Friday, August 16, 2013

WAANDISHI WA HABARI MKOANI RUVUMA WAPIGWA MSASA JUU YA MATUMIZI BORA YA INTANETI


Baadhi ya Waandishi wa habari wa mkoa wa Ruvuma, wakiwa katika picha ya pamoja na wawezeshaji waliokaa wawili kutoka kushoto, ni Sengiyuva Gasirigwa na Simon Berege wakati walipokuwa kwenye mafunzo ya Intaneti yaliyofanyika kwenye ukumbi wa VETA mjini Songea. Upande wa kulia aliyekaa ni Ngaiwona Nkondora mwandishi wa habari wa Radio Free Africa.  (Picha zote na Kassian Nyandindi)

Na Steven Augustino,
Songea.

WAANDISHI wa habari mkoani Ruvuma, wameonywa kuamini habari kutoka mitandaoni na kuzitumia kuhabarisha umma bila  kuzifanyia utafiti wa kutosha katika intaneti, na kutumia vyanzo vya kuaminika ikiwemo kuwahoji wahusika kupata habari za ukweli ambazo zitakuwa na manufaa kwa wasomaji.

Onyo hilo limetolewa na Simon Berege wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa namna ya kuandika habari kwa kutumia mitandao ya Intaneti na kutuma picha za kihabari  mtandaoni yanayoendeshwa katika Ukumbi wa Veta, Manispaa ya Songea mjini hapa, na Taasisi ya Vyombo vya habari kusini mwa Africa (Media Institute Of Southern Africa) MISA TANZANIA.

Wanahabari hao wamehitimu leo mafunzo hayo ambapo wamefundishwa namna ya kufanya utafiti wa vyanzo vya habari mbalimbali katika Intaneti, na kufungua njia nyingine za mawasiliano kama  ‘youtube’, Blogu na namna ya kuzitumia katika tasnia ya habari na kuzitengeneza zikiwa na takwimu sahihi.



Awali akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo ya siku tatu, afisa habari kutoka MISA -TANZANIA, Sengiyuva Gasirigwa,  alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wanahabari wa Ruvuma, ili waweze kwenda na wakati hasa katika teknolojia ya kimtandao.

Wanahabari hao pia wananolewa ili waweze kujua kwa undani maana ya interneti, ‘World Wide Web’, ‘Computer’,  na matumizi yake kwa manufaa ya maendeleo ya teknolojia, uchumi, siasa na utamaduni na kujali maadili ya kazi zao.

Gasiligwa alisema kuwa mafunzo hayo yanawahusisha Waandishi wa habari wa magazeti, televisheni na Rradio yanafanyika kwa ushirikiano wa MISATAN na shirika la VIKES  toka Finland, na kwamba kwa kuanzia mafunzo hayo yalifanyika mkoani Pemba huko Zanzibar, na sasa mkoani Ruvuma na baadaye mkoa wa Mwanza.

Kadhalika naye mwezeshaji wa mafunzo hayo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa,  Saimon Berege,  pamoja na mambo mengine aliwataka wanahabari kuwa na ari ya kujiendeleza kielimu na kuwakaribisha kwenda kusoma digrii ya pili (masters) inayotolewa na chuo hicho.

Kwa nyakati tofauti wanahabari hao nao waliipongeza taasisi hiyo kwa kuona umuhimu wa kutoa mafunzo hayo kwa waandishi wa habari, huku wakiongeza kwamba  kuanzia sasa wataweza kufanya kazi za uandishi wa habari wakiuchambuzi kwa kuoanisha habari kutoka vyanzo mbalimbali vya kimataifa, kuandika habari kwa kutumia takwimu kutoka katika mitandao na kutumia taarifa na hotuba zilizopita zilizotolewa na viongozi wa kimataifa duniani.

Aidha washiriki hao wameonyesha ushirikiano mkubwa katika uchambuzi wa
mada zilizotolewa na wameomba mafunzo kama hayo yaendelee kutolewa ili kuwajengea uwezo zaidi waandishi wa habari hapa nchini.












No comments: