Monday, September 18, 2017

WANANCHI WILAYA MBINGA WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA INAYOTOLEWA BURE MSAADA WA KISHERIA NA USHAURI

Mkuu wa Kituo cha Sheria na Haki za binadamu (LHRC) wilayani Mbinga, Daniel Chindengwike wa pili kutoka upande wa kulia akiwatambulisha wageni wa kituo hicho ambao ni wataalamu wa masuala ya kisheria kutoka jijini Dar es Salaam leo katika Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Mbinga kwa Katibu tawala wa wilaya hiyo, Mhandisi Gilbert Simya ambaye amevaa koti lenye rangi nyeusi.

Anna Henga wa pili kutoka kulia ambaye ni Mkurugenzi wa utetezi na maboresho kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) jijini Dar es Salaam, akisisitiza jambo kwa Wasaidizi wa kisheria (Paralegals) wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wakati alipowasili leo kwenye ofisi za kituo hicho wilayani humo.
Aliyesimama ambaye ni Reginald Martin mtaalamu wa kisheria na ushauri kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) jijini Dar es Salaam, leo akiwa katika ofisi za kituo hicho wilayani Mbinga akisisitiza jambo na kutoa muongozo wa namna watakavyotoa msaada wa kisheria na ushauri kwa muda wa siku tano kwa wananchi wa wilaya hiyo. 
Na Kassian Nyandindi,        
Mbinga.

WANANCHI wenye matatizo ya aina mbalimbali katika jamii yanayohitaji msaada wa kisheria na ushauri wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kuchangamkia fursa hiyo na kujitokeza kwa wingi ili waweze kupata msaada huo.

Aidha imeelezwa kuwa msaada utakaotolewa ni bure, hivyo watumie fursa hiyo kwenda katika Ofisi za Kituo cha sheria na haki za binadamu zilizopo mtaa wa Mbuyula, jengo la Mwalimu house karibu na hospitali ya wilaya hiyo iliyopo mjini hapa.

Mkurugenzi wa utetezi na maboresho kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) jijini Dar es Salaam, Anna Henga akiwa ameambatana na Wataalamu wenzake wa kisheria alisema hayo leo wakati alipokuwa akitoa utambulisho kwa Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Mbinga kwa Katibu tawala wa wilaya hiyo, Mhandisi Gilbert Simya.

Anna alifafanua kuwa kazi kubwa waliyokuja kuifanya wilayani humo ni kutoa msaada wa kisheria bure kwa wananchi, wakishirikiana na Wasaidizi wao wa kisheria (Paralegals) waliopo wilayani hapa kwa muda wa siku tano kuanzia Septemba 19 hadi 23 mwaka huu majira ya asubuhi hadi jioni.


Alisema kuwa masuala watakayohudumiwa wananchi wenye matatizo ni pamoja na mashauri ya ndoa, ardhi, ajira, taratibu za kimahakama, uandaaji wa nyaraka na mikataba ya madai mbalimbali, mirathi, sheria za mtoto, bima, ushauri katika kesi za jinai na mengineyo yanayohusiana na masuala ya kisheria.

Vilevile aliongeza kuwa LHRC wamekuwa wakitembelea na kutoa huduma katika wilaya ambazo kuna wasaidizi wao wa kisheria na haki za binadamu na kwamba kuna wilaya 30 hapa nchini ambazo wananchi tayari wamekuwa wakipata huduma hizo kutoka katika kituo hicho.

Kadhalika kwa muda wa siku hizo pia watakuwa wakitoa huduma kwa wananchi wengine waliopo katika kata ya Litembo, Mapera, Matiri, Kigonsera, Utiri, Mbinga mjini na Mpapa zilizopo wilayani humo.

“Kwa mwaka tunatembelea wilaya tatu mpaka nne na mpango wetu wa baadaye ni kupanua huduma zetu kwa kuweza kuwafikia wananchi waliopo kwenye wilaya zote zilizopo hapa Tanzania”, alisema Henga.

Pia alieleza kuwa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu huu ni mwaka wa 22 sasa hapa Tanzania tokea waanze shughuli hizo, ambapo kwa mwaka hutoa msaada wa kisheria na ushauri kwa watu 12,000.

Naye kwa upande wake Katibu tawala wa wilaya ya Mbinga, Simya alifurahishwa na ujio wa wageni hao wa kutoa huduma hizo za kisheria na kueleza kuwa, watakuwa ni msaada mkubwa katika kutatua migogoro mbalimbali ikiwemo ya ardhi ambayo imeshamiri wilayani hapa.

“Ninyi mtakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wetu, tunaomba mshirikiane na Ofisi hii ya Mkuu wa wilaya mtusaidie kuhamasisha watu wajitokeze kwa wingi ili tuweze kusuluhisha migogoro iliyopo ndani ya jamii”, alisema Simya.

No comments: