Friday, September 15, 2017

WAZIRI MAHIGA ASEMA TANZANIA IMESHITUSHWA KUCHUNGUZWA NA UMOJA WA MATAIFA

Waziri wa mambo ya nje Tanzania, Dokta Augustine Mahiga.
Na Waandishi wetu,

TANZANIA imesema kwamba, imeshitushwa baada ya kuorodheshwa miongoni mwa nchi ambazo zimechunguzwa na Umoja wa Mataifa na kuhusishwa kuwa na uhusiano wa kibiashara na Korea Kaskazini.

Akizungumza leo katika mkutano na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Waziri wa mambo ya nje Dokta Augustine Mahiga alisema kuwa licha ya uhusiano uliokuwepo awali tangu mnamo mwaka 2014, Tanzania imepunguza kabisa uhusiano wa kibiashara na kidiplomasia na nchi hiyo.

“Hatuna ugomvi na Korea Kaskazini, lakini kitendo chao cha kutengeneza masilaha ya kuangamiza sio mazuri kwa heshima na usalama duniani, ndiyo maana tumeanza kuchukua hizo hatua za kupunguza mahusiano”, alisema Dokta Mahiga.


Waziri huyo aliongeza kuwa uhusiano huo wa kibiashara ulikuwepo kabla ya vikwazo vilivyowekwa hivi karibuni na Baraza la Umoja wa Mataifa.

Waziri Mahiga alifafanua kuwa anaelekea katika mkutano wa kawaida wa umoja wa Mataifa ambapo atatumia fursa hiyo kujibu tuhuma hizo kwa Baraza la usalama.

Tanzania na Uganda ni miongoni mwa baadhi ya nchi zinazochunguzwa na Umoja wa Mataifa kwa tuhuma za kwenda kinyume na vikwazo vilivyowekwa na Baraza la usalama la umoja wa Mataifa dhidi ya Korea Kaskazini.


Ripoti ya uchunguzi huo ilitolewa mnamo Septemba 9 mwaka huu ambapo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limesema kwamba, linachunguza tuhuma hizo za Tanzania kuingia mikataba ya kijeshi na Korea Kaskazini inayogharimu dola za Kimarekani milioni 12.5.

No comments: