Sunday, September 17, 2017

MRADI PANDA MITI KIBIASHARA KUWANUFAISHA WANANCHI WA MBINGA




David Hyera ambaye ni Afisa misitu wa Halmashauri ya mji wa Mbinga akiwa katika eneo la kitalu cha miti Kihaha Mbinga mjini, ambalo linatumika kuzalisha miche ya Mikaratasi (Pines) na Milingoti (Eucalyptus) kwa ajili ya kuwagawia wananchi kwenda kuipanda.
Na Kassian Nyandindi,        
Mbinga.

MRADI wa Panda miti kibiashara ambao umeanzishwa katika Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, umeweza kuzalisha miche bora ya miti milioni 1.2 katika kitalu cha miti Kihaha kilichopo mjini hapa ambayo watagawiwa wananchi bure na kuipanda ili waweze kuondokana na umaskini.

Aidha imeelezwa kuwa miche hiyo itapandwa katika hekta 500 msimu wa mvua mwaka huu katika eneo la Lihumbe na Ukimo kata ya Mbangamao pamoja na Lipilipili kata ya Mpepai.

Imeelezwa kuwa lengo kuu la mradi huo ni kuwasaidia wananchi maskini ambao wamejiunga kwenye vikundi katika maeneo hayo, ili waweze kuinua kipato chao kwa njia ya panda miti kibiashara ambapo watagawiwa bure miti hiyo na kuipanda kwa njia ya kitaalamu ili baadaye waweze kuvuna mbao bora.

Mwandishi wa habari hizi ambaye alitembelea katika eneo la uzalishaji wa miche hiyo na kuzungumza na Afisa misitu wa halmashauri ya mji huo, David Hyera alisema kuwa miche ya miti iliyozalishwa kwenye kitalu hicho ni aina ya Milingoti (Eucalyptus) na Mikaratasi (Pines).


Hyera alisema kuwa upandaji wa miti hiyo ambao ni wa mbegu bora ukishafanyika kitaalamu uvunaji wake unakuwa ni wa muda mfupi tokea ipandwe ardhini tofauti na mtu ambaye hutumia mbegu za kienyeji.

Alifafanua kuwa miche aina ya Milingoti ikishapandwa uvunaji wake unakuwa ni wa ndani ya miaka mitano ambapo mpandaji anaweza kupata faida ya kuvuna nguzo, kama zile ambazo hutumiwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) tofauti na yule anayetumia mbegu za kienyeji huchukua muda wa zaidi ya miaka 10 mpaka kuanza kuivuna.

Pia aliongeza kuwa kwa yule ambaye hupanda miti aina ya Mikaratasi kwa kutumia mbegu bora uvunaji wake hutumia miaka 12 tu, tofauti na yule atakayetumia mbegu za kienyeji huchukua muda wa zaidi ya miaka 20 mpaka kuivuna.

“Kwa mwaka huu eneo la Lihumbe na Ukimo kata ya Mbangamao pamoja na Lipilipili kata ya Mpepai, mradi unakwenda kwenye vikundi vya wananchi na kupandwa miti hii bora katika hekta 500 zilizopo kwenye maeneo hayo”, alisema Hyera.

Alibainisha kuwa eneo hilo la upandaji ni la serikali na kwamba litabaki kuwa la serikali, lakini miti itakayopandwa itabaki kuwa mali ya wananchi wenyewe walioipanda ambao wataingia mkataba wa maelewano sio chini ya miaka 33 na halmashauri ya mji wa Mbinga.

Vilevile alieleza kuwa mkataba huo utawawezesha wananchi hao kupanda miti hiyo mpaka kuivuna, watapata kipato ambapo halmashauri hiyo na serikali kwa ujumla itaweza kupata ushuru wake kupitia mavuno yatakayofanyika kwenye miti hiyo na hatimaye kuweza kuboresha huduma za kijamii.

Hyera alisema kuwa mradi wa uzalishaji miche katika kitalu cha Kihaha unafanywa kwa ufadhili wa nchi ya Finland na kusimamiwa na Wakala wa mbegu za miti Tanzania chini ya usimamizi wa Afisa misitu huyo wa halmashauri ya mji wa Mbinga.


Kadhalika mradi huo tokea uanzishwe miaka minne iliyopita umeweza kusaidia kutengeneza ajira kwa wakazi wanaoishi karibu na eneo la kitalu hicho kufuatia malipo wanayolipwa kwa wale wanaofanya kazi za ugani, utunzaji wa vitalu na upandaji miti vijijini.

No comments: