Friday, September 15, 2017

POLISI KUWASHUGHULIKIA WATUMIAJI WA MITANDAO

Na Mwandishi wetu,

MSEMAJI wa Jeshi la Polisi hapa nchini, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) Barnabas Mwakalukwa amewataka wananchi wanaofanyiwa vitendo vya uhalifu mitandaoni wasiende Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), bali wanapaswa haraka kutoa taarifa katika jeshi hilo ili wahalifu waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
ACP Barnabas Mwakalukwa.

Mwakalukwa alisema hayo leo alipokuwa akizungumza katika mkutano wa pamoja na viongozi wa Mamlaka hiyo, kuhusu suala zima la uhalifu wa makosa ya mitandao ambapo hivi sasa linaonekana kuendelea kushika kasi kubwa.

Alisema kuwa chochote kinachofanyika ambacho ni kosa la jinai kwa watoa huduma wa mitandao ya simu mbalimbali wananchi wanapaswa kwenda katika kituo cha Polisi kutoa taarifa ili waweze kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya kisheria kwa hatua zaidi.

Vilevile aliongeza kuwa kutokana na kukua kwa teknolojia hivi sasa vitu vingi vimekuwa vikifanyika 'online' hivyo mitandao ya kijamii imeonekana ni muhimu kwa maendeleo, lakini pia imebadilisha mbinu ya kufanya uhalifu katika mitandao ya kijamii kwa kutumiwa na baadhi ya watu kutapeli, hata kutishia kuua, hivyo jeshi la Polisi limejipanga kikamilifu kwa ajili ya kushughulikia makosa ambayo yanatokana na mtandao.


Hata hivyo kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa TCRA, Thadayo Ringo naye alilishukuru jeshi la Polisi hapa nchini kwa kuweza kuwasaidia katika kutatua changamoto mbalimbali hasa za kiusalama, huku akiwataka wananchi watakaopata matatizo katika mtandao kwenda kutoa taarifa Polisi ili waweze kuwasaidia kabla ya kufika kwao.

No comments: