Sunday, September 17, 2017

KIHUNGU WAIPONGEZA WIZARA YA ELIMU KWA KUIPATIA MAMILIONI YA FEDHA UJENZI VYUMBA VYA MADARASA

Na Dustan Ndunguru,    
Mbinga.

WANANCHI wa kata ya Kihungu, Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoa wa Ruvuma wameipongeza serikali ya awamu ya tano hapa nchini kupitia Wizara ya elimu, sayansi, teknolojia na ufundi kwa kuipatia shule ya msingi Kihungu iliyopo katika kata hiyo, shilingi milioni 66.6 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na vyoo vya shule hiyo.

Naibu wa Wizara ya elimu, Injinia Stella Manyanya.
Aidha imeelezwa kuwa hali hiyo itawawezesha wanafunzi wa shule hiyo kuweza kusoma katika mazingira mazuri na kuinua kiwango chao cha ufaulu wa masomo hasa pale wanapokuwa darasani.

Katika kikao kilichofanyika jana shuleni hapo na kuhudhuriwa na wazazi, walimu na wanafunzi hao walisema kuwa shule yao ambayo ilijengwa miaka ya tisini iliyopita na wananchi wenyewe ina vyumba vya madarasa na vyoo vilivyokuwa chakavu ambavyo sio rafiki kwa matumizi ya watoto hao.

Mashaka Lupogo ambaye ni mkazi wa kijiji hicho licha ya kuipongeza serikali alisema kuwa fundi ambaye amepewa jukumu la kujenga vyumba hivyo vya madarasa na vyoo hivyo anapaswa kutekeleza majukumu yake kwa umakini mkubwa ili ujenzi wa viwango vinavyotakiwa uweze kufikiwa kulingana na thamani halisi ya fedha iliyotolewa na serikali.


Vilevile naye Aderick Komba na Romwald Komba walisema kwa nyakati tofauti kuwa wale viongozi wenye jukumu la kusimamia ujenzi huo pia wanapaswa kuhakikisha kwamba, malengo husika yanafikiwa ili kuwepo na matumizi mazuri ya fedha hizo na kwamba wao kama wananchi hawatasita kutoa taarifa sehemu husika pale watakapobaini uwepo wa dalili za matumizi mabaya ya fedha hizo.

Mtaalamu wa majengo wa halmashauri ya mji wa Mbinga ambaye ni msimamizi mkuu wa ujenzi wa miundombinu hiyo ya shule ya msingi Kihungu, Jordan Kapinga alisema kuwa atahakikisha anatekeleza majukumu yake ipasavyo ili hatimaye yaweze kupatikana majengo yenye ubora unaotakiwa.


Naye fundi aliyepewa jukumu la ujenzi wa shule hiyo, Valence Urio alithibitisha kuwa atatekeleza jukumu hilo alilopewa na serikali kwa ufanisi mzuri ili hatimaye vyumba hivyo vya madarasa na vyoo viweze kukamilika ujenzi wake kwa wakati na viwango vinavyotakiwa na hatimaye miundombinu yake iweze kudumu kwa miaka mingi kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.

No comments: