Thursday, September 28, 2017

NHIF RUVUMA YAHIMIZA WANAMICHEZO KUCHANGAMKIA FURSA YA KUJIUNGA NA MPANGO WA MATIBABU

Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) mkoa wa Ruvuma, Abdiel Mkaro akikagua timu ya soka ya NHIF wakati wa bonanza maalum la kuhamasisha wanamichezo wa mkoa huo kuchangamkia fursa ya kujiunga na mfuko huo ili waweze kupata huduma bora za matibabu pale wanapougua.

Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) mkoa wa Ruvuma, Abdiel Mkaro upande wa kulia akikagua timu ya soka ya Makambi FC kabla ya kuanza mchezo wa kirafiki kati ya timu hiyo na timu ya NHIF katika bonanza la kuhamasisha wanamichezo wa mkoa huo na jamii kwa ujumla ili waweze kujiunga na mfuko huo.

Wafanyakazi wa NHIF mkoa wa Ruvuma Wakifanya mazoezi ya viungo wakati wa bonanza la kuhamasisha wanamichezo na jamii kuchangamkia fursa ya kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na Mfuko wa Afya ya Jamii CHF.

Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) mkoa wa Ruvuma, Abdiel Mkaro akikabidhi zawadi kwa mshindi wa mbio za kukimbiza kuku, Edwina Bilungi aliyekuwa upande wa kulia katika bonanza hilo lililofanyika mwishoni mwa wiki mjini hapa.
Na Mwandishi wetu,       
Songea.

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umewataka na kuwahimiza wanamichezo hapa nchini, kuchangamkia fursa ya kujiunga na mpango wa matibabu kupitia Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) na wa NHIF ili waweze kupata huduma bora za matibabu hasa pale wanapougua au kupata majeraha wanapokuwa michezoni.

Rai hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Meneja NHIF mkoani Ruvuma, Abdiel Mkaro wakati wa Bonanza maalum la kuhamasisha jamii hasa wana michezo wajiunge na mifuko hiyo ili waweze kuwa na afya bora pale wanapougua.

Pia aliwataka Watanzania wakiwemo waandishi wa habari, kuona umuhimu wa kijunga na mpango huo kwa lengo la kuwa na uhakika wa kupata matibabu pale inapotokea wanapata ajali na magonjwa mbalimbali.


Bonanza hilo liliandaliwa na NHIF kwa kushirikisha michezo ya aina mbalimbali kama vile kukimbia, mazoezi ya viungo, kukimbiza kuku pamoja na mpira wa miguu ambapo timu ya soka ya Mkambi FC ilifanikiwa kuibuka mshindi baada ya kuifunga timu ya NHIF magoli 4 kwa 2 kwa njia ya Penati baada ya matokeo ya awali kufungana 1 kwa 1 katika kipindi cha dakika 90 za mchezo huo.


Pamoja na mambo mengine bonanza hilo lililoonekana kuvutia watu wengi kutoka maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Songea, huku baadhi ya washiriki wakiomba Mfuko huo wa Taifa Bima ya Afya kuendelea kuandaa bonanza kama hilo kila mwisho wa mwezi ili kutoa fursa kwa wananchi wengi kushiriki na kufanya mazoezi ya mara kwa mara ili kuepusha uwezekano wa kupata magonjwa.

No comments: