Friday, September 29, 2017

ONGEZEKO LA VIFO VYA UZAZI NCHINI LINASIKITISHA

Na Mwandishi wetu,

IMEELEZWA kuwa vifo vinavyotokana na uzazi vimeongezeka kutoka 432 kwa vizazi hadi laki moja katika kipindi cha mwaka 2012/2013 na kufikia 556 mwaka 2016/2017 sawa na akina mama 900 wanaopoteza maisha kila mwezi na 30 kila siku nchini wakati wanapojifungua.

Takwimu hizo zimetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa afya, Ummy Mwalimu alipokuwa akipokea mashine ya kisasa ya kutoa dawa ya usingizi wakati wa upasuaji, ambayo ilitolewa na taasisi ya utepe mweupe ambapo alisema katika kukabiliana na tatizo hilo ifikapo mwezi Juni mwaka 2018 Serikali itaongeza vyumba vya upasuaji kutoka 109 hadi kufikia 279 hapa nchini.

Akizungumza baada ya kukabidhi mashine hiyo Mratibu wa kitaifa wa taasisi ya utepe mweupe, Rose Mlay alisema kuwa ongezeko hilo la vifo linasikitisha na kwamba amemuomba Waziri Mwalimu kuhakikisha anaendelea kuweka mkazo katika suala la upatikanaji wa huduma za dharura na kwa haraka kwa akina mama wajawazito hasa katika maeneo ya vijijini.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dokta Mpoki Ulisubisya ambaye pia ni mtaalamu wa usingizi alielezea namna mashine hiyo inavyofanyakazi, uwezo wake na faida zake kwani haihitaji mitungi ya gesi wala umeme na ina uwezo wa kuonyesha viashiria vya hatari pale wakati inapotumika.


No comments: