Wednesday, September 20, 2017

GILBERT: KWA NIABA YA SERIKALI MBINGA BINAFSI NAKUBALIANA NA UTENDAJI KAZI MZURI WA PARALEGALS

Wafadhili Anette Widholme Bolme, Alexandra Hallqvist na Ludviq Bontell ambao ni Meneja miradi kutoka Ubalozi wa ufalme Sweden na Victor Mlunde Meneja miradi kutoka Ubalozi wa ufalme wa Norway wakiwa katika Ofisi ya Katibu tawala wa wilaya ya Mbinga mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Gilbert Simya ambaye upande wa kulia amevaa koti rangi nyeusi walipomtembelea leo kwa lengo la kufahamiana.

Mfadhili Victor Mlunde Meneja miradi kutoka Ubalozi wa ufalme wa Norway aliyeshika kalamu akisoma taarifa akiwa na wafadhili wenzake katika Ofisi ya Katibu tawala wa wilaya ya Mbinga mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Gilbert Simya kutoka kushoto aliyevaa koti rangi nyeusi walipomtembelea leo kwa lengo la kufahamiana.


Wafadhili Anette Widholme Bolme, Alexandra Hallqvist na Ludviq Bontell ambao ni Meneja miradi wa Ubalozi wa ufalme Sweden na Victor Mlunde Meneja miradi kutoka Ubalozi wa ufalme wa Norway upande wa kushoto, wakiwa katika picha ya pamoja na Wasaidizi wa kisheria (Paralegals) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma walipotembelea leo katika kijiji cha Lituru kata ya Litembo wilayani humo.
Na Kassian Nyandindi,    
Mbinga.

SERIKALI wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma imesema kwamba, wanakubaliana na utendaji kazi wa Kituo cha msaada wa Kisheria na Haki za Binadamu (LHRC) kilichopo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kufuatia Wasaidizi wake wa kisheria (Paralegals) kutekeleza majukumu yao ya kazi kwa misingi na taratibu husika zilizowekwa.

Hayo yalisemwa na Katibu tawala wa wilaya hiyo, Mhandisi Gilbert Simya alipokuwa akizungumza Ofisini kwake na wageni kutoka Ubalozi wa Sweden na Norway Tanzania ambao ndiyo Wafadhili wanaoendesha na kufanikisha shughuli za msaada wa kisheria katika Kituo cha sheria na haki za binadamu wilayani hapa.

Leo Septemba 20 mwaka huu Wafadhili waliotembelea kwa Katibu tawala huyo ni Anette Widholme Bolme, Alexandra Hallqvist na Ludviq Bontell ambao ni Meneja wa miradi Ubalozi wa ufalme Sweden na Victor Mlunde wa kutoka Ubalozi wa ufalme wa Norway.

“Kwa niaba ya serikali Mbinga binafsi nakubaliana na utendaji kazi mzuri wa hawa wenzetu Paralegals, kwa sababu asilimia kubwa ya watu wetu wa Mbinga hawajui masuala ya kisheria na namna ya kupata haki zao za msingi”, alisema Simya.


Kwa upande wake Anette Widholme Bolme akihoji kwa niaba ya wenzake alipotaka ufafanuzi juu ya namna Wasaidizi hao wa kisheria wanavyoshirikiana na vyombo vya serikali wilayani humo, Katibu tawala huyo alifafanua kuwa wamekuwa wakiishirikisha serikali ipasavyo hususan katika hata mafunzo mbalimbali yanayotolewa pale wanapokuwa wakielimisha wananchi au jamii katika eneo fulani.

Vilevile alipotaka kujua juu ya masuala gani ambayo yameshamiri wilayani Mbinga na kuwa kikwazo katika kuleta migogoro katika jamii, Simiya alisema kuwa kwa wilaya hiyo kumekuwa hasa na matatizo katika masuala ya ardhi, familia (watoto), ndoa na makosa ya jinai ambayo wananchi muda mwingi wanahitaji msaada wa karibu wa kisheria.

Kadhalika wageni hao walipozungumza na Afisa maendeleo ya jamii wa wilaya hiyo, Paschal Ndunguru aliwaeleza kuwa watu wengi hivi sasa wamekuwa wakikimbilia kwa Wasaidizi wa kisheria kituo cha Mbinga, kwa sababu ya kupata huduma nzuri na kuona wanafanikiwa katika masuala yao.

“Hawa Wasaidizi wa kisheria wananchi hapa kwetu wamekuwa wakiwakubali kwa utendaji wao mzuri wa kazi jinsi wanavyosaidia wanambinga wenzao”, alisema Ndunguru.

Alisema kuwa halmashauri ya wilaya inatambua kuwa tatizo kubwa linalokabili mashirika yasiyokuwa ya kiserikali ni ukosefu wa fedha za kuweza kuendeshea shughuli za kusaidia wananchi, ikiwemo kufikisha elimu husika katika jamii kama vile masuala ya kupambana na maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ukimwi (HIV), jinsia na kuzuia tatizo la watoto wa shule za sekondari wasiweze kupata ujauzito.

Ndunguru alisema katika kupunguza matatizo hayo halmashauri imekuwa ikitenga fedha katika bajeti zake kila mwaka na pale inapofanikiwa fedha kidogo hupita kwa wananchi kuelimisha jamii namna ya kuweza kudhibiti hali hiyo. (Family care)

Pamoja na mambo mengine, kwa upande wao wageni hao kwa nyakati tofauti waliahidi kuendelea kushirikiana na Wasaidizi wa kisheria wa wilaya ya Mbinga, ili kuweza kutatua migogoro mbalimbali ambayo inaendelea kuitesa jamii hasa kwa wale watu wanaoishi vijijini. 

No comments: