Saturday, September 16, 2017

YANGA YAAMBULIA SARE MAJIMAJI SONGEA

Na Mwandishi wetu,
Songea.

MCHEZAJI, Donald Dombo Ngoma leo ameinusuru timu yake ya Yanga SC kupoteza mechi mbele ya Majimaji baada ya kuifungia bao la kusawazisha kipindi cha pili, timu hizo zikitoka sare ya bao 1-1 katika uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma katika mchezo wa Ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Ngoma alifunga bao la kusawazisha dakika ya 79 kwa kichwa akimalizia krosi ya Mzambia, Obrey Chirwa kumtungua kipa wa zamani wa Simba, Andrew Ntalla.

Hayo yalifuatia Majimaji kutangulia kwa bao la Peter Mapunda dakika ya 54 akimalizia pasi ya mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Jerson John Tegete kumtungua kipa Mcameroon Youthe Rostand.

Kipindi cha kwanza wenyeji Majimaji walitawala mchezo na kufika mara nyingi kwenye eneo la hatari la Yanga, lakini hawakuweza kufunga kutokana na utulivu wa safu ya ulinzi ya mabingwa hao watetezi chini ya beki mkongwe, Kelvin Yondan.


Sifa zaidi zimuendee kipa Mcameroon, Rostand aliyeokoa michomo mingi ya hatari likiwemo shuti la mpira wa adhabu la Mapunda kutoka upande wa kushoto ambalo alilipangua pembezoni mwa lango juu na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Yanga walicheza kwa kasi nzuri ya kushambulia kwa dakika 10 tu za mwanzo, baada ya hapo wakalazimika kucheza kwa kuwadhibiti zaidi wenyeji walioanza kutawala mchezo.
Lakini dakika tano kuelekea mapumziko, Yanga nao wakaanza kuwasukuma langoni mwao Majimaji ambao nao walisimama imara kuondoa hatari zote upande wao.

Kipindi cha pili, Majimaji walikianza vizuri baada ya mabadiliko yaliyofanywa na kocha Habib Kondo akiwaingiza wakongwe, kiungo wa zamani wa Simba, Abdulhalim Humud na mshambuliaji Tegete kuchukua nafasi za Yakubu Kibiga na Danny Mrwanda.

Majimaji ikaenda kuuteka kabisa mchezo katika safu ya kiungo na kuanza kuwashambulia Yanga mfululizo kabla ya kupata bao la kuongoza.  Baada ya kufungwa, Yanga wakaamua kutoka kwenda kushambulia hadi kufanikiwa kupata bao la kusawazisha.

Na baada ya Yanga kusawazisha timu hizo zilianza kushabuliana kwa zamu, huku zikicheza kwa tahadhari zaidi ambapo Winga wa Yanga, Emmanuel Martin aliumia na kukimbizwa hospitali dakika ya 85 baada ya kugongana na mchezaji wa Majimaji, Marcel Kaheza.

Kwa matokeo hayo, Yanga inafikisha pointi tano baada ya kucheza mechi tatu, ikitoa sare mbili na kushinda moja, lakini Majimaji inafikisha pointi mbili baada ya kufungwa mechi moja na sare mbili.

Kikosi cha Majimaji kilikuwa; Andrew Ntala, Juma Salamba, Mpoki Mwakinyuke, Kennedy Kipepe, Tumba Sued, Hassan Hamisi, Suleiman Kassim ‘Selembe’, Yakubu Kibiga/Abdulhalim Humud dk46, Danny Mrwanda/Jerry Tegete dk46, Marcel Kaheza na Peter Mapunda.


Yanga SC; Youthe Rostand, Juma Abdul/Hassan Kessy dk65, Gardiel Michael, Andrew Vincent ‘Dante’, Kevin Yondan, Papy Kabamba Tshishimbi, Obrey Chirwa, Raphael Daudi, Donald Ngoma, Ibrahim Hajib na Geoffrey Mwashiuya/Eammnuel Martin dk75/Said Juma ‘Makapu’ dk85.

No comments: