Tangaza Biashara yako nasi kwa Matangazo ya aina mbalimbali, Mawasiliano zaidi piga simu namba 0762 578960
Friday, March 3, 2017
SERIKALI YAZUIA UCHIMBAJI MADINI KWENYE MTO MUHUWESI TUNDURU
Na Mwandishi wetu,
Tunduru.
SERIKALI hapa nchini imezuia shughuli za uchimbaji wa madini
ya vito katika mto Muhuwesi wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, hadi hapo taarifa
za kitaalamu zitakapotolewa mara baada ya kukamilika kwa zoezi la tathimini na
ukaguzi husika.
Agizo hilo la kuzuia kazi hiyo kufanyika katika mto huo limetolewa
hivi karibuni wilayani humo na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
alipofanya ziara yake kwenye mto huo ili kujionea hali ya eneo hilo kufuatia
ajali iliyosababisha kifo cha mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Kanje Ally na
majeruhi mmoja ambao waliingia na kuanza kuchimba ndani ya mto huo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisa madini mkazi wa wilaya ya Tunduru,
Mhandisi Fredrick Mwanjisi alisema kuwa zaidi ya watu sita walivamia eneo hilo
la mto kufanya shughuli za uchimbaji wa madini kinyume cha taratibu, kutokana
na kutokuwa na vibali vilivyowaruhusu kufanya shughuli hiyo ya uchimbaji katika
eneo hilo.
Tuesday, February 28, 2017
GOMBO SAMANDITO AWAKEMEA WALIMU WATORO KAZINI ASISITIZA ATAKAYEKAMATWA ATAMFUKUZA KAZI
Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
WALIMU wa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya
wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wametakiwa kuzingatia maadili ya kazi zao
ikiwemo kuacha vitendo vya ulevi na utoro kazini.
Aidha wamesisitizwa kuwahi na kuwa katika mazingira ya kazi
wakati wote na kufuata taratibu za kazi zao kwa mujibu wa nafasi walizonazo
kazini.
| Gombo Samandito. |
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya
wilaya hiyo, Gombo Samandito wakati alipokuwa akizungumza kwenye kikao cha
tathimini ya maendeleo ya elimu kilichofanyika kwenye ukumbi wa Kanisa Katoliki
Jimbo la Mbinga mjini hapa.
“Walimu mnatabia ya kuwa watoro kazini natambua mnajua kwamba
zikipita siku tano haupo kazini nakufukuza kazi, wakati wa kazi fanyeni kazi zenu
kwa kutekeleza ipasavyo majukumu mliyopewa mkayasimamie haya vizuri msiwe
sehemu ya matatizo”, alisisitiza Samandito.
Samandito alisisitiza pia kwa atakayepuuza maagizo yake hatua
kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake ikiwemo kufukuzwa kazi huku
akiongeza kuwa adui mkubwa wa maendeleo katika maisha ya kila siku ya binadamu
ni tabia ya mtu husika hivyo walimu hao wanapaswa kujiangalia kwanza wenyewe na
kubadilika mara moja kuwa na tabia nzuri kazini.
Monday, February 27, 2017
MAGHEMBE ASHANGAZWA NA UTAJIRI WA VIVUTIO VYA UTALII ZIWA NYASA
![]() |
| Wageni mbalimbali wakiwa katika eneo la viwanja vya Makumbusho ya Taifa ya Vita vya Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma. |
Songea.
WAZIRI wa Maliasili na Utalii,
Profesa Jumanne Maghembe ameshangazwa na utajiri wa vivutio vya utalii
vilivyopo katika mkoa wa Ruvuma, wakiwemo aina ya samaki wa mapambo zaidi ya
400 katika ziwa Nyasa mkoani humo na viumbe wengine adimu waliopo katika ziwa
hilo.
Kwa ujumla viumbe hao licha ya kuwa
ni adimu pia wamekuwa hawapatikani sehemu yoyote ile hapa duniani.
Profesa Maghembe alishangazwa na
hayo wakati alipokuwa akizungumza katika sherehe za kumbukizi ya miaka 110 ya
Vita vya Majimaji, zilizofanyika kwenye viwanja vya Makumbusho ya Taifa ya
Majimaji Songea mkoani hapa.
Alisisitiza kuwa ni fursa pekee
sasa, kuendelea kutangaza vivutio hivyo ili viweze kuleta tija kwa Taifa hili
kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho wakiwemo Wananyasa na mkoa wa Ruvuma
kwa ujumla.
MANISPAA SONGEA YAGAWA MICHE YA MATUNDA BURE KWA WATUMISHI WAKE
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
KATIKA kuhakikisha kwamba mazingira yanaendelea kuboreshwa
Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, idara ya kilimo katika Manispaa hiyo imegawa
bure miche bora ya matunda kwa watumishi wake wa idara mbalimbali.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Ofisa habari wa
Manispaa hiyo, Albano Midelo alisema kuwa uongozi wa Manispaa umefanya hivyo
kwa lengo la kuwajenga watumishi wake, kuwa na tabia ya mara kwa mara kupenda
kupanda miti ya matunda na miti mingine ya aina mbalimbali ili kusaidia kuhifadhi
mazingira na watu kuweza kupata matunda.
Midelo alifafanua kuwa Manispaa ya Songea, imenunua miche
bora ya matunda 2000 yenye thamani ya shilingi milioni 5,000,000 kutoka Chuo Kikuu
cha Kilimo cha Sokoine Morogoro (SUA).
VIONGOZI WA VYAMA VYA SIASA WATAKIWA KUJENGA USHIRIKIANO
Na Dustan Ndunguru,
Mbinga.
MWENYEKITI wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,
Ambrose Nchimbi amewataka viongozi wa kisiasa na watendaji katika maeneo
mbalimbali wilayani humo, kujenga ushirikiano katika kutekeleza majukumu yao na
kuacha kuendekeza malumbano badala yake wasimamie vyema ujenzi wa miradi ya
wananchi ili iweze kukamilika kwa wakati na viwango vinavyotakiwa.
Akizungumza na mwandishi wetu, Nchimbi alisema kuwa baadhi ya maeneo
wilayani humo miradi ya wananchi ya maendeleo imekwama haijakamilika kwa wakati
uliopangwa kutokana na tabia ya viongozi kuendekeza malumbano hasa
yanayochochewa na viongozi wa vyama vya siasa.
Alivinyoshea kidole vyama vya upinzani kutokana na tabia ya
viongozi wake kuwakatisha tamaa wananchi kwa kuwadanganya kuwa serikali
imewasahau kitu ambacho sio cha kweli.
Sunday, February 26, 2017
MWALIMU SHULE YA SEKONDARI KIAMILI MBINGA ATAFUTWA NA POLISI KWA KUMSHAMBULIA MWANDISHI WA HABARI
Na Mwandishi wetu,
Songea.
JESHI la Polisi mkoani Ruvuma linamtafuta Mwalimu wa shule ya
sekondari Kiamili wilaya ya Mbinga mkoani humo, Victor John Kayombo ambaye
amekimbia hajulikani wapi alipo kwa kosa la kumshambulia mwandishi wa habari,
kumpiga na kutaka kumjeruhi.
Kwa mujibu wa taarifa zilizomfikia mwandishi wa habari hizi zinaeleza
kwamba tukio hilo lilitokea Februari 24 mwaka huu majira ya saa 11:00 jioni
katika mtaa wa Soko kuu Mbinga mjini.
Imefafanuliwa kuwa Kayombo alimshambulia mwandishi wa habari
Kassian Nyandindi wa gazeti la Majira mkoani hapa, baada ya kumhoji masuala ya
utoro kazini ambapo amekuwa akilalamikiwa kwa muda mrefu na Walimu wenzake wa
sekondari hiyo kwamba, haudhurii ipasavyo vipindi vyake vya masomo darasani
pale anapotakiwa kufundisha wanafunzi wa shule hiyo.
![]() |
| Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Zubery Mwombeji. |
Aidha imeelezwa kuwa tokea mwalimu huyo ahamie shuleni hapo
Januari 11 mwaka 2016 akitokea shule ya sekondari Dokta Shein, iliyopo katika
kata ya Mpepai halmashauri ya mji wa Mbinga amekuwa na tabia hiyo ya
kutozingatia vipindi vya kufundisha watoto darasani.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji amethibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kwamba mwalimu Kayombo amefunguliwa shauri hilo
katika Kituo kikuu cha Polisi wilaya ya Mbinga, Jalada la uchunguzi lenye namba
MBI/IR/286/2017 na baadaye aweze kufikishwa Mahakamani kujibu tuhuma hizo
zinazomkabili.
Awali kwa upande wake Nyandindi alipotakiwa kutolea ufafanuzi
juu ya hali hiyo alikiri kushambuliwa na mwalimu huyo ambapo alieleza kuwa
ilitokana na kumhoji kufuatia kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa Walimu wenzake
shule ya sekondari Kiamili kwamba, haudhurii ipasavyo darasani hivyo walimu
wenzake hulazimika kujitolea kufundisha masomo ambayo alipaswa yeye
kuyafundisha shuleni hapo.
WANANCHI WAHAKIKISHIWA UJENZI WA DARAJA MTO KITURA
Na Dustan Ndunguru,
Mbinga.
Mbinga.
MWENYEKITI wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma
Ambrose Nchimbi amewahakikishia wananchi wa kata ya Kitura wilayani humo kwamba
halmashauri hiyo itajenga daraja la mto Kitura ambalo limekuwa kero kubwa kwa
wananchi wa kata hiyo, sambamba na kuzipatia ufumbuzi wa kudumu changamoto
zingine ambazo zimekuwa zikikwamisha shughuli za maendeleo ndani ya kata hiyo.
| Mkurugenzi mtendaji Halmashauri wilaya Mbinga, Gombo Samandito. |
Alisema kuwa lengo la ziara hiyo ni kukagua miradi hiyo ambayo
imekuwa ikitekelezwa kwa nyakati tofauti wilayani humo, sambamba na kubaini
changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo na
kwamba wananchi amewaasa kutoa ushirikiano wa karibu kwa kueleza ukweli hasa
pale wanapobaini mradi unatekelezwa chini ya kiwango.
SONGEA WAPONGEZWA KWA KUKUZA TAALUMA ELIMU YA MSINGI NA SEKONDARI
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
POLOLET Kamando Mgema, ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Songea
mkoani Ruvuma amewapongeza walimu wa shule za msingi na sekondari katika
Manispaa ya Songea mkoani humo, kwa kufanya kazi nzuri ambayo imeleta mafanikio
mazuri ya kukuza taaluma katika matokeo ya mitihani darasa la saba na kidato
cha nne.
Mkuu huyo wa wilaya alitoa pongezi hizo kwenye kikao cha
tathimini ya elimu kwa mwaka wa 2015/2016 ambacho kiliwakutanisha Wadau mbalimbali
wa elimu Waratibu elimu kata, Walimu wakuu wa shule za msingi, Wakuu wa shule
za sekondari, Madiwani na Maofisa elimu ambacho kilifanyika kwenye ukumbi wa
shule ya sekondari ya wasichana Songea.
Pamoja na kuwapatia pongezi hizo, Mgema alikemea pia tabia
zinazofanywa na baadhi ya walimu kuwa na utoro kazini ambapo amewataka waache
mara moja vinginevyo kwa yule atakayebainika hatua kali za kisheria
zitachukuliwa ikiwemo kufukuzwa kazi.
KITURA SEKONDARI HAINA MWALIMU WA HESABU NA FIZIKIA
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
SHULE ya Sekondari Kitura
iliyopo katika kata ya Kitura wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, haina mwalimu wa somo
la Hisabati na Fizikia tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007 jambo ambalo limekuwa
likisababisha wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo kutosoma kabisa masomo hayo
muhimu kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.
![]() |
| Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye. |
Kaimu Mkuu wa shule hiyo,
Stanslaus Mapunda alisema hayo juzi wakati wa ziara ya Madiwani ambao ni
Wajumbe wa Kamati ya uongozi na mipango ya halmashauri ya wilaya hiyo, iliyokuwa
ikiongozwa na Mwenyekiti wake Ambrose Nchimbi.
Mapunda alisema kuwa licha ya
kulifikisha tatizo hilo katika mamlaka husika kwa muda mrefu hakuna utekelezaji
uliofanyika na kwamba mpaka sasa pia hakuna ufumbuzi uliofikiwa juu ya utatuzi
wa tatizo hilo hivyo wanalazimika kufundisha masomo mengine tu jambo ambalo
limekuwa likisababisha watoto hao kutopata fursa nzuri ya kujisomea.
Thursday, February 23, 2017
SERIKALI YATOA UFAFANUZI JUU YA KUWAFUNGIA VIBANDA WAFANYABIASHARA SOKO KUU SONGEA
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
SERIKALI kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Songea
mkoani Ruvuma, imetoa ufafanuzi juu ya hatua iliyochukua ya kuwafungia vibanda
Wafanyabiashara wa Soko kuu Songea lililopo katika Manispaa hiyo kwamba,
walifanya hivyo kutokana na wafanyabiashara hao kudaiwa shilingi milioni 150 za
pango la vibanda vya biashara ambavyo wamepanga.
Ufafanuzi huo umetolewa na Mkuu wa wilaya ya Songea,
Pololet Kamando Mgema alipokuwa akizungumza jana na waandishi wa habari ofisini
kwake katika ukumbi wa mikutano wa wilaya hiyo.
Mgema alifafanua kuwa soko hilo lilianzishwa mwaka 1938
na kwamba ulipofika mwaka 1996 halmashauri hiyo ililazimika kuwaruhusu
wafanyabiashara kukarabati vibanda hivyo vya soko ambavyo walikuwa wakifanyia
biashara zao.
Alisema kuwa kila mfanyabiashara kwa wakati huo alikuwa
akilipa pango la shilingi 8,000 kwa mwezi ambapo kiasi hicho kilikuwa
kikiendelea kulipwa mpaka Agosti 20 mwaka 2002 wakati soko hilo lilipoungua na
kuteketea kwa moto.
Sunday, February 19, 2017
KAMATI YA UONGOZI NA MIPANGO YARIDHISHWA NA UJENZI NYUMBA ZA WALIMU KITURA SEKONDARI
Na Dustan Ndunguru,
Mbinga.
WAJUMBE Kamati ya
uongozi na mipango katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,
imepongeza kazi nzuri inayoendelea kufanywa na Kampuni ya Sinani Building
Contactors katika kukamilisha ujenzi wa nyumba za walimu shule ya sekondari
Kitura iliyopo wilayani humo, mradi ambao hadi kukamilika kwake utagharimu
shilingi milioni 168.7.
Mwenyekiti wa
kamati hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, Ambrose
Nchimbi alitoa pongezi hizo wakati wa ziara yake ya kukagua mradi huo iliyofanyika
mwishoni mwa wiki ambapo alisema kwamba mradi huo hadi kukamilika kwake utasaidia
kuondoa tatizo la walimu kukosa nyumba za kuishi na kuondokana na adha ya kupanga
uraiani.
Nchimbi alisema
kuwa mradi huo unagharimu fedha nyingi hivyo ni vyema ujenzi wake unapaswa kuwa
wa viwango vinavyokubalika na kwamba kamwe halmashauri hiyo, haitawavumiliwa makandarasi
ambao wamekuwa na tabia ya kuhujumu miradi ya maendeleo ya wananchi na
kusababisha kuzua malalamiko yasiyokuwa ya lazima.
WAJUMBE WA BODI MBINGA WALIMU SACCOS WASWEKWA RUMANDE WAKITUHUMIWA KUIBA MILIONI 540,704,572
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WAJUMBE wa bodi ya Kamati ya usimamizi Chama cha ushirika
Mbinga Walimu SACCOS iliyopo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wamekamatwa na
kuwekwa mahabusu wakituhumiwa kuiba shilingi milioni 540,704,572 za wanachama
wa chama hicho cha ushirika na kusababisha hasara kubwa kwa chama kushindwa
kujiendesha kwa manufaa ya wanachama.
Aidha hatua hiyo ya kukamatwa kwa Wajumbe hao ilitolewa na
Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika mkoani humo, Biezel Malila baada ya
kusomwa taarifa ya ukaguzi juu ya mwenendo wa chama hicho cha ushirika ambayo
ilibainisha wizi wa fedha hizo katika mkutano mkuu maalumu wa wanachama,
uliofanyika Februari 18 mwaka huu kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini
hapa.
“Kwa masikitiko makubwa ndugu zangu wanachama mliohudhuria
mkutano huu naomba niwaeleze kwamba mwenendo wa chama hiki sio mzuri unatia
kichefuchefu, chama kina hali mbaya kina hati chafu ya ukaguzi kwa kuwa Wajumbe
wa bodi hii wameshiriki kwa namna moja au nyingine kukiuka taratibu za
uendeshaji wa chama hiki, hivyo wanapaswa kuwajibika kwa mujibu wa sheria na
taratibu husika za vifungu vya uendeshaji wa vyama vya ushirika”, alisema
Malila.
Mrajisi huyo wa vyama vya ushirika mkoa wa Ruvuma alifafanua
kuwa fedha hizo ambazo Wajumbe hao wanadaiwa kuiba na kujinufaisha kwa matakwa
yao binafsi zilitokana na baki ya mikopo shilingi milioni 174,915,794 hisa,
akiba na amana shilingi milioni 363,873,778 na mikopo ambayo waliitengeneza
bila kufuata taratibu husika walichota shilingi milioni 1,915,000.
WILAYA YA MBINGA MKOANI RUVUMA YAONGOZA KWA KILIMO CHA BANGI
Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
IMEELEZWA kuwa katika mkoa wa Ruvuma wilaya ya Mbinga mkoani
humo imekuwa ikiongoza kwa kilimo cha bangi, hivyo serikali itaendelea
kupambana na watu wanaohusika na uzalishaji wa zao hilo kwa kuwachukulia hatua
za kisheria ikiwemo kuwafikisha Mahakamani.
Aidha wananchi wametakiwa kutoa ushirikiano mara kwa mara kwa
viongozi wa ngazi ya vijiji, kata hadi wilaya katika utoaji wa taarifa ni wapi
kumekuwa na mashamba ambayo yamekuwa yakitumika kuzalisha zao hilo.
Mkuu wa wilaya hiyo, Cosmas Nshenye alisema hayo jana
alipokuwa akizungumza na Madiwani pamoja na wananchi kwenye kikao cha kujadili
mapendekezo ya mpango wa bajeti ya maendeleo halmashauri ya mji wa Mbinga kwa
mwaka wa fedha wa 2017/2018 kilichofanyika kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo
mjini hapa.
Tuesday, February 14, 2017
WALIOCHUKUA MIKATABA SOKO KUU SONGEA WAANZA KUFUNGULIWA VIBANDA VYAO
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, Abdul Hassan Mshaweji amesema kwamba tayari
vibanda vya Soko kuu la Manispaa hiyo vimeanza kufunguliwa na kupewa
wafanyabiashara ambao wametimiza masharti yaliyowekwa na Manispaa hiyo.
![]() |
| Pololet Mgema, Mkuu wa wilaya ya Songea. |
Mshaweji alifafanua kuwa hadi mwishoni mwa wiki hii
wanatarajia idadi kubwa ya vibanda vitakuwa vimefunguliwa, baada ya
wafanyabiashara wengi kuhamasika kuchukua mikataba na kulipia kodi ya vyumba
vilivyopo katika soko hilo.
NAMTUMBO WASAMBAZA MICHE BORA YA KAHAWA KWA WAKULIMA WAKE
Na Yeremias Ngerangera,
Namtumbo.
HALMASHAURI ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, imejiwekea
mikakati ya usambazaji wa miche bora ya kahawa kwa wakulima wake ambapo tayari
miche 33,333 imegawiwa kwa wakulima wanaoishi katika vijiji vya Litola,
Namabengo na Lumecha wilayani humo katika msimu wa kilimo mwaka huu.
Aidha lengo la uzalishaji huo ni kuwafanya wakulima hao
waweze kupanda zao hilo katika mashamba yao na baadaye waweze kujikwamua
kiuchumi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.
Kaimu Ofisa kilimo wa wilaya hiyo, Aniceth Ndunguru alisema
kwamba yeye ndiye aliyesimamia zoezi la ugawaji wa miche hiyo kwenye vijiji
hivyo na kwamba halmashauri hiyo, katika bajeti yake ya mwaka 2016/2017
ilitenga kiasi cha shilingi milioni 10 kwa ajili ya kununulia miche hiyo ambayo
wakulima hugawiwa bure hatimaye waweze kupanda katika mashamba yao.
Monday, February 13, 2017
AFISA KILIMO HALMASHAURI MJI WA MBINGA ADAIWA KUINGIA MITINI NA MBEGU ZA WAKULIMA WA TANGAWIZI
| Dkt. Binilith Mahenge, Mkuu wa mkoa wa Ruvuma. |
Na Dustan Ndunguru,
Mbinga.
MALALAMIKO yametolewa na baadhi ya Wananchi waishio katika
kata ya Kihungu Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, dhidi ya Kaimu Ofisa
kilimo wa halmashauri hiyo, Maganga Ngahy wakimshutumu kutokana na kitendo
chake cha kuwapelekea mbegu pungufu za zao la Tangawizi wananchi wa kata hiyo, ambazo
walipaswa kuzalisha katika mashamba yao katika msimu wa mwaka huu.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti
Wanachama wa kikundi cha JITUME waliopo katika kata hiyo walisema kuwa kabla ya
kupelekewa mbegu hizo walielezwa kwamba wangepata kilo 500 za zao hilo, lakini cha
kushangaza wamepewa kilo 400 tu huku kukiwa na upungufu wa kilo 100 jambo
ambalo limewafanya washindwe kutimiza ndoto yao ya kupanda eneo lote walilotarajia
kupanda Tangawizi hizo.
Walisema kuwa mbegu hizo za Tangawizi wanachotambua ni kwamba
wamekopeshwa ili wakati wa mavuno utakapowadia wanapaswa kurejesha baadhi ya
mbegu kwa wakulima wengine, ambapo wasiwasi wao walionao sasa ni kwamba
kutokana na kupatiwa mbegu pungufu watashindwa kurejesha kiasi husika ipasavyo
ukizingatia kwamba uongozi wa halmashauri hiyo unatambua wao wamepewa kilo zote
miatano na sio vinginevyo.
MGOGORO SOKO KUU SONGEA WAFANYABIASHARA WAFUNGA SAFARI DODOMA KUMUONA WAZIRI MKUU
Na Mwandishi wetu,
Songea.
WAFANYABIASHARA wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani
Ruvuma wametuma ujumbe wa wafanyabiashara wenzao watano na wazee watano kwenda
Dodoma kumuona Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kwa lengo la kupeleka kilio chao baada
ya Mkuu wa wilaya ya Songea Pololet Kamando Mgema kudaiwa kuwafungia vibanda vyao vya
biashara, tangu Februari 11 mwaka huu kwa madai kwamba wanadaiwa shilingi
milioni 100 na halmashauri hiyo jambo ambalo wamekana na kueleza kuwa sio la
kweli.
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Masoko katika Manispaa ya
Songea (UWABIMASO) Leonard Chiunga alisema hayo jana wakati alipokuwa akizungumza
kwenye mkutano wa dharura na wafanyabiashara hao, uliofanyika kwenye ukumbi wa
mikutano wa Chama cha walimu Songea uliopo mjini hapa ambao ulihudhuriwa pia na
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania mkoa wa Ruvuma, Issaya
Mwilamba.
Chiunga alisema kuwa tokea maduka hayo yalipofungwa wateja
ambao wamekuwa wakienda kwa ajili ya kupata mahitaji kwenye maduka hayo wanashindwa
kupata mahitaji husika, jambo ambalo limeonekana kuwa ni kero kubwa kwao hivyo wanaziomba
mamlaka za juu zione umuhimu wa kuchukua hatua haraka kuyafungua ili hata
wafanyabiashara hao nao wasiweze kupata hasara kutokana na kuyafunga huko.
WATANZANIA WASHAURIWA KUSHIRIKIANA NA MALAWI
Na Kassian
Nyandindi,
Songea.
WANANCHI wanaoishi katika mikoa inayopakana na nchi ya Malawi
wamehimizwa kuona umuhimu wa kutumia fursa mbalimbali zilizopo nchini humo,
ikiwemo kufanya biashara kwa njia ambazo ni halali ili waweze kuinua uchumi
wao.
Katibu tawala wa mkoa wa Ruvuma Hassan Bendeyeko alisema hayo
juzi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake ambapo
alisisitiza kuwa wananchi wanaoishi katika mikoa ya Mbeya, Songwe, Njombe na
Ruvuma wanayo fursa kubwa ya kuweza kufanya hivyo ili waweze kuondokana na
umaskini.
Bendeyeko alisema kuwa hivi sasa ni wakati pekee wa
kuchangamkia fursa hizo kwa kujenga ushirikiano mzuri kati ya Tanzania na
Malawi, jambo ambalo litaweza kuleta tija katika shughuli zao za kukuza uchumi wa
kila siku.
Sunday, February 12, 2017
WANAFUNZI AMBAO HAWAJARIPOTI SHULE KUCHUKULIWA HATUA ZA KISHERIA
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MAOFISA elimu katika Halmashauri ya mji wa Mbinga na wilaya
ya Mbinga mkoani Ruvuma, kwa kushirikiana na watendaji wa vijiji na kata
wametakiwa kuhakikisha kwamba watoto wote waliochaguliwa kwenda shule kwa ajili
ya kuanza kidato cha kwanza wanaripoti haraka katika shule husika, kabla hatua
za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao.
Agizo hilo limetolewa juzi na Mkuu wa wilaya hiyo, Cosmas
Nshenye alipokuwa akizungumza na Madiwani, Maofisa elimu na Watendaji wa
halmashauri hizo mjini hapa huku akieleza kuwa katika kipindi cha kuanzia mwezi
Januari mwaka huu mpaka sasa kwa shule hizo za sekondari jumla ya wanafunzi 120
hawajaripoti kwenye shule walizopangiwa kwenda kusoma wilayani humo, hivyo kuna
kila sababu kwa serikali kuchukua hatua ili kuweza kudhibiti hali hiyo isiweze
kuendelea kuwepo na kujenga mazoea katika jamii.
“Naendelea kusisitiza kwamba wanafunzi wote waliochaguliwa
kuingia kidato cha kwanza wanapaswa kwenda shuleni kusoma, nawataka maofisa
elimu na watendaji wa vijiji na kata mshirikiane kumaliza tatizo hili mapema na
ofisi yangu ipate taarifa haraka kwamba watoto hawa wapo shuleni wanasoma”,
alisisitiza.
DC AWAPONGEZA MADIWANI MBINGA
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye amewapongeza
wajumbe wa kikao cha maridhiano ya kugawana mali kati ya pande mbili za
halmashauri ya mji wa Mbinga na wilaya ya Mbinga kwa kumaliza kikao hicho
katika hali ya amani, utulivu na maelewano bila ya kuwepo kwa mgogoro, mvutano
na malumbano.
| Cosmas Nshenye. |
Nshenye ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kikao hicho, alitoa
pongezi hizo juzi wakati alipokuwa akizungumza na Madiwani wa halmashauri hizo
katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa.
Alisema kuwa kitendo hicho kimeonyesha utashi na ukomavu wa
kifikra kwa kile alichoeleza kuwa kuna baadhi ya maeneo mengine wanapokuwa
kwenye vikao kama hivyo, imekuwa ikizuka migogoro na malumbano ambayo
yanachangia kwa kiasi kikubwa kukwamisha shughuli za maendeleo ya wananchi huku
akisisitiza kuwa uhamisho wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga utafanyika mara
baada ya kukamilika kwa ujenzi wa ofisi zao.
Akichangia hoja kwenye kikao hicho, Mwenyekiti wa halmashauri
ya mji wa Mbinga Kipwele Ndunguru alisema kuwa mapendekezo yaliyoridhiwa na
kikao cha kamati ya ushauri ni kuhamisha bajeti ya shilingi bilioni 2.1 ambayo
ilikuwa inatakiwa kujenga boma la halmashauri hiyo na kuzihamishia halmashauri
ya wilaya ya Mbinga ambapo mpaka sasa kwa kuanzia kimetolewa kiasi cha shilingi
milioni 500.
ASHIKILIWA NA POLISI KWA TUHUMA YA KUMUUA MDOGO WAKE
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
JESHI la Polisi mkoani Ruvuma linamshikilia Omary Likande (32)
ambaye ni mkazi wa kijiji cha Msechela wilayani Tunduru mkoani humo, kwa tuhuma
ya kumuua mdogo wake Unda Likande (23) kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali
shingoni.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Kamanda wa Polisi wa
mkoa huo, Zubery Mwombeji alisema kuwa tukio hilo lilitokea Februari 7 mwaka
huu majira ya mchana katika kitongoji cha Mkalala kilichopo katika kijiji cha Msechela
tarafa ya Namasakata wilayani humo.
Mwombeji alisema kuwa siku hiyo ya tukio inadaiwa kuwa Unda
aliuawa kwa kukatwa shingoni na kaka yake, Omary Likande wakati baba yao alipokuwa
ametoka kwenda kutafuta chakula.
SITA WAJERUHIWA VIBAYA NA MMOJA AFARIKI DUNIA BAADA YA KUPIGWA NA RADI
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
WATU sita wanaoishi katika kitongoji cha Kifaguro kijiji cha
Lituta wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, wamejeruhiwa vibaya na mtu mmoja kufariki
dunia baada ya kupigwa na radi kufuatia mvua kubwa ambayo iliambatana na upepo
mkali, kuezua nyumba zenye kaya 37 na kusababisha kuharibika kwa mali
mbalimbali zilizokuwemo ndani ya nyumba hizo.
Katika tukio hilo wakazi 79 wa kitongoji hicho pia wamekosa
mahali pa kuishi ambapo habari zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi wa mkoa
huo, Zubery Mwombeji alisema kuwa tukio hilo lilitokea Februari 4 mwaka huu
majira ya saa 9 alasiri.
Mwombeji alifafanua kuwa siku ya tukio hilo mvua hiyo iliambatana
na upepo mkali na kusababisha kuezuliwa kwa nyumba hizo na vitu mbalimbali
vilivyokuwemo ndani yake viliharibika ikiwemo vyakula ambapo thamani yake halisi
bado haijajulikana.
Saturday, February 11, 2017
DC: VITUO VYA KUTOLEA HUDUMA YA AFYA MBINGA KUMEKUWA NA TATIZO LA UKOSEFU WA DAWA
![]() |
| Sehemu ya watumishi wa halmashauri ya wilaya Mbinga, wakimsikiliza Mkuu wa wilaya hiyo Cosmas Nshenye. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye
amesema kuwa katika wilaya hiyo kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa
wananchi ambayo amekuwa akiyapokea kwa nyakati tofauti kwamba katika vituo vya
kutolea huduma za afya wilayani humo, kumekuwa na tatizo la ukosefu wa dawa
jambo ambalo limekuwa ni kero kubwa kwa wananchi.
Aidha kufuatia hali hiyo amewataka watendaji waliopewa
dhamana kusimamia kikamilifu majukumu yao ya kazi ikiwemo kujipanga ipasavyo
katika kuhudumia wagonjwa wanaokwenda kutibiwa ili kuweza kuondoa malalamiko
hayo yasiyokuwa ya lazima.
Nshenye alisema kuwa tatizo hilo linaanzia hospitali ya
wilaya ambapo malalamiko juu ya ukosefu wa dawa yamekuwa yakitolewa na wananchi
kwa muda mrefu na kwamba wamekuwa wakilazimika wakati mwingine kwenda kununua
dawa hizo kwenye maduka ya dawa muhimu badala ya kupewa hospitalini hapo.
BARAZA LA MADIWANI MBINGA LAWAFUKUZA KAZI WATUMISHI WAKE
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani
Ruvuma limewafukuza kazi baadhi ya watumishi wake, kutokana na makosa
mbalimbali yakiwemo ya utoro kazini na kuisababishia halmashauri hiyo hasara ya
shilingi milioni 46,680,000.
Nchimbi alisema kuwa waliofukuzwa kazi ni Mosta Ndunguru
ambaye ni Afisa tabibu na Bapara Mwang'ombe Mhudumu wa afya ambapo wote kwa
pamoja wamefukuzwa kwa makosa ya utoro kazini.
Wednesday, February 8, 2017
SAMANDITO: MPANGO WA BAJETI MBINGA UNALENGA KUBORESHA HUDUMA ZA KIJAMII NA KUKUZA UCHUMI KWA KUZINGATIA DIRA YA MAENDELEO YA TAIFA KUWA NA VIWANDA VYA KATI
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
IMEELEZWA kuwa malengo makuu ya mpango wa bajeti kwa Halmashauri
ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma ni kuimarisha amani na utawala bora, kuboresha
huduma za kijamii, kukuza uchumi wa wilaya hiyo kwa lengo la kuboresha maisha
ya wananchi wake, sambamba na dira ya maendeleo ya taifa inayolenga Tanzania
kuwa nchi ya viwanda vya kati.
Aidha halmashauri hiyo inaendelea na jitihada za kuongeza
vyanzo vipya vya mapato ya ndani badala ya kutegemea zao la kahawa pekee ambalo
hivi sasa halikidhi mahitaji husika, ambapo jitihada zinafanyika za kutafuta
wawekezaji watakaoweza kutumia rasilimali zilizopo wilayani humo kama vile madini,
ardhi na misitu viweze kuingiza mapato zaidi.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya
wilaya ya Mbinga, Gombo Samandito wakati alipokuwa akitoa maelezo mafupi juu ya
rasimu ya mpango wa bajeti kwa Baraza maalum la Madiwani wa halmashauri hiyo, mwaka
wa fedha 2017 hadi 2018 lililoketi leo kwenye ukumbi wa Umati uliopo mjini hapa.
Samandito alisema kuwa kuongezeka kwa fedha hizo za mapato
kutatokana pia na fedha za upimaji wa mashamba ya kahawa ambapo ekari moja
hupimwa kwa shilingi 100,000 na kwamba tayari mashamba 70,000 ya wananchi
wilayani humo yamepimwa na wahusika kupewa hati za kimila huku halmashauri
ikiweza kupata shilingi bilioni 7,000,000,000.
Tuesday, February 7, 2017
ASHIKILIWA NA POLISI KWA TUHUMA YA KUMNYWESHA SUMU MWANAYE NA KUMSABABISHIA KIFO
Na Mwandishi wetu,
Songea.
JESHI la Polisi mkoani Ruvuma linamshikilia Suzana Mgaya (19)
ambaye ni mkazi wa kijiji cha Wino tarafa ya Madaba wilayani Songea mkoa wa
Ruvuma, kwa tuhuma ya kumnywesha sumu mwanaye mwenye umri wa mwaka mmoja na
nusu aliyejulikana kwa jina la Gerlad Kabelege na kusababisha afariki dunia huku
yeye mwenyewe pia akinywa sumu hiyo kwa lengo la kutaka kujiua.
Taarifa zilizopatikana jana mjini Songea na kuthibitishwa na Kamanda
wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji alieleza kuwa tukio hilo lilitokea Februari
5 mwaka huu majira ya saa 12:00 jioni katika kijiji hicho cha Wino.
Akizungumzia tukio hilo Kamanda huyo wa Polisi alisema kuwa
Suzana Mgaya siku hiyo alikutwa akitoka povu mdomoni na puani jambo ambalo
lilisababisha hofu kwa mashuhuda kuwa huenda amekunywa sumu.
MASHINDANO KUMTAFUTA BALOZI WA UTALII RUVUMA YAFANYIKA MAJIMAJI SONGEA
![]() |
| Samson Kahabuka, Mratibu wa kituo cha habari za utalii mkoa wa Ruvuma. |
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MASHINDANO ya kumtafuta Balozi wa utalii mkoa wa Ruvuma,
ambayo yanaratibiwa na Kituo cha habari za utalii mkoani humo yameanza kufanyika
kwenye hoteli ya Majimaji iliyopo mjini Songea.
Mratibu wa kituo hicho, Samson Kahabuka alisema kuwa warembo
15 kutoka wilaya ya Songea wameanza mazoezi kwenye ukumbi wa hoteli hiyo ambapo
lengo kuu la kufanya hivyo ni kuwapata warembo watakaotoka wilaya zote za mkoa huo.
Kahabuka alisema lengo kuu la shindano hilo ni kutangaza
vivutio vyote vya mkoa wa Ruvuma, ambapo Februari 10 mwaka huu warembo 15
kutoka wilaya ya Songea watatembelea wilaya ya Nyasa ili kuweza kuona baadhi ya
vivutio vya wilaya hiyo.
SONGEA WAPITISHA BAJETI YA SHILINGI BILIONI 26.5
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
BARAZA la Madiwani katika Halmashauri ya wilaya ya Songea
mkoani Ruvuma limepitisha bajeti ya shilingi bilioni 26,531,667,816 katika
mwaka wa fedha wa 2017 hadi 2018 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali
ya maendeleo ya wananchi wilayani humo.
MADIWANI MBINGA WATAKIWA KUSIMAMIA KIKAMILIFU MIRADI YA WANANCHI
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MKUU wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye
amewataka Madiwani wa wilaya hiyo kusimamia kikamilifu miradi mbalimbali ya
maendeleo ya wananchi ambayo inatekelezwa katika kata zao, ili iweze kukamilika
kwa wakati na viwango vinavyokubalika.
Pia amewaasa wazingatie masuala ya kitaalamu pindi watendaji
wanapotoa ushauri wakati huo wa utekelezaji wa miradi jambo ambalo litasaidia
kuepusha migongano baina yao.
Sunday, February 5, 2017
WATUMISHI SABA WA HALMASHAURI AMBAO NI WAJUMBE BODI YA KURUGENZI SACCOS MBINGA WABURUTWA MAHAKAMANI WAKIDAIWA KULA NJAMA NA KUJIPATIA MILIONI 500
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
HATIMAYE Watumishi saba wanaotoka katika Halmashauri ya mji
wa Mbinga, wilaya ya Mbinga na Nyasa mkoani Ruvuma ambao pia ni Wajumbe wa bodi
ya Chama cha ushirika Mbinga Kurugenzi SACCOS, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama
ya Hakimu mkazi mkoani humo wakituhumiwa kula njama na kutenda kosa la
kujipatia mkopo wa shilingi milioni 500 kutoka benki ya CRDB kinyume na
taratibu husika.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa Mahakamani hapo na
Mwendesha mashtaka ambaye ni Wakili wa serikali mkoani hapa, Shaban Mwegole
mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi wa Mahakama hiyo Simon Kobero alidai kuwa
washtakiwa hao pia wanakabiliwa na makosa kumi, wakidaiwa kughushi nyaraka mbalimbali
na kufanikiwa kufanya wizi katika sehemu ya fedha hizo jambo ambalo limesababisha
hasara kubwa kwa chama hicho kushindwa kujiendesha kwa manufaa ya wanachama.
Mwendesha mashtaka huyo aliwataja washtakiwa wanaokabiliwa
kufanya makosa hayo na kufunguliwa kesi Jinai namba 1 ya mwaka 2017 kuwa ni,
Emmanuel Mwasaga, Alex Kalilo na Zackaria Lingowe ambao ni watumishi wa
halmashauri ya wilaya ya Nyasa, Jamima Challe na Stella Mhagama wanatoka
halmashauri ya mji wa Mbinga, Lucas Nchimbi na Mhadisa Meshack nao ni watumishi
wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga.
MPANGO WA KUUZA KAHAWA KWA JINA LA EX MBINGA WANUFAISHA WAKULIMA
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
KATIKA kuhakikisha kwamba wananchi wa wilaya ya Mbinga mkoani
Ruvuma, wanaendelea kunufaika na uzalishaji wa zao la kahawa wilayani humo,
wilaya inaendelea kutekeleza mpango wa kuhifadhi na kuuza kahawa ikiwa na jina
la Ex Mbinga, badala ya Miji ya Makambako mkoani Njombe kama ilivyokuwa hapo
awali.
Aidha mpango huo wa kuuza kahawa kwa majina ya Ex Makambako
ulikuwa ukisababisha kupunguza faida ya mauzo ya kahawa kwa mkulima na
kuhamasisha wafanyabiashara kutorosha kahawa ya Mbinga na kumfanya mkulima
aendelee kupata hasara.
Taarifa hiyo ilitolewa na Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas
Nshenye ambapo alifafanua kuwa gharama hizo kwa mkulima hivi sasa zimepungua
ikiwemo na suala la utoroshaji wa kahawa, hali ambayo inavutia hata kuwepo kwa
wawekezaji wa zao hilo wilayani humo.
MBINGA WAENDELEA KUFANIKIWA ZOEZI LA UPIMAJI ARDHI
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
IMEELEZWA kuwa hadi kufikia Disemba mwaka jana, mashamba
yenye ukubwa wa ekari 78,149.065 sawa na hekta 31,259.626 yameingizwa na
kupimwa katika mpango wa upimaji ardhi, ambapo halmashauri ya wilaya ya Mbinga katika
kipindi hicho imefanikiwa kupima ekari 70,491.165 na ekari 7,657.9 zimepimwa
kutoka halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma.
Kwa mujibu wa takwimu hizo na taarifa zilizomfikia mwandishi
wetu kutoka vyanzo mbalimbali vya habari vimethibitisha kuwa, halmashauri hizo
zinaendelea kutekeleza sheria za ardhi pamoja na kutimiza agizo la serikali la
kupima kila kipande cha ardhi na kukimilikisha kwa walengwa husika.
Aidha halmashauri zimekuwa zikiendelea kuhamasisha wamiliki
wa viwanja na mashamba kulipia kodi za ardhi pamoja na kuviendeleza viwanja
vyao kwa mujibu wa sheria, ikiwa ni pamoja na kusambaza hati za madai ya kodi
kwa wadaiwa sugu na kwamba wale wanaoshindwa kulipa hufikishwa Mahakamani.
ATIWA MBARONI KWA TUHUMA YA KUMBAKA MWANAFUNZI
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MKAZI mmoja wa kijiji cha Luhimba kata ya Mtyangimbole wilaya
ya Songea mkoani Ruvuma, Allan Kihwili (48) ametiwa mbaroni na Jeshi la Polisi
mkoani humo kwa tuhuma ya kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka sita, ambaye
anasoma shule ya msingi Ngembambili na kumsababishia maumivu makali katika
sehemu zake za siri.
![]() |
| Zubery Mwombeji. |
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake Kamanda wa Polisi wa mkoa
huo, Zubery Mwombeji alisema kuwa tukio hilo lilitokea Januari 24 mwaka huu
majira ya saa 11 jioni katika kijiji hicho wilayani hapa.
Mwombeji alifafanua kuwa inadaiwa siku ya tukio hilo mwanafunzi
huyo ambaye jina lake limehifadhiwa akiwa anapita jirani na nyumba ya mtuhumiwa
huyo ghafla alimkamata na kumwingiza kwenye nyumba anayoishi kisha kumfanyia unyama
huo.
Friday, February 3, 2017
DC MBINGA AWATAKA WADAU WA SHERIA KUTENDA HAKI NA KUTEKELEZA WAJIBU WAO IPASAVYO
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
IMEELEZWA kuwa ucheleweshaji wa utoaji haki kwa wakati unasababisha kupoteza rasilimali muda na kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi,
hivyo wito umetolewa kwa wadau wote washeria kuhakikisha kwamba wanatenda haki
na kutekeleza wajibu wao ipasavyo.
Hayo yalisemwa jana na Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas
Nshenye wakati alipokuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya siku ya sheria
nchini yaliyofanyika kiwilaya katika viwanja vya Mahakama ya wilaya hiyo mjini
hapa.
“Nasisitiza kwamba zile kesi ambazo zinauwezekano wa kutolewa
dhamana zitolewe dhamana kwa wakati, tuache tabia ya kuwaweka mahabusu gerezani
tupunguze wasiwepo wengi wanaokaa huko bila sababu yoyote ile ya msingi”,
alisema Nshenye.
WAFUASI WATATU CHADEMA WAPANDISHWA KIZIMBANI WAKIDAIWA KUHARIBU GARI LA CCM
Na Mwandishi wetu,
Songea.
WAFUASI watatu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wamepandishwa kizimbani katika
Mahakama ya Hakimu mkazi mkoani humo, kwa tuhuma ya kula njama na kuharibu gari
la Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kulipiga mawe.
Mwanasheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria mkuu wa serikali kanda
ya Songea Tumaini Ngiruka aliwataja Mahakamani hapo washitakiwa hao kuwa ni Joseph
Fuime (52) mkazi wa Songea mjini aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA mkoani
humo, Emmanuel Kalisinjesi (37) mkazi wa mtaa wa Ruvuma na Sedrick Komba (51) mkazi
wa Bombambili mjini hapa.
Mwendesha mashtaka ambaye ni Mwanasheria huyo wa Serikali kanda
ya Songea, Ngiruka alidai mbele ya Hakimu mkazi mwandamizi wa Mahakama ya mkoa
wa Ruvuma, Issa Magori kuwa mnamo Januari 20 mwaka huu majira ya usiku katika
eneo la mtaa wa Pambazuko uliopo nje kidogo ya Manispaa ya Songea washtakiwa hao
waliharibu gari la CCM aina ya Landcruiser lenye namba za usajili T 640 BEU kwa
kulipiga mawe na kusababisha kuvunjika kioo cha mbele ya gari hilo na upande wa
dereva.
WASHIKILIWA NA POLISI KWA TUHUMA YA KUJERUHI
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
JESHI la Polisi mkoani Ruvuma linawashikilia wakazi wawili wanaoishi
katika mtaa wa Pambazuko uliopo katika kata ya shule ya Tanga Manispaa ya
Songea mkoani humo, kwa tuhuma ya kumjeruhi Abethi Ponera (25) kwa kumkata na
kitu chenye ncha kali kwenye paja lake la mguu upande wa kulia na kumsababishia
jeraha na maumivu makali.
![]() |
| Zubery Mwombeji. |
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji amewataja
watuhumiwa hao kuwa ni Bernad Mng`ong`o (39) na Boniface Mbecha (27) wote
wakazi wa mtaa huo.
Mwombeji alisema kuwa tukio hilo lilitokea Januari 21 mwaka
huu majira ya saa tano usiku, katika mtaa huo.
Alifafanua kwamba siku ya tukio hilo Ponera akiwa anarudi
nyumbani kwake akitokea kunywa pombe kwenye kilabu cha pombe za kienyeji, ghafla
alivamiwa na watu asiowafahamu na kuanza kumpiga kisha kumjeruhi paja lake la
mguu wa kulia na kuathiri sehemu zake za siri.
Alisema kuwa Ponera kabla ya kukutwa na tukio hilo akiwa
katika kilabu hicho ambacho kinamilikiwa na Mg’ong’o kulikuwa na malumbano kati
yake na watu wengine aliokuwa anakunywa nao pombe hizo za kienyeji, ambao
walikuwa wakimtaka ifikapo Januari 22 mwaka huu aende kwenye uchaguzi mdogo
akamchague mgombea udiwani wanayemtaka wao (chama ambacho jina lake
linahifadhiwa) jambo ambalo Ponera alipingana nalo kisha baadaye aliamua
kuondoka kuelekea nyumbani.
Subscribe to:
Posts (Atom)








