Sunday, September 10, 2017

JKT MLALE WAISHUKURU SERIKALI KUREJESHA MAFUNZO YA VIJANA

Na Mwandishi wetu,

WAHITIMU wa mafunzo ya awali ya kijeshi Operesheni Tanzania ya viwanda kwa mujibu wa sheria 2017 waliohitimu mafunzo yao katika kikosi cha 842 Mlale JKT wilayani Songea mkoa wa Ruvuma, wameishukuru serikali kwa  kurejesha mafunzo ya vijana kwa mujibu wa sheria hatua ambayo itawezesha Taifa kuwa na viongozi wenye maadili, utiifu na watakaoitumikia nchi katika misingi inayofaa.

Katika risala yao iliyosomwa na Yusuph George na Magreth Masuki vijana hao walisema wakiwa katika mafunzo hayo wamejifunza mambo muhimu ambayo  ni pamoja na kuwasaidia  katika uzalishaji mali pamoja na ukakamavu, nidhamu, uwajibikaji, umoja na ushirikiano, utunzaji muda, kazi za mikono na malezi.

Aidha wameahidi kuendelea kushirikiana hata baada ya kumaliza mafunzo yao ili waweze kuwa na maendeleo endelevu miongoni mwao na Taifa kwa ujumla na kuwataka vijana wenzao wanapomaliza elimu ya kidato cha sita na kupata nafasi ya kujiunga na JKT kujifunza mambo yanayohusu uzalendo, tamaduni za Mtanzania, nidhamu na ukakamvu lakini sio kujiunga kwa lengo la kupata cheti bali uzalendo wa kweli katika nchi yao.


Kwa upande wake Mkuu wa mafunzo hayo Kapteni Hassan Bakari alisema kuwa mafunzo hayo yalifunguliwa mwezi Juni mwaka huu yakiwa na vijana 1,735 hata hivyo vijana waliofanikiwa kumaliza mafunzo walikuwa 1,710 kufuatia vijana 25 kushindwa kumaliza mafunzo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utoro.

Alisema kuwa mafunzo hayo yalichukua muda wa miezi mitatu ambapo wakati wote wa mafunzo vijana hao wamejifunza kwa nadharia na vitendo katika masomo mbalimbali ya mafunzo ya kijeshi kama mbinu za kivita, ujanja wa porini, usalama, utambuzi, elimu ya uraia na huduma ya kwanza.

Pia alisema katika mafunzo ya uraia wamejifunza namna ya kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi kwa kutii sheria bila shuruti, kufanya kazi kwa bidii, kutetea na kulinda katiba ya nchi na kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele katika kudumisha amani ya nchi na maendeleo yaliyokusudiwa na Serikali.

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa JKT ambaye pia ni afisa ustawi wa Jeshi hilo la taifa Kanali Anchilla Kagombola alisema kuwa Jeshi la kujenga taifa limepewa jukumu la kuwaanda vijana katika kuipenda na kuitetea na kuilinda nchi yao pamoja na kuwajengea uwezo katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali.

Alisema serikali itaendelea kuongeza mpango mkakati katika makambi yake ili JKT iweze kutekeleza adhima yake ya kuwajenga vijana waweze kuwa sehemu ya jamii itakayowezesha taifa letu kupiga hatua mbele katika uzalishaji mali na mkakati wa kukuza uchumi wa kufikia nchi ya viwanda.


Alisema kuwa serikali itaendelea kutoa mchango wake wa hali na mali katika kuboresha mafunzo kwa vijana wote watakaopata nafasi ya kujiunga na mafunzo kwa mujibu wa sheria na wale wa kujitolea huku akiwataka vijana waliomaliza mafunzo hayo kwenda kuonesha mfano bora katika jamii badala ya kushiriki na kujiunga katika makundi ya hovyo yanayoweza kuharibu sifa nzuri ya JKT.

No comments: