Monday, September 4, 2017

DAWA ZA NYWELE NI HATARI KWA AFYA YA WANAWAKE

DAWA za kulainisha nywele (Relaxer) ambazo zimekuwa zinapendwa na wanawake wengi wa Afrika kwa kuwa zina uwezo wa kulainisha nywele na kumfanya apendeze na awe wa kuvutia imeelezwa kuwa ni hatari kwa afya zao.

Wataalamu wa afya wanadai kuwa dawa hizo zinasababisha uvimbe kwenye kizazi kutokana na kemikali za dawa hizo huingia mwilini kupitia majeraha au ngozi wakati wa kupaka.

Daktari wa Manispaa ya Ilala, Laurent Chipata amefanya utafiti na kubaini kuwa dawa za nywele na vipodozi zina kemikali ambazo husababisha uzalishwaji wa vichocheo kwa kiasi kikubwa na kusababisha uvimbe kwenye kizazi uitwao Fibroids au Leimyoma.

“Kemikali hizi hupenya kwenye ngozi na wakati mwingine hata kwa harufu tu, husababisha kuzalishwa kwa wingi wa vichocheo aina ya Estrogen ambavyo huchangia kuota kwa uvimbe wa Fibroids,” alisema Dokta Chipata.


Dokta Chipata alisema kuwa kukua kwa uvimbe kwenye kizazi hutokea katika kipindi ambacho mama yupo kwenye uzazi yaani kabla hajakoma hedhi.

Utafiti wa Dokta Chipata ulifanywa nchini na kujumuisha wanawake wa kada tofauti tofauti wanaotumia dawa za nywele na wale wasiotumia na ukubwa wa tatizo hili ulibainika.

“Zipo kemikali tofauti tofauti zinazosababisha uvimbe kwenye kizazi, zipo za kwenye dawa za kilimo kama DDT na zile kwenye mafuta ya ngozi kama vile  Mercury na Hydroquionone,” alisema.

Alisema kuwa madhara yanayopatikana katika kemikali za vipodozi ni makubwa siyo tu kwenye kizazi bali nyingine husababisha Saratani au kufeli kwa figo. Anatoa mfano wa kemikali ya Zebaki (Mercury).

“Dawa za nywele zina madhara si lazima zipenye kwenye ngozi baada ya mtu kupata jeraha la kuungua bali zinaweza kupenya zenyewe kwenye ngozi kutokana na mfumo wa ngozi,” alisema Dokta Chipata.

Pia alishauri kuwa ni vyema watu wakasoma kwanza kipodozi kimetengenezwa kwa nini kabla ya kukitumia na kuongeza kuwa ni salama zaidi kubaki na ngozi au nywele halisi badala ya kujibadilisha.

Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imekataza vipodozi vyenye kemikali kama biothionol, hexachlorophene, mercury, vinylchloride, zirconium na bidhaa zenye aerosol, chloroquionone, steroids, methylene na chloroform.

Utafiti mwingine uliofanywa mwaka 2012 na Dokta Lauren Wise na wenzake nchini Marekani na kuchapishwa kwenye Jarida la afya la nchini Marekani ulibaini kuwa vipodozi vingi vina kemikali zenye vichocheo vya estrogen ambavyo kwa kawaida huchochea kasi ya kuota kwa uvimbe kwenye kizazi cha mwanamke na wakati mwingine kwenye mji wa mimba. Kitaalamu uvimbe au vivimbe hivi hujulikana kama Fibroids au Myoma.

Dokta Wise alisema kuwa aliwafanyia uchunguzi wanawake wanaotumia dawa za kulainisha nywele na kuangalia umri walioanza kutumia dawa hizo, mara ngapi, waliungua kiasi gani na walikaa na dawa hizo kichwani kwa kipindi gani.

Aliwafuatilia wanawake 23,580 wanaotumia dawa za kulainisha nywele na baada ya kipindi fulani walipimwa. Kati yao, 7146 waligundulika kuwa na uvimbe kwenye kizazi baada ya kupimwa kwa mionzi na wengine kufanyiwa upasuaji.

Kwa nini Relaxer ni hatari kwa wanawake?

Dokta Wise alifafanua kuwa mchanganyiko uliokwenye dawa za nywele hasa zilizoandikwa “Lye Relaxer” ni sodium hydroxide wakati makopo ya dawa yaliyoandikwa “No Lye Relaxer” yana calcium hydroxide na guanidine carbonate.


Bidhaa za kulainisha nywele zilizoandikwa ‘No lye relaxer’ zinadaiwa kusababisha majeraha kwa kiasi kidogo ukilinganisha na zile zilizoandikwa “Lye Relaxer”.

No comments: