Friday, September 1, 2017

TAMISEMI YATOA MAMILIONI YA FEDHA KUKARABATI SHULE YA WASIOONA SONGEA

Hili ni moja kati ya majengo ya shule ya msingi Luhira katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma ambayo yanakarabatiwa baada ya kupata fedha kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Na Kassian Nyandindi,  
Songea.

OFISI ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeipatia Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, zaidi ya shilingi milioni 151 kwa ajili ya kazi ya ujenzi na ukarabati wa shule ya msingi ya watoto walemavu wasioona iliyopo Luhira katika Manispaa hiyo.

Aidha mradi huo imeelezwa kuwa unahusisha ujenzi wa mabweni matatu, vyoo vya ndani ya mabweni ya shule hiyo vyenye matundu 18, shimo la choo la nje na ukarabati wa darasa moja ikiwemo uezekaji wa majengo mawili ya madarasa.

Mradi huo ambao mkandarasi wake ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ulianza Aprili 20 mwaka huu na unatarajia kukamilika ifikapo Oktoba 20 mwaka huu na kwamba shule ya msingi Luhira ina wanafunzi mchanganyiko ambao ni wale wanaoona na wasioona.


Kwa mujibu wa maelezo ya Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule hiyo, Gisbert Ndunguru alisema jumla ya wanafunzi wanaoona wapo 1,411 ambapo kati yao wasichana 672 na wanaume 739.

Ndunguru alieleza kuwa shule hiyo ina kitengo pia kwa ajili ya watoto wasioona nchini ambacho kilianzishwa mwaka 1982 hata hivyo shule ya msingi Luhira ni miongoni mwa shule kongwe nchini, ilianzishwa mwaka 1929 na kwamba Waziri Mkuu wa kwanza wa Tanzania Hayati Rashid Kawawa alisoma na kupata elimu yake ya msingi katika shule hiyo.

Naye Mkuu wa kitengo cha wanafunzi wasioona katika shule hiyo ambaye pia ni mlemavu wa macho, Salum Hapendeki alisema kitengo hicho kina wanafunzi 44 wasioona kati yao wavulana ni 19 na wasichana 25 na kwamba uwezo wa kitengo hicho ni kuchukua wanafunzi wasioona 60.

Afisa elimu maalum katika Manispaa ya Songea, Rehema Nyagawa alisema shule hiyo kwa muda mrefu imekuwa inakabiliwa na upungufu wa matundu ya vyoo hali ambayo ilikuwa ikisababisha watoto wa kiume kujisaidia choo kimoja na walimu.

Pia Nyagawa aliongeza kuwa shule ina majengo chakavu ambayo ni mabweni, jiko na bwalo la chakula na uchakavu wa magodoro na vitanda vya kulalia wanafunzi.

Kadhalika aliipongeza serikali kwa mradi wa ukarabati ujenzi wa mabweni na matundu ya vyoo ambao utapunguza changamoto hizo zilizokuwa kero kubwa na kuathiri mazingira ya watoto hao.

No comments: