Monday, September 25, 2017

HALMASHAURI MJI WA MBINGA WATILIANA SAINI NA WANANCHI MAKUBALIANO USIMAMIZI SHIRIKISHI WA UPANDAJI MITI

Mikataba ya makubaliano mradi wa Panda miti kibiashara ikisainiwa kati ya halmashauri ya mji wa Mbinga na wananchi wa kijiji cha Lipilipili kata ya Mpepai katika ukumbi wa halmashauri hiyo mjini hapa, ambapo mradi huo wa panda miti kibiashara unafadhiliwa hapa nchini na Wizara ya maliasili na utalii pamoja na serikali ya Finland kwa lengo la kuinua kipato cha wananchi.
Upande wa kushoto Mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Mbinga, Kipwele Ndunguru akimkabidhi mmoja kati ya wanakikundi mkataba wa makubaliano wa mradi wa Panda miti kibiashara baada ya kusainiwa pande zote mbili kati ya halmashauri na wananchi wa kijiji cha Lipilipili kata ya Mpepai, Anayeshuhudia aliyevaa shati rangi nyeupe ni Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Robert Mageni.

Baadhi ya wakulima wa kijiji cha Lipilipili (Upande wa kulia) katika halmashauri ya mji wa Mbinga wakikabidhiwa ramani ya eneo la mlima Lihumbe na Mwenyekiti wa halmashauri ya mji huo, Kipwele Ndunguru aliyevaa koti rangi nyeusi na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Robert Mageni aliyevaa shati rangi nyeupe ambapo ramani hiyo ndiyo inaonesha eneo la mlima huo ambao mradi wa panda miti kibiashara utaanza kutekelezwa msimu wa mvua kuanzia mwezi Novemba hadi Disemba mwaka huu. 
Na Kassian Nyandindi,   
Mbinga.

IMEELEZWA kuwa Tanzania ni nchi ambayo imekuwa ikiongoza kwa uzalishaji wa mazao ya misitu Afrika Mashariki na kati, kupitia mikoa ya Nyanda za juu kusini hivyo wananchi wanaoishi katika mikoa hiyo wanapaswa kuendelea kupanda miti ili iweze kuwasaidia kuinua kipato chao.

Hayo yalisemwa juzi na Mshauri wa maliasili mkoa wa Ruvuma, Afrikanus Chale wakati alipokuwa kwenye kikao cha makubaliano ya kutiliana saini juu ya usimamizi shirikishi wa upandaji miti aina ya Milingoti (Eucalyptus) na Mikaratasi (Pines) katika msitu wa Lihumbe uliopo kijiji cha Lipilipili kata ya Mpepai halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani humo.

Kikao hicho kilifanyika kwenye ukumbi wa halmashauri ya mji huo ambapo kilifuatia baada ya wananchi wanaoishi katika kijiji hicho kuikubali programu hiyo ambayo ni ya upandaji miti kibiashara kupitia vikundi vya wakulima wa miti chini ya uangalizi wa halmashauri hiyo.


Akizungumzia hilo Mshauri huyo wa maliasili alisema kuwa mradi huo wa panda miti kibiashara ni mradi ambao unatekelezwa na Serikali na kufadhiliwa kwa pamoja kati ya Wizara ya maliasili na utalii hapa nchini na Serikali ya Finland ambao utekelezaji wake ulianzia mwaka 2014 katika mkoa wa Njombe.

Chale alifafanua kuwa mradi huo umekuwa ukiendelea mkoani Ruvuma katika wilaya zake hususan kwa hapa Mbinga, ambapo lengo ni kuweza kusaidia vikundi vya wakulima ambavyo vimejikita katika shughuli za upandaji wa miti kwa namna ambayo ni bora zaidi ili waweze kupata tija hasa katika uzalishaji wa mazao yatokanayo na miti.

“Miti hii baadaye wananchi itawasaidia kuinua kipato chao, tunategemea itakapokomaa halmashauri na Serikali kwa ujumla itaweza kupata kipato wananchi wa Mbinga na maeneo jirani pia wataweza kunufaika kupitia mradi huu”, alisema.

Alifafanua kuwa msitu wa hifadhi ya Lihumbe una jumla ya hekta 797.94 ambazo ni sawa na ekari 1,994.85 ndizo zinazotarajiwa kupandwa miti na wananchi waliojiunga kwenye vikundi hivyo na kwamba kwa pamoja wamesaini mikataba ya makubaliano hayo kati ya wananchi hao na halmashauri hiyo kwa kipindi cha miaka 33.

Awali akizungumza katika kikao hicho cha makubaliano hayo Mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Mbinga, Kipwele Ndunguru alisema kuwa makubaliano hayo yanalenga kuwanufaisha wanavikundi wenyewe ambapo mradi utawapatia bure miche bora ya miti na kuipanda katika msitu huo.

Kipwele alisema kuwa miti hiyo ambayo watakwenda kuipanda inachukua muda mfupi kuivuna hivyo wanavikundi watanufaika pale itakapofikia hatua ya kukomaa na kuanza kuivuna kwa mfumo wa kupasua mbao au kuuza nguzo za umeme.


Hata hivyo alieleza kuwa shughuli za upandaji miti hiyo wanatarajia kuanza rasmi msimu wa mvua zitakapoanza mwaka huu mwezi Novemba hadi Disemba ambapo aliwataka wanavikundi kutunza mazingira kwa kuzuia vitendo vya uchomaji moto katika eneo ambalo miti hiyo itapandwa.

No comments: