Na Kassian Nyandindi,
Songea.
WANANCHI wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wameshtushwa na
kuwepo kwa wimbi la wasichana kutoka nje ya wilaya hiyo, wanaofika na kufanya
vitendo vya ukahaba katika mitaa mbalimbali nyakati za usiku huku wengine wakicheza muziki wakiwa nusu uchi kwenye nyumba za starehe maarufu kwa jina la Kangamoko, jambo
linalohofiwa kuongezeka kwa maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ukimwi.
Ilielezwa kuwa kundi hilo la makahaba linadaiwa kutoka mikoa
ya Mbeya, Tanga, Dar es Salaam na miji mingine mikubwa wamekuja Songea kwa
ajili ya kufanya biashara hiyo ya ukahaba, ambapo ikifika majira ya saa tatu
usiku wamekuwa wakijipanga katika mitaa mbalimbali kutafuta wanaume.
Makahaba hao ambao wanalalamikiwa wanakadiriwa kuwa na umri
kati ya miaka 18 hadi 30 ambao wamekuwa wakifanya shughuli hiyo isiyo rasmi
hasa katika mitaa maarufu ya Delux, Serengeti, Majimaji na barabara ya Sokoine,
huvaa nguo fupi na nyingine zinazoonesha maumbile ya miili yao kwa lengo la
kutaka kuwavutia wanaume, ambao hujikuta wakiingia mtegoni bila kutarajia
kutokana na ushawishi unaofanywa na wasichana hao.