Wednesday, September 20, 2017

SAKATA MRADI WA MAJI MKAKO MHANDISI MBINGA ASWEKWA LUPANGO

Na Kassian Nyandindi,   
Mbinga.

MHANDISI wa idara ya maji katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Vivian Mndolwa anashikiliwa na Jeshi la Polisi wilayani humo akituhumiwa kushiriki na wenzake, kuhujumu ujenzi mradi wa maji wa wananchi ambao serikali iligharimia shilingi milioni 718,896,533.

Vivian Mndolwa.
Aidha Mndolwa ambaye amewekwa Mahabusu katika Kituo kikuu cha Polisi cha wilaya hiyo tokea Septemba 19 mwaka huu anadaiwa kushindwa kusimamia mradi huo na kujengwa chini ya kiwango uliopo katika kitongoji cha Mnazi mmoja kijiji cha Mkako kata ya Mkako wilayani hapa.

Akizungumza leo na mwandishi wa habari hizi, Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma Germin Mushy amethibitisha kushikiliwa kwa Mhandisi huyo na kueleza kuwa mpaka sasa bado yupo mahabusu na kwamba kuna wenzake ambao wanatafutwa na jeshi hilo, walioshiriki kwa namna moja au nyingine kuhujumu mradi huo ili waweze kukamatwa na kuunganishwa katika shauri hilo na hatimaye watafikishwa Mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Mushy alieleza kuwa kutokana na taratibu za kiuchunguzi bado hazijakamilika hataweza kuwataja watu hao wanaotafutwa na kwamba aliongeza kuwa taarifa kamili za tukio hilo zitatolewa baadaye.


“Mradi wa maji Mkako ulishindwa kufunguliwa au kuzinduliwa na mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa kwa sababu ulikuwa hauendani na viwango vinavyotakiwa na huyu Mhandisi wa maji ndiye mhusika wa mradi huu”, alisema Mushy.

Aliongeza kuwa uhusika wake katika mradi huo bado unachunguzwa hivyo taratibu za kupewa dhamana zitatolewa baadaye, mara baada ya Polisi kukamilisha kazi yake na Jalada la kesi hiyo kupelekwa kwa Mwanasheria mkuu wa Serikali kwa hatua zaidi.

Baadhi ya wananchi wa kata ya Mkako wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wetu kwa kuomba majina yao yasitajwe walisema kwamba wameshangazwa na Serikali kwa kutochukua hatua za haraka mapema licha ya kulalamikia jambo hilo kwa muda mrefu, hadi ilipofikia hatua ya kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Amour Hamad Amour kutoa agizo lake Mei 8 mwaka huu kwa kumtaka Mkuu wa wilaya hiyo, Cosmas Nshenye aunde Kamati ya kuchunguza mradi huo na hatua za kisheria zichukuliwe haraka iwezekanavyo.

Walisema kuwa mradi huo ulianza kujengwa Machi 28 mwaka 2014 chini ya ufadhili wa benki ya dunia ambapo ilibidi ujenzi wake ukamilike mapema katika kipindi cha mwaka mmoja tangu uanze kujengwa, lakini inashangaza kuona kwamba hadi kufikia kipindi cha mwaka huu 2017 ujenzi huo bado haujakamilika na sehemu kubwa ya fedha za mradi huo zimekwisha tumika.

Kampuni iliyohusika na kazi ya ujenzi huo imetajwa kuwa ni ya Patty Interplan ya kutoka Jijini Dar es Salaam, na kwamba matumizi ya fedha hizo katika mradi huo wa maji zinadaiwa kutumika vibaya ndiyo maana mradi umejengwa chini ya kiwango na wananchi wanaendelea kukosa huduma ya maji safi na salama.

No comments: