Saturday, August 24, 2013

MFANYABIASHARA MAARUFU WA JIJINI MBEYA AKAMATWA MBINGA AKITOROSHA KAHAWA KINYEMELA KWA LENGO LA KUKWEPA KULIPA USHURU

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga Allanus Ngahi (Kushoto), aliyevaa kofia akiangalia gari ambalo lilikamatwa na shehena ya magunia ya kahawa ambalo mfanyabiashara maarufu Madawa Mwaijande wa Mwanjelwa mkoani Mbeya, alikuwa akilitorosha kuelekea Mbeya kwa lengo la kukwepa kulipa ushuru.


Gari lenye namba za usajili T. 856 CFL mali ya Medson Ulendo mkazi wa Mbinga mjini, lipo chini ya ulinzi katika kituo kikuu cha polisi wilaya Mbinga, ambalo lilikuwa likitumika kutorosha kahawa tani 10,000 kutoka kijiji cha Langiro wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma. Gari hilo lilikamatwa katika kijiji cha Kitai kwenye geti la kukagua mazao ya maliasili wilayani humo.(Picha zote na Kassian Nyandindi) 


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, imemkamata mfanyabiashara mmoja maarufu, ambaye alikuwa akitorosha kahawa tani 10 yenye thamani ya shilingi milioni 28 kutoka wilayani humo kuelekea mkoani Mbeya, kwa lengo la kukwepa kulipa ushuru wa halmashauri hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Allanus Ngahi alisema kahawa hiyo ilikamatwa Agosti 21 mwaka huu kijiji cha Kitai wilayani humo, majira ya saa tano usiku katika geti la kukagua mazao ya maliasili ikiwa inasafirishwa kwenye gari aina ya Scania lenye namba za usajili T. 856 CFL mali ya Medson Ulendo mkazi wa mjini hapa.

Ngahi alisema kahawa hiyo iliyokamatwa ni mali ya mfanyabiashara  Madawa Mwaijande ambaye ni wa Mwanjelwa mkoani Mbeya, ambapo wakati anakamatwa alikuwa na dereva aliyekuwa akiendesha gari hilo aliyemtaja kwa jina la Julius Kinunda.


Alifafanua kuwa kukamatwa huko kunatokana na halmashauri ya wilaya ya Mbinga, kuendelea kupambana vikali na wafanyabiashara wajanja ambao wanatabia ya kuhujumu ushuru wa halmashauri hiyo kwa njia za kutorosha mazao yanayozalishwa wilayani humo.  

“Wafanyabiashara hawa wamekamatwa na kahawa hii, wakiwa wanatokea Kata ya Langiro hapa wilayani, hivyo kahawa iliyokamatwa ni magunia 200 yenye jumla ya kilo 10,000”, alisema.

Hata hivyo Mwenyekiti huyo alieleza kuwa kahawa hiyo imechukuliwa na halmashauri hiyo na itauzwa hapo baadaye, baada ya taratibu husika za kisheria kufuata mkondo wake.


   

No comments: