Wednesday, September 6, 2017

RC RUVUMA AWATAKA WAKULIMA WA MAHINDI WASIKATE TAMAA

Na Mwandishi wetu,
Songea.

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Dokta Binilith Mahenge amewataka wakulima wanaozalisha zao la mahindi mkoani humo kuacha kukata tamaa kutokana na ukosefu wa soko la uhakika la kuuza zao hilo.

Aidha Dokta Mahenge alisisitiza kuwa badala yake wanatakiwa kuendelea na uzalishaji ili kuepuka uwezekano wa kutokea njaa ndani ya mkoa huo na jamii kukosa chakula.

Vilevile Mkuu huyo wa mkoa amewaomba wafanyabiashara wa ndani na nje ya mkoa huo kuunga mkono hatua ya serikali, kununua mahindi ya wakulima ambayo bado yanapatikana kwa bei ndogo ili kuweza kuwanusuru wakulima wasiweze kupata hasara.

Dokta Mahenge alitoa kauli hiyo jana wakati alipotembelea kituo cha ununuzi wa mahindi kijiji cha Mgazini kata ya Mgazini halmashauri ya wilaya ya Songea mkoani hapa.


Alisema kuwa serikali imepanga kununua tani 8,182 ndani ya mkoa wa Ruvuma, kiasi ambacho kinatajwa kuwa ni kidogo ikilinganishwa na uzalishaji mkubwa wa mahindi uliofanywa na wakulima wa mkoa huo.

Kadhalika alieleza kuwa serikali imepanga kununua kiasi hicho cha mahindi kwa ajili ya kuweka akiba ya chakula hasa pale itakapotokea njaa, hivyo wakulima nao ni lazima wachangamkie fursa ya kutafuta soko la ndani la kuuza mahindi yao kwa kuwa serikali haitakuwa na uwezo wa kununua mahindi yote yaliyozalishwa.

Kiwango hicho kinafuatia baada ya Wakala wa Hifadhi ya Chakula ya Taifa (NFRA) msimu uliopita alishindwa kufikia lengo lake la kununua mahindi licha ya kupangiwa kununua  tani 20,000 ambapo alifanikiwa kununua tani 10,000 tu ikilinganishwa na msimu wa mwaka 2015 ambapo alinunua tani 75,000 za mahindi Kanda ya Songea mkoani hapa.

“Lengo la serikali kuanzisha NFRA ni kwa ajili ya kununua mahindi kwa lengo la kuweka akiba, serikali haifanyi biashara kama baadhi ya watu wanavyofikiria tunawaomba wawekezaji wa ndani na nje kujenga viwanda vitakavyosaidia kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa na wakulima wetu”, alisema.

Pia Dokta Mahenge amemuagiza Meneja wa Wakala wa hifadhi ya chakula Kanda ya Songea kupunguza mgawo wa mahindi katika vituo vyenye mwitikio mdogo na kuelekeza nguvu kubwa katika maeneo ambayo kuna mwitiko mkubwa wa wakulima kupeleka mahindi yao.

“Nakuagiza maeneo ambayo wakulima hawachangamkii fursa hii ya kupeleka mahindi yao punguza mgawo na elekeza nguvu katika maeneo ambayo wakulima wameonesha mahitaji ya kupata fedha mimi ndiyo Mkuu wa mkoa nakuagiza tekeleza jambo hili”, alisisitiza Dokta Mahenge.

Naye kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Songea, Pololet Mgema alifafanua kuwa wilaya hiyo katika kipindi cha mwaka huu imepata mgao mdogo wa fedha ambao hauwezi kutosheleza mahitaji ya wakulima ambapo ameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuongeza fedha za kununulia mahindi hayo ili kuepusha wakulima wasiweze kupata hasara.

Meneja wa NFRA Kanda ya Songea, Amos Mtafya alisema kuwa ununuzi wa mahindi katika kanda hiyo ulianza rasmi mwezi Agosti mwaka huu ambapo kanda hiyo imepangiwa na serikali kununua tani 8,182 za mahindi.

Alisema kuwa katika mgawo huo halmashauri ya wilaya ya Namtumbo imepangiwa kununua tani 1400, Manispaa ya Songea tani 582, Songea vijijini kata ya Mgazini tani 2,000, Madaba tani 400, Mbinga mji tani 500, Mbinga vijijini tani 1,100 na Nyasa tani 200.


Mtafya alibainisha kwamba katika zoezi hilo changamoto kubwa ni ukosefu wa fedha kwani wakulima wamezalisha mahindi mengi na Wakala huyo hana uwezo wa kuyanunua yote na kwamba taarifa husika zimekwisha pelekwa NFRA makao makuu juu ya uwepo wa tatizo hilo ili kuweza kuona namna linavyotatuliwa na kuweza kuwaweka wakulima mahali pazuri.

No comments: