Friday, September 15, 2017

MASASI WATAKIWA KUACHA TABIA YA KUUZA ARDHI WAJIKITE NA UZALISHAJI WA MAZAO YA CHAKULA NA BIASHARA

Na Dustan Ndunguru,      
Mbinga.

WANANCHI wa kijiji cha Masasi, wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wametakiwa kuacha tabia ya kuuza ardhi waliyonayo badala yake wajikite katika uzalishaji wa mazao mbalimbali ya chakula na biashara ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Mwito huo ulitolewa hivi karibuni na Katekista mstaafu, Raphael Mapunda wa Kanisa katoliki jimbo la Mbinga wakati alipokuwa akihubiri katika kigango cha Masasi ambapo pia alisisitiza kwa waumini wenzake juu ya umuhimu wa uwajibikaji ipasavyo katika maeneo yao ya kazi.

Mapunda alisema kuwa kuuza ardhi bila sababu ya msingi kutasababisha watoto wao wakumbane na changamoto ya kukosa maeneo ya kufanyia shughuli za kilimo siku za mbele, hivyo wazazi wanakilasababu ya kutunza rasilimali hiyo muhimu na kwamba kinachotakiwa ni kujikita zaidi katika mfumo mwingine wa kuweza kujipatia kipato badala ya kutegemea mauzo ya ardhi.


“Juzi nilisikitishwa sana pale mjini mara baada ya kukutana na mmoja kati ya mkazi wa hapa Masasi, akitangaza kuuza ardhi yake ambapo nilipomuuliza sababu hasa ya kuuza hakuwa na jibu la msingi nikamtaka arudi nyumbani kwake akatekeleze majukumu mengine badala ya kupoteza muda kutembea njiani kutangaza kuuza mali za watoto wake”, alisema Mapunda.

Alisema kuwa ardhi ni rasilimali muhimu katika jamii hivyo wanachotakiwa ni kuitumia vizuri kwa kuzalisha mazao ya chakula na biashara ambayo yakitunzwa vizuri kwa kuzingatia maelekezo yanayotolewa na maofisa ugani wataweza kupata mazao mengi na yenye ubora ambayo yana bei nzuri sokoni.

Mapunda alisema kuwa moja ya zao muhimu ambalo wananchi wa kijiji hicho wanapaswa kuanza kuzalisha ni kilimo cha mbaazi ambapo kwa sasa soko lake limekuwa kubwa hasa kwa nchi ya India na kwamba upatikanaji wa mbegu ni rahisi na kwamba kwa kuanzia anaendelea kuwasiliana na baadhi ya wadau wa zao hilo ili hatimaye kabla ya msimu wa mvua kuanza waweze kupata mbegu hizo na wananchi waweze kuanza kuzalisha.

Akizungumzia juu ya uwajibikaji alifafanua kuwa kila mmoja wao anapaswa kutekeleza majukumu yake kwa umakini na kwa uaminifu katika sehemu yake ya kazi, ili maendeleo yanayotarajiwa kufikiwa hapa nchini yaweze kupatikana kwa wakati na kwamba uzembe unapaswa kuepukwa kwa kila hali kwani kimekuwa ndicho chanzo kikuu cha umaskini miongoni mwa jamii.

“Niwaombe waumini wenzangu tuige mfano wa Rais wetu Magufuli, amekuwa mzalendo wa kweli kwa uwajibikaji wa hali ya juu anaouonyesha kwa taifa hili kama tutafuata nyayo zake tutashuhudia Tanzania mpya ikionekana hususan katika suala zima la maendeleo”, alisema Mapunda.


Katekista Mapunda aliwaasa viongozi kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji, kata, wilaya, mkoa na taifa kwa ujumla wahakikishe wanawajibika ipasavyo kwa kuonesha uaminifu hasa kwa rasilimali za taifa jambo ambalo kwa muda mrefu lilikuwa halifanyiki na kusababisha wachache kunufaika na rasilimali hizo huku walio wengi wakibaki maskini.

No comments: