Thursday, September 7, 2017

RAIS DOKTA MAGUFULI APOKEA TAARIFA YA UCHUNGUZI MADINI YA ALMASI NA TANZANITE IKULU JIJINI DAR ES SALAAM


RAIS Dokta John Pombe Magufuli amewataka viongozi mbalimbali wa Serikali ambao wametajwa kwenye ripoti za Bunge ya madini ya Almasi na Tanzanite, waachie ngazi mapema katika nafasi zao ili vyombo vya usalama viweze kufanya kazi yake vizuri katika kuwachunguza na kuwachukulia hatua za kisheria.

Kauli ya Rais huyo aliitoa leo wakati alipokuwa akikabidhiwa ripoti hizo Ikulu Jijini Dar es Salaam mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na viongozi wengine walioalikwa katika tukio hilo la makabidhiano ya ripoti hizo.

“Wapo watu wametajwa tajwa na wengine mimi ndio nilihusika kuwateua sasa ukishatajwa tajwa, naagiza vyombo vya ulinzi na usalama vifuatilie hili tena kwa haraka na wale ambao wametajwa kwenye ripoti hii ambao ni wateule wangu ili vyombo vya usalama viweze kufanya kazi yake vizuri ni matumaini yangu watakaa pembeni”, alisema Rais Magufuli.


Pia alieleza kuwa atashangaa kuona endapo watu waliotajwa kwenye sakata hilo la wizi wa madini hayo hawataanza kukamatwa na kwamba leo hii anataka wakamatwe.

Katika ripoti hiyo ambayo iliwasilishwa jana mjini Dodoma na hivi leo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kumkabidhi Rais Magufuli iliweza kuwataja baadhi ya viongozi wa serikali akiwemo Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) George Simbachawene, Waziri wa zamani wa Nishati na Madini na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja pamoja na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na viongozi wengine mbalimbali ambao Rais ameagiza washughulikiwe haraka.

Pamoja na mambo mengine Rais Magufuli alisema kuwa Profesa Abdulkadir Mruma ambaye pia alitajwa kwenye ripoti hizo alipandikizwa kwa maadui ili kuibua taarifa ya namna nchi inavyoibiwa madini.


No comments: