Friday, September 1, 2017

DC SONGEA APIGA MARUFUKU MAENEO YALIYOTENGWA KWA SHUGHULI ZA UFUGAJI KUTUMIKA KWA KAZI YA KILIMO

Mkuu wa wilaya ya Songea Pololet Mgema, akiweka alama Ng’ombe wakati wa zoezi la uzinduzi wa usajili, utambuzi na ufuatiliaji wa mifugo katika shamba la mifugo kijiji cha Hanga kata ya Gumbiro halmashauri ya wilaya ya Madaba.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Madaba, Shafi Mpenda naye akiweka alama ya utambuzi wa Ng’ombe kwenye uzinduzi wa usajili, ufuatiliaji na utambuzi wa mifugo katika moja wapo ya shamba la mifugo kijiji cha Hanga ambapo jumla ya Ng’ombe 35,000 watawekewa alama hiyo ya utambuzi.
Na Mwandishi wetu,  
Madaba.

MKUU wa wilaya ya Songea Pololet Mgema amepiga marufuku maeneo yaliyotengwa kwa shughuli za ufugaji kutumika kwa kazi ya kilimo, badala yake wakulima watumie maeneo yao yaliyoainishwa na serikali zao za vijiji au kata kwa kazi hiyo.

Alisema serikali imekwisha maliza kazi ya kuainisha maeneo yote kwa ajili ya ufugaji na kilimo katika halmashauri mbalimbali za wilaya hivyo wanachopaswa kutekeleza ni kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kuepusha migogoro kati ya wakulima na wafugaji.

“Katika wilaya hii sitaki kusikia kuna migogoro kati ya wakulima na wafugaji kugombea masuala ya ardhi, serikali imekwisha maliza kuainisha maeneo yote kwa ajili ya shughuli za maendeleo naagiza kila mmoja wetu kuzingatia maelekezo haya”, alisema.

Mgema alisema hayo juzi wakati wa uzinduzi wa zoezi la usajili, utambuzi na ufuatiliaji wa mifugo katika kijiji cha Hanga kata ya Gumbiro halmashauri ya wilaya ya Madaba mkoani hapa.


Aliwataka pia wananchi kuheshimu mipaka iliyowekwa na sio kuingilia maeneo yaliyohifadhiwa na kuleta migogoro isiyokuwa na tija katika jamii ambayo inarudisha nyuma maendeleo yao na kuleta madhara makubwa.

Katika hatua nyingine Mgema, ameiagiza halmashauri ya wilaya ya Madaba kuhakikisha kwamba inatenga fedha za kutosha kwa ajili ya huduma za mifugo kama vile chanjo na ujenzi wa miundombinu husika katika maeneo ya ufugaji ili wafugaji waweze kufuga kisasa hatua ambayo itaweza kusaidia serikali kupata mapato yake.

Awali naye Mkurugenzi mtendaji wa wilaya hiyo, Shafi Mpenda akizungumza katika uzinduzi wa zoezi hilo alisema kuwa huo ni utekelezaji wa sheria ya Bunge namba 12 ya mwaka 2010 ambapo Serikali imeagiza Sekretarieti za mikoa kufanya utekelezaji huo kupitia halmashauri zake za wilaya.

Mpenda alieleza kuwa uzinduzi wa kupiga chapa mifugo kimkoa ulifanyika Julai 18 mwaka huu katika kijiji cha Matepwende halmashauri ya wilaya ya Namtumbo, ambapo mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dokta Binilith Mahenge aliagiza halmashauri zote nane za mkoa huo kukamilisha kazi hiyo kabla ya Septemba Mosi 2017.

Alisema kuwa kwa halmashauri ya Madaba imejitahidi kuhamasisha na kuelimisha wafugaji wake juu ya umuhimu wa zoezi hilo na wengi wameitikia wito huo kwa maendeleo ya ufugaji wenye tija.


Alibainisha kuwa kufuatia hali hiyo anayo imani kubwa kwamba, wataweza kuwa na daftari la kudumu lenye takwimu za mifugo ambalo litakuwa linaboreshwa kila baada ya miezi sita.

No comments: