Mwalimu alipokuwa akipokea mashine ya kisasa ya kutoa dawa ya usingizi wakati wa upasuaji, ambayo ilitolewa na taasisi ya utepe mweupe ambapo alisema katika kukabiliana na tatizo hilo ifikapo mwezi Juni mwaka 2018 Serikali itaongeza vyumba vya upasuaji kutoka 109 hadi kufikia 279 hapa nchini.

Akizungumza baada ya kukabidhi mashine hiyo Mratibu wa kitaifa wa taasisi ya utepe mweupe, Rose Mlay alisema kuwa ongezeko hilo la vifo linasikitisha na kwamba amemuomba Waziri Mwalimu kuhakikisha anaendelea kuweka mkazo katika suala la upatikanaji wa huduma za dharura na kwa haraka kwa akina mama wajawazito hasa katika maeneo ya vijijini.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dokta Mpoki Ulisubisya ambaye pia ni mtaalamu wa usingizi alielezea namna mashine hiyo inavyofanyakazi, uwezo wake na faida zake kwani haihitaji mitungi ya gesi wala umeme na ina uwezo wa kuonyesha viashiria vya hatari pale wakati inapotumika.


MATUKIO KATIKA PICHA USALAMA BARABARANI SONGEA

Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani (RTO) mkoa wa Ruvuma, Abel Swai akikagua daladala yenye namba T 657 BEZ linalofanya safari zake kati ya Songea mjini hadi kijiji cha Mtakanini wilayani Namtumbo mkoani humo, ambapo magari hayo hubainikia kuwa na matatizo mbalimbali ikiwemo ubovu na wafanyakazi wake kutokuwa na sare wanapofanya kazi hiyo ya kusafirisha abiria.
Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Ruvuma, Abel Swai akitoa elimu ya usalama barabarani kwa mwendesha baiskeli ambaye alikutwa akitembeza mkaa barabarani bila kufuata taratibu na sheria za usalama barabarani, jambo ambalo limekuwa ni chanzo cha kuongezeka kwa matukio mengi ya ajali zinazotokea mkoani humo. sha abiria. (Picha zote na Muhidin Amri)

Thursday, September 28, 2017

NHIF RUVUMA YAHIMIZA WANAMICHEZO KUCHANGAMKIA FURSA YA KUJIUNGA NA MPANGO WA MATIBABU

Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) mkoa wa Ruvuma, Abdiel Mkaro akikagua timu ya soka ya NHIF wakati wa bonanza maalum la kuhamasisha wanamichezo wa mkoa huo kuchangamkia fursa ya kujiunga na mfuko huo ili waweze kupata huduma bora za matibabu pale wanapougua.

Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) mkoa wa Ruvuma, Abdiel Mkaro upande wa kulia akikagua timu ya soka ya Makambi FC kabla ya kuanza mchezo wa kirafiki kati ya timu hiyo na timu ya NHIF katika bonanza la kuhamasisha wanamichezo wa mkoa huo na jamii kwa ujumla ili waweze kujiunga na mfuko huo.

Wafanyakazi wa NHIF mkoa wa Ruvuma Wakifanya mazoezi ya viungo wakati wa bonanza la kuhamasisha wanamichezo na jamii kuchangamkia fursa ya kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Mfuko wa Afya ya Jamii CHF.

Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) mkoa wa Ruvuma, Abdiel Mkaro akikabidhi zawadi kwa mshindi wa mbio za kukimbiza kuku, Edwina Bilungi aliyekuwa upande wa kulia katika bonanza hilo lililofanyika mwishoni mwa wiki mjini hapa.
Na Mwandishi wetu,       
Songea.

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umewataka na kuwahimiza wanamichezo hapa nchini, kuchangamkia fursa ya kujiunga na mpango wa matibabu kupitia Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) na wa NHIF ili waweze kupata huduma bora za matibabu hasa pale wanapougua au kupata majeraha wanapokuwa michezoni.

Rai hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Meneja NHIF mkoani Ruvuma, Abdiel Mkaro wakati wa Bonanza maalum la kuhamasisha jamii hasa wana michezo wajiunge na mifuko hiyo ili waweze kuwa na afya bora pale wanapougua.

Pia aliwataka Watanzania wakiwemo waandishi wa habari, kuona umuhimu wa kijunga na mpango huo kwa lengo la kuwa na uhakika wa kupata matibabu pale inapotokea wanapata ajali na magonjwa mbalimbali.

Monday, September 25, 2017

HALMASHAURI MJI WA MBINGA WATILIANA SAINI NA WANANCHI MAKUBALIANO USIMAMIZI SHIRIKISHI WA UPANDAJI MITI

Mikataba ya makubaliano mradi wa Panda miti kibiashara ikisainiwa kati ya halmashauri ya mji wa Mbinga na wananchi wa kijiji cha Lipilipili kata ya Mpepai katika ukumbi wa halmashauri hiyo mjini hapa, ambapo mradi huo wa panda miti kibiashara unafadhiliwa hapa nchini na Wizara ya maliasili na utalii pamoja na serikali ya Finland kwa lengo la kuinua kipato cha wananchi.
Upande wa kushoto Mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Mbinga, Kipwele Ndunguru akimkabidhi mmoja kati ya wanakikundi mkataba wa makubaliano wa mradi wa Panda miti kibiashara baada ya kusainiwa pande zote mbili kati ya halmashauri na wananchi wa kijiji cha Lipilipili kata ya Mpepai, Anayeshuhudia aliyevaa shati rangi nyeupe ni Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Robert Mageni.

Baadhi ya wakulima wa kijiji cha Lipilipili (Upande wa kulia) katika halmashauri ya mji wa Mbinga wakikabidhiwa ramani ya eneo la mlima Lihumbe na Mwenyekiti wa halmashauri ya mji huo, Kipwele Ndunguru aliyevaa koti rangi nyeusi na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Robert Mageni aliyevaa shati rangi nyeupe ambapo ramani hiyo ndiyo inaonesha eneo la mlima huo ambao mradi wa panda miti kibiashara utaanza kutekelezwa msimu wa mvua kuanzia mwezi Novemba hadi Disemba mwaka huu. 
Na Kassian Nyandindi,   
Mbinga.

IMEELEZWA kuwa Tanzania ni nchi ambayo imekuwa ikiongoza kwa uzalishaji wa mazao ya misitu Afrika Mashariki na kati, kupitia mikoa ya Nyanda za juu kusini hivyo wananchi wanaoishi katika mikoa hiyo wanapaswa kuendelea kupanda miti ili iweze kuwasaidia kuinua kipato chao.

Hayo yalisemwa juzi na Mshauri wa maliasili mkoa wa Ruvuma, Afrikanus Chale wakati alipokuwa kwenye kikao cha makubaliano ya kutiliana saini juu ya usimamizi shirikishi wa upandaji miti aina ya Milingoti (Eucalyptus) na Mikaratasi (Pines) katika msitu wa Lihumbe uliopo kijiji cha Lipilipili kata ya Mpepai halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani humo.

Kikao hicho kilifanyika kwenye ukumbi wa halmashauri ya mji huo ambapo kilifuatia baada ya wananchi wanaoishi katika kijiji hicho kuikubali programu hiyo ambayo ni ya upandaji miti kibiashara kupitia vikundi vya wakulima wa miti chini ya uangalizi wa halmashauri hiyo.

Wednesday, September 20, 2017

GILBERT: KWA NIABA YA SERIKALI MBINGA BINAFSI NAKUBALIANA NA UTENDAJI KAZI MZURI WA PARALEGALS

Wafadhili Anette Widholme Bolme, Alexandra Hallqvist na Ludviq Bontell ambao ni Meneja miradi kutoka Ubalozi wa ufalme Sweden na Victor Mlunde Meneja miradi kutoka Ubalozi wa ufalme wa Norway wakiwa katika Ofisi ya Katibu tawala wa wilaya ya Mbinga mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Gilbert Simya ambaye upande wa kulia amevaa koti rangi nyeusi walipomtembelea leo kwa lengo la kufahamiana.

Mfadhili Victor Mlunde Meneja miradi kutoka Ubalozi wa ufalme wa Norway aliyeshika kalamu akisoma taarifa akiwa na wafadhili wenzake katika Ofisi ya Katibu tawala wa wilaya ya Mbinga mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Gilbert Simya kutoka kushoto aliyevaa koti rangi nyeusi walipomtembelea leo kwa lengo la kufahamiana.


Wafadhili Anette Widholme Bolme, Alexandra Hallqvist na Ludviq Bontell ambao ni Meneja miradi wa Ubalozi wa ufalme Sweden na Victor Mlunde Meneja miradi kutoka Ubalozi wa ufalme wa Norway upande wa kushoto, wakiwa katika picha ya pamoja na Wasaidizi wa kisheria (Paralegals) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma walipotembelea leo katika kijiji cha Lituru kata ya Litembo wilayani humo.
Na Kassian Nyandindi,    
Mbinga.

SERIKALI wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma imesema kwamba, wanakubaliana na utendaji kazi wa Kituo cha msaada wa Kisheria na Haki za Binadamu (LHRC) kilichopo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kufuatia Wasaidizi wake wa kisheria (Paralegals) kutekeleza majukumu yao ya kazi kwa misingi na taratibu husika zilizowekwa.

Hayo yalisemwa na Katibu tawala wa wilaya hiyo, Mhandisi Gilbert Simya alipokuwa akizungumza Ofisini kwake na wageni kutoka Ubalozi wa Sweden na Norway Tanzania ambao ndiyo Wafadhili wanaoendesha na kufanikisha shughuli za msaada wa kisheria katika Kituo cha sheria na haki za binadamu wilayani hapa.

Leo Septemba 20 mwaka huu Wafadhili waliotembelea kwa Katibu tawala huyo ni Anette Widholme Bolme, Alexandra Hallqvist na Ludviq Bontell ambao ni Meneja wa miradi Ubalozi wa ufalme Sweden na Victor Mlunde wa kutoka Ubalozi wa ufalme wa Norway.

“Kwa niaba ya serikali Mbinga binafsi nakubaliana na utendaji kazi mzuri wa hawa wenzetu Paralegals, kwa sababu asilimia kubwa ya watu wetu wa Mbinga hawajui masuala ya kisheria na namna ya kupata haki zao za msingi”, alisema Simya.

SAKATA MRADI WA MAJI MKAKO MHANDISI MBINGA ASWEKWA LUPANGO

Na Kassian Nyandindi,   
Mbinga.

MHANDISI wa idara ya maji katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Vivian Mndolwa anashikiliwa na Jeshi la Polisi wilayani humo akituhumiwa kushiriki na wenzake, kuhujumu ujenzi mradi wa maji wa wananchi ambao serikali iligharimia shilingi milioni 718,896,533.

Vivian Mndolwa.
Aidha Mndolwa ambaye amewekwa Mahabusu katika Kituo kikuu cha Polisi cha wilaya hiyo tokea Septemba 19 mwaka huu anadaiwa kushindwa kusimamia mradi huo na kujengwa chini ya kiwango uliopo katika kitongoji cha Mnazi mmoja kijiji cha Mkako kata ya Mkako wilayani hapa.

Akizungumza leo na mwandishi wa habari hizi, Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma Germin Mushy amethibitisha kushikiliwa kwa Mhandisi huyo na kueleza kuwa mpaka sasa bado yupo mahabusu na kwamba kuna wenzake ambao wanatafutwa na jeshi hilo, walioshiriki kwa namna moja au nyingine kuhujumu mradi huo ili waweze kukamatwa na kuunganishwa katika shauri hilo na hatimaye watafikishwa Mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Mushy alieleza kuwa kutokana na taratibu za kiuchunguzi bado hazijakamilika hataweza kuwataja watu hao wanaotafutwa na kwamba aliongeza kuwa taarifa kamili za tukio hilo zitatolewa baadaye.

Tuesday, September 19, 2017

SERIKALI YALIFUNGIA GAZETI LA MWANAHALISI MIAKA MIWILI


WASAIDIZI WA KISHERIA MBINGA WAVITAKA VYOMBO VYA DOLA KUELIMISHA WANANCHI

Upande wa kushoto anayezungumza ni Mkurugenzi wa utetezi na maboresho kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) jijini Dar es Salaam, Anna Henga akiwa pamoja na Wafadhili wa kituo hicho kutoka Ubalozi wa ufalme wa Sweden na Norway katika kikao cha pamoja kilichofanyika leo na Wasaidizi wa kisheria (Paralegals) wa wilaya ya Mbinga mkoa wa Ruvuma katika Ofisi za wilaya hiyo zilizopo mtaa wa Mbuyula karibu na hospitali ya wilaya iliyopo mjini hapa.

Wasaidizi wa kisheria (Paralegals) kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu wilaya ya Mbinga mkoa wa Ruvuma, wakiwa katika kikao na viongozi wa LHRC kutoka jijini Dar es Salaam pamoja na Wafadhili wao wa Ubalozi wa ufalme wa Sweden na Norway, kikao ambacho kilifanyika katika Ofisi za kituo hicho zilizopo mtaa wa Mbuyula karibu na hospitali ya wilaya mjini hapa.
Wasaidizi wa kisheria (Paralegals) wilaya ya Mbinga mkoa wa Ruvuma leo wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kutoka jijini Dar es Salaam na Wafadhili wao wa kutoka Ubalozi wa ufalme wa Sweden na Norway katika Ofisi ya wilaya hiyo ya LHRC iliyopo mjini hapa.
Na Kassian Nyandindi,      
Mbinga.

KUFUATIA kushamiri kwa matukio ya watu kuchukua sheria mkononi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, Wasaidizi wa kisheria (Paralegals) Kituo cha Sheria na Haki za binadamu (LHRC) wilayani humo wamevitaka vyombo vya dola kuelimisha wananchi ili wasiendelee kufanya vitendo hivyo.

Wasaidizi hao walisema kuwa wananchi hao wamekuwa na tabia ya kuchukua sheria mkononi kwa kufanya vitendo vya kikatili ikiwemo mauaji, hasa pale wanapomkamata mhalifu ambaye anadaiwa kushiriki vitendo vya wizi kwa namna moja au nyingine.

Pia walieleza kwamba kufuatia uwepo wa jitihada za utoaji wa msaada wa kisheria na ushauri katika jamii wilayani humo, vitendo hivyo vimeanza kupungua na kwamba kinachotakiwa sasa ni Serikali kuendelea kuwaelimisha wananchi ili waachane na tabia hiyo.

Hayo yalisemwa leo na Wasaidizi hao wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu wilaya ya Mbinga mkoani humo, wakati walipokuwa kwenye kikao chao wakizungumza mbele ya Wafadhili wao wa kutoka Ubalozi wa ufalme wa Sweden ambao ni Anette Windolm Bolme, Alexandra Hallqvist na Ludviq Bontell Meneja wa miradi Ubalozi wa ufalme wa Sweden na Victor Mlunde kutoka Ubalozi wa ufalme wa Norway walipotembelea katika Ofisi za kituo hicho zilizopo mtaa wa Mbuyula jengo la Mwalimu house karibu na hospitali ya wilaya hiyo mjini hapa.

KUBENEA ASHIKILIWA NA POLISI

Dar es Salaam. 

MBUNGE wa Ubungo (CHADEMA), Saed Kubenea yupo mikononi mwa polisi akisubiri mchakato wa kusafirishwa kupelekwa mjini Dodoma kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.

Saed Kubenea.
Akizungumza kwa simu na Mwananchi leo Jumanne, Kubenea amesema yupo katika kituo cha polisi cha Oysterbay  wilayani Kinondoni na akisubiri utaratibu wa safari ya kwenda Dodoma kwa ajili ya kuhojiwa kama Spika wa Bunge Job Ndugai alivyoagiza.

Kubenea amesema awali kabla ya kushikiliwa alikwenda kujisalimisha polisi katika kituo hicho kisha aliambatana na askari hadi Katika Hospitali ya Aga Khan ambako alitakiwa kwenda kwa ajili ya kufanyiwa kipimo cha MRI.

Monday, September 18, 2017

WANANCHI WILAYA MBINGA WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA INAYOTOLEWA BURE MSAADA WA KISHERIA NA USHAURI

Mkuu wa Kituo cha Sheria na Haki za binadamu (LHRC) wilayani Mbinga, Daniel Chindengwike wa pili kutoka upande wa kulia akiwatambulisha wageni wa kituo hicho ambao ni wataalamu wa masuala ya kisheria kutoka jijini Dar es Salaam leo katika Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Mbinga kwa Katibu tawala wa wilaya hiyo, Mhandisi Gilbert Simya ambaye amevaa koti lenye rangi nyeusi.

Anna Henga wa pili kutoka kulia ambaye ni Mkurugenzi wa utetezi na maboresho kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) jijini Dar es Salaam, akisisitiza jambo kwa Wasaidizi wa kisheria (Paralegals) wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wakati alipowasili leo kwenye ofisi za kituo hicho wilayani humo.
Aliyesimama ambaye ni Reginald Martin mtaalamu wa kisheria na ushauri kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) jijini Dar es Salaam, leo akiwa katika ofisi za kituo hicho wilayani Mbinga akisisitiza jambo na kutoa muongozo wa namna watakavyotoa msaada wa kisheria na ushauri kwa muda wa siku tano kwa wananchi wa wilaya hiyo. 
Na Kassian Nyandindi,        
Mbinga.

WANANCHI wenye matatizo ya aina mbalimbali katika jamii yanayohitaji msaada wa kisheria na ushauri wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kuchangamkia fursa hiyo na kujitokeza kwa wingi ili waweze kupata msaada huo.

Aidha imeelezwa kuwa msaada utakaotolewa ni bure, hivyo watumie fursa hiyo kwenda katika Ofisi za Kituo cha sheria na haki za binadamu zilizopo mtaa wa Mbuyula, jengo la Mwalimu house karibu na hospitali ya wilaya hiyo iliyopo mjini hapa.

Mkurugenzi wa utetezi na maboresho kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) jijini Dar es Salaam, Anna Henga akiwa ameambatana na Wataalamu wenzake wa kisheria alisema hayo leo wakati alipokuwa akitoa utambulisho kwa Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Mbinga kwa Katibu tawala wa wilaya hiyo, Mhandisi Gilbert Simya.

Anna alifafanua kuwa kazi kubwa waliyokuja kuifanya wilayani humo ni kutoa msaada wa kisheria bure kwa wananchi, wakishirikiana na Wasaidizi wao wa kisheria (Paralegals) waliopo wilayani hapa kwa muda wa siku tano kuanzia Septemba 19 hadi 23 mwaka huu majira ya asubuhi hadi jioni.

MADIWANI NA MAOFISA WATENDAJI MBINGA WATAKIWA KUSIMAMIA UBORA WA KAHAWA

Wakulima wa kahawa wakianika kahawa kwenye vichanja kabla haijapelekwa sokoni kwa mauzo.
Na Dustan Ndunguru,     
Mbinga.

MADIWANI na Maofisa watendaji wa vijiji na kata katika maeneo yao wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wamesisitizwa kusimamia vyema ubora wa zao la kahawa kwa kuwahimiza wakulima kuzingatia ipasavyo kanuni bora za maandalizi ya zao hilo ikiwemo kuanika kahawa kwenye vichanja, na sio kama baadhi yao wanavyotandika mikeka chini na kuianika pale wanapoichuma kutoka shambani.

Onyo hilo limetolewa juzi na Mkuu wa wilaya hiyo, Cosmas Nshenye alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu kuhusiana na ubora wa zao hilo unavyopaswa kuzingatiwa kanuni zake za kilimo, hasa kipindi hiki cha msimu wa mavuno ya zao la kahawa unaondelea kufanyika wilayani humo.

Nshenye alisema kuwa kahawa ni zao ambalo limekuwa ni tegemeo kubwa kwa uchumi wa wananchi wa wilaya ya Mbinga, hivyo wakulima wanapaswa wakati wote kuzingatia maelekezo wanayopewa na wataalamu wa ugani juu ya utunzaji na uzalishaji wake wa zao hilo.

BALOZI WA FINLAND ASHANGAZWA NA VIVUTIO VYA UTALII ZIWA NYASA

Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

MSHAURI na Mwakilishi wa Balozi wa Finland nchini Tanzania, Kari Leppanen amefanya ziara ya siku mbili Mwambao mwa ziwa Nyasa mkoani Ruvuma.
Mwakilishi wa Balozi wa Finland Tanzania, Kari Leppanen.

Akihojiwa juzi kwenye Hoteli ya kitalii ya Watawa wa Mtakatifu Vincent iliyopo katika fukwe za Kilosa mjini Mbambabay wilayani humo, alisema kuwa ameshangazwa na vivutio vya utalii ambavyo ni vya kipekee na adimu havipatikani sehemu nyingine yoyote Duniani vilivyopo katika ziwa hilo.

Balozi huyo alisisitiza kuwa iwapo vivutio hivyo vikiendelezwa vitafungua fursa kubwa ya uwekezaji na utalii kwa wananchi wa eneo hilo na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.


Miongoni mwa vivutio vilivyopo katika ziwa Nyasa ni fukwe za asili, visiwa ambazo samaki wa mapambo aina zaidi ya 400 huzaliana kwa wingi, milima ya Livingstone, mawe ya ajabu kama vile jiwe la Pomonda na vivutio vingine vya Ikolojia na Utamaduni.

Sunday, September 17, 2017

MRADI PANDA MITI KIBIASHARA KUWANUFAISHA WANANCHI WA MBINGA




David Hyera ambaye ni Afisa misitu wa Halmashauri ya mji wa Mbinga akiwa katika eneo la kitalu cha miti Kihaha Mbinga mjini, ambalo linatumika kuzalisha miche ya Mikaratasi (Pines) na Milingoti (Eucalyptus) kwa ajili ya kuwagawia wananchi kwenda kuipanda.
Na Kassian Nyandindi,        
Mbinga.

MRADI wa Panda miti kibiashara ambao umeanzishwa katika Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, umeweza kuzalisha miche bora ya miti milioni 1.2 katika kitalu cha miti Kihaha kilichopo mjini hapa ambayo watagawiwa wananchi bure na kuipanda ili waweze kuondokana na umaskini.

Aidha imeelezwa kuwa miche hiyo itapandwa katika hekta 500 msimu wa mvua mwaka huu katika eneo la Lihumbe na Ukimo kata ya Mbangamao pamoja na Lipilipili kata ya Mpepai.

Imeelezwa kuwa lengo kuu la mradi huo ni kuwasaidia wananchi maskini ambao wamejiunga kwenye vikundi katika maeneo hayo, ili waweze kuinua kipato chao kwa njia ya panda miti kibiashara ambapo watagawiwa bure miti hiyo na kuipanda kwa njia ya kitaalamu ili baadaye waweze kuvuna mbao bora.

Mwandishi wa habari hizi ambaye alitembelea katika eneo la uzalishaji wa miche hiyo na kuzungumza na Afisa misitu wa halmashauri ya mji huo, David Hyera alisema kuwa miche ya miti iliyozalishwa kwenye kitalu hicho ni aina ya Milingoti (Eucalyptus) na Mikaratasi (Pines).

KIHUNGU WAIPONGEZA WIZARA YA ELIMU KWA KUIPATIA MAMILIONI YA FEDHA UJENZI VYUMBA VYA MADARASA

Na Dustan Ndunguru,    
Mbinga.

WANANCHI wa kata ya Kihungu, Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoa wa Ruvuma wameipongeza serikali ya awamu ya tano hapa nchini kupitia Wizara ya elimu, sayansi, teknolojia na ufundi kwa kuipatia shule ya msingi Kihungu iliyopo katika kata hiyo, shilingi milioni 66.6 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na vyoo vya shule hiyo.

Naibu wa Wizara ya elimu, Injinia Stella Manyanya.
Aidha imeelezwa kuwa hali hiyo itawawezesha wanafunzi wa shule hiyo kuweza kusoma katika mazingira mazuri na kuinua kiwango chao cha ufaulu wa masomo hasa pale wanapokuwa darasani.

Katika kikao kilichofanyika jana shuleni hapo na kuhudhuriwa na wazazi, walimu na wanafunzi hao walisema kuwa shule yao ambayo ilijengwa miaka ya tisini iliyopita na wananchi wenyewe ina vyumba vya madarasa na vyoo vilivyokuwa chakavu ambavyo sio rafiki kwa matumizi ya watoto hao.

Mashaka Lupogo ambaye ni mkazi wa kijiji hicho licha ya kuipongeza serikali alisema kuwa fundi ambaye amepewa jukumu la kujenga vyumba hivyo vya madarasa na vyoo hivyo anapaswa kutekeleza majukumu yake kwa umakini mkubwa ili ujenzi wa viwango vinavyotakiwa uweze kufikiwa kulingana na thamani halisi ya fedha iliyotolewa na serikali.

ZITTO KABWE AZUNGUMZA JUU YA KUUNGUA MOTO NYUMBA YAKE

Zitto Kabwe.
Na Mwandishi wetu,

MBUNGE wa Kigoma mjini, Zitto Kabwe amewataka wananchi kuwa watulivu wakati Jeshi la Polisi likiendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha moto ulioteketeza nyumba yake.

Nyumba hiyo iliteketea jana Jumamosi alasiri na hakuna madhara kwa binadamu yaliyotokea isipokuwa mali zote zilizokuwamo ndani zimeteketea.

“Tumepata ajali kidogo, nyumba yangu ninayoishi katika eneo la Kibingo, mji mdogo wa Mwandiga, Kigoma imeteketea kwa moto jioni hii. Alhamdulillah, kuwa hakuna binaadam aliyeumia”, aliandika Zitto katika ukurasa wake wa Facebook.

Saturday, September 16, 2017

WANANCHI WASHAURIWA KUEPUKA LUGHA ZA UPOTOSHAJI

Na Dustan Ndunguru,    
Mbinga.

WANANCHI wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma wametakiwa kuepuka kusikiliza kauli za watu wanaopita kwenye maeneo yao wanayoishi, ambao hutoa lugha za upotoshaji kuhusiana na matumizi ya dawa zinazotolewa na serikali katika jamii kwa ajili ya kuzuia na kutibu magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele.

Kauli hiyo imetolewa jana na Mratibu wa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele wa wilaya hiyo, Sebastian Mhagama wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi juu ya magonjwa hayo jinsi ambavyo yanavyoathiri jamii.

Mhagama alisema kuwa jitihada kubwa inaendelea kufanyika kila mwaka wilayani humo kutibu wale wote ambao huathirika sambamba na utoaji wa elimu kwa wananchi, ili kuwafahamisha namna ya kuepukana nayo lakini kikwazo kikubwa kimekuwa kutoka kwa baadhi ya watu ambao wamekuwa na tabia ya kuwakatisha tamaa wenzao wanaotumia dawa hizo.

WAKUU WA MIKOA NA WILAYA WATAKIWA KUSIMAMIA KIKAMILIFU UPATIKANAJI DAWA NA VIFAA TIBA

Dokta Khamis Kigwangala.
Na Waandishi wetu, 

WAKUU wa mikoa na wilaya hapa nchini, wametakiwa kusimamia kikamilifu upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kuanzia kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali ili wananchi waweze kupata huduma bora.

Agizo hilo limetolewa hivi karibuni na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dokta Khamis Kigwangala alipokuwa akifungua majengo ya kutoa huduma ya afya ya uzazi katika zahanati 26 mkoani Kigoma, shughuli iliyofanyika kijiji cha Mwakizega, wilaya ya Uvinza mkoa wa Kigoma.

Dokta Kigwangala alisema kuwa serikali imetenga shilingi bilioni 269 kwa ajili ya kununua dawa katika kipindi cha mwaka huu ambapo mwaka jana 2015 kiasi kilichotengwa kununua dawa hizo kilikuwa ni shilingi bilioni 31.

YANGA YAAMBULIA SARE MAJIMAJI SONGEA

Na Mwandishi wetu,
Songea.

MCHEZAJI, Donald Dombo Ngoma leo ameinusuru timu yake ya Yanga SC kupoteza mechi mbele ya Majimaji baada ya kuifungia bao la kusawazisha kipindi cha pili, timu hizo zikitoka sare ya bao 1-1 katika uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma katika mchezo wa Ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Ngoma alifunga bao la kusawazisha dakika ya 79 kwa kichwa akimalizia krosi ya Mzambia, Obrey Chirwa kumtungua kipa wa zamani wa Simba, Andrew Ntalla.

Hayo yalifuatia Majimaji kutangulia kwa bao la Peter Mapunda dakika ya 54 akimalizia pasi ya mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Jerson John Tegete kumtungua kipa Mcameroon Youthe Rostand.

Kipindi cha kwanza wenyeji Majimaji walitawala mchezo na kufika mara nyingi kwenye eneo la hatari la Yanga, lakini hawakuweza kufunga kutokana na utulivu wa safu ya ulinzi ya mabingwa hao watetezi chini ya beki mkongwe, Kelvin Yondan.

BREAKING NEWS: NYUMBA YA MBUNGE ZITTO KABWE YATEKETEA KWA MOTO


Nyumba ya Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo) iliyopo Mwandiga, mkoani Kigoma yadaiwa kuungua moto muda huu.