Tuesday, July 16, 2013

MAMA PINDA AWATAKA WANATUNDURU KUZINGATIA ELIMU

Mama Tunnu Pinda.

























Na Steven Augustino,

Tunduru.

WAZAZI na walezi  wilayani Tunduru mkoani Ruvuma, wamehimizwa kupeleka watoto wao katika Kituo cha maendeleo KIUMA ili waweze kupata elimu na kuwawezesha kujiendeleza.

Wito umetolewa na mke wa Waziri mkuu Mama Tunnu Pinda, wakati akiwasalimia wananchi wa kijiji cha Milonde wilayani humo, muda mfupi baada ya Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa chuo cha ualimu ngazi ya Diploma  ambacho kinajengwa na taasisi hiyo.

Mama pinda alieleza kwamba endapo watapeleka vijana wao kupata elimu katika taasisi hiyo, pamoja na mafanikio watakayo yapata pia watalisaidia taifa la watanzania kwa kuongeza idadi ya wataalamu watakao toa huduma katika maeneo yao.

Alisema kitendo hicho kadhalika wananchi hao watakuwa wametoa mchango mkubwa wa maendeleo katika wilaya yao na mkoa kwa ujumla tofauti na sasa ambapo wilaya yao inakabiliwa na changamoto lukuki za kukosa wataalamu katika idara mbalimbali zinazotoa huduma katika jamii.

Awali akisoma taarifa ya kituo hicho, Mkurugenzi wa kituo hicho Dkt. Matomora Matomora alisema kituo hicho ambacho kinamilikiwa na Kanisa la Upendo wa Kristo Yesu masihi, kilijengwa mwaka 1996 kwa lengo la kutoa huduma mbalimbali katika eneo hilo, hadi sasa kimefanikiwa kujenga hospitali yenye vitanda 100 na kufanikiwa kuokoa maisha zaidi ya wanawake 150 kila mwaka ambao hujifungua kwa njia ya upasuaji.


Dkt. Matomora alibainisha kuwa huduma nyingine zinazopatikana katika kituo chake kuwa ni pamoja na chuo cha ufundi kinachotoa mafunzo na sasa zaidi ya mafundi 200 wa ujuzi wa aina mbalimbali hutolewa kwa mwaka, kinamiliki pia shule ya sekondari yenye kidato cha kwanza hadi cha sita, chuo cha uuguzi, chuo cha kilimo na mifugo na sasa kinajenga chuo hicho cha ualimu ngazi ya diploma kinacho tarajiwa kufunguliwa mapema Agosti 2014  mwakani, kwa kuanza na wanafunzi 320 huku uongozi husika ukiwa na malengo ya kupanua majengo yake na kuongeza idadi hiyo mara mbili zaidi kuanzia mwaka 2015 na kufikia wanafunzi 640.

Akifafanua upande wa huduma za hospitali Dkt. Matomora alisema kuwa  taasisi hiyo pia imejipanga kuhakikisha kuwa inaongeza idadi ya vitanda vyake kutoka 100 hadi 200 ili kuongeza ufanisi na kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya katika wilaya hiyo.

No comments: