Tuesday, September 5, 2017

WANAFUNZI 917,072 WANAOHITIMU DARASA LA SABA KUHENYEKA KESHO

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania, Dokta Charles Msonde. 
Na Mwandishi wetu,

BARAZA la Mitihani Tanzania (NECTA) limetishia kuvifutia usajili vituo vyote vya kufanyia mitihani ya darasa la saba inayotarajiwa kuanza kufanyika kesho Septemba 6 hadi 7 mwaka huu hapa nchini.

Katibu Mtendaji wa NECTA Dokta Charles Msonde alisema hayo leo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya ofisi za Baraza hilo la mitihani Mikocheni Jijini Dar es Salaam.

Msonde alisisitiza kuwa Baraza hilo linawataka wamiliki wa shule zote hapa nchini kutambua kwamba, shule zao ni vituo maalum vya kufanyia mitihani hivyo hawatakiwi kwa namna yoyote ile kuingilia majukumu ya wasimamizi wa mitihani hiyo.


“Baraza halitasita kukifuta kituo chochote cha mitihani endapo litabaini na kuthibitisha pasina shaka kuwa kituo hicho kinajihusisha na udanganyifu wa mitihani, tunatoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano kwa kipindi hiki cha ufanyikaji wa mitihani ili wanafunzi wafanye kwa utulivu”, alisema.

Vilevile aliwaasa walimu, wamiliki wa shule, wasimamizi na jamii kwa ujumla kutojihusisha na udanganyifu wa aina yoyote ile na kwamba kwa wale watakaokiuka watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za nchi.

Awali alifafanua kuwa wanafunzi hao watafanya masomo matano ambayo ni Kiswahili, Hisabati, Maarifa ya Jamii, Sayansi na somo la Kingereza ambapo mitihani hiyo mpaka sasa imekwisha safirishwa na kupelekwa katika vituo husika.

Watahiniwa 917,072 kutoka shule za msingi 16, 583 ndiyo wanaotarajia kufanya masomo hayo ambapo kati ya wanafunzi hao, wavulana ni 432,744 sawa na asilimia 47.19, wakati wasichana ni 484,328 sawa na asilimia 52.81.

Watahiniwa 882,249 watafanya mtihani huo kwa lugha ya Kiswahili na 34,823 watatumia lugha ya Kiingereza.

Jumla ya watahiniwa 94 wasioona wamesajiliwa kufanya mtihani huo, wakiwemo wavulana 58 na wasichana 36.

Dokta Msonde alisema kuwa maandalizi yamekwisha kamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa vifaa vinavyohitajika katika halmashauri zote nchini.

Pia amezitaka halmashauri kuhakikisha utaratibu wa uendeshaji wa mitihani hiyo unazingatiwa kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa.


No comments: