Monday, August 12, 2013

WATOTO WA FAMILIA MOJA WILAYANI NAMTUMBO, WAFARIKI DUNIA KWA KULA CHAKULA CHENYE SUMU WAKATI WAKISHEREHEKEA SHEREHE ZA IDD

Kamanda wa polisi mkoa wa Ruvuma, Deusdedith Nsimeki.


























Na Kassian Nyandindi,
Namtumbo.

WATOTO wa nne wa familia moja kijiji cha Ligunga Kata ya Lusewa tarafa ya Sasawala wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma wamefariki dunia kwa kile kinachodaiwa kuwa baada ya kula chakula chenye sumu.

Kufuatia tukio hilo, aidha wengine 12 wamelazwa katika hospitali ya mkoa huo iliyopo Songea mjini, na wengine katika kituo cha afya Lusewa wilayani Namtumbo kwa madai ya kula chakula hicho.

Waandishi wa habari wamezungumza na katibu tarafa wa Sasawala Fred Maliyao alisema wanafamilia hao walikula vyakula karibu aina tatu na baadaye kupatwa na matatizo hayo.


Maliyao alifafanua kuwa katika siku ya sikukuu ya Idd wanafamilia hao walikula ugali na samaki, mbogamboga na utumbo wa kuku ambao unasadikika ulikuwa umechemshwa mchuzi wa samaki huku wengine walikula ugali kwa mboga ya mbaazi.

Alieleza kwamba walikuwa wakila vyakula hivyo wakiwa kwa baba yao mdogo na mkubwa  kwa zamu, ambapo walikuwa wakisherehekea sikukuu hiyo ya Idd.

Kwa upande wake mwanafamilia mmoja Bilahi Mumba alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 9 mwaka huu majira ya saa 5 asubuhi hadi majira ya mchana, baada ya watoto hao kula chakula hicho chenye sumu.
  
“Nasisi tunashangaa tuliona muda mfupi baada ya kula chakula hicho walianza kuanguka na wengine kutapika huku tukijitahidi kuokoa maisha ya watoto hao, lakini wanne wameweza kufariki na wengine tuliwakimbiza kituo cha afya cha Lusewa”, alisema.

Mumba aliwataja watoto hao waliokufa kuwa ni Zidane Mumba[25] Tazamio Mumba[9] Selemani Mumba[7] na Zahara Mumba[2] wakiwa wote wa familia moja.

Naye muuguzi wa kituo cha afya Lusewa Edrisa Ndauka alisema kuwa walipokelewa wagonjwa 16 katika kituo hicho, na wanne walifariki watano walikimbizwa hospitali ya mkoa Songea na kuwa wengine walibaki kituoni hapo.

Hata hivyo mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Abdula Lutavi ambaye naye alishuhudia tukio hilo, alisema kuwa tatizo hilo ni kubwa hivyo serikali wilayani humo, italifanyia uchunguzi wa kina.

Lutavi alisema licha ya watalamu kuchukua matapishi na mabaki ya vyakula hivyo kwa kwenda kuvipima, lakini taarifa za awali zinaonyesha kuwa sumu iliwekwa kwenye samaki.

Mkuu huyo wa wilaya ametoa onyo  kwa baadhi ya watu wa kijiji hicho,  ambao huvua samaki kwa kutumia sumu mbalimbali ikiwemo za zao la Tumbaku, kwa ajili ya kujipatia kitoweyo, sasa waache mchezo huo badala yake watumie a bora zinazokubalika katika uvuvi.

Kamanda wa polisi mkoani Ruvuma Deusdedith Nsimeki amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, na kwamba hivi sasa mtu mmoja anayejulikana kwa jina moja la Salum anashikiliwa kwa mahojiano zaidi kuhusiana na tukio hilo.

No comments: