Tuesday, July 16, 2013

MKUU WA POLISI WILAYA YA MBINGA ALALAMIKIWA NA ASKARI WAKE, IGP MWEMA AOMBWA KUINGILIA KATI

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgqbi07Mj110Eqpnq8-bl5Mpx8pQLStOaQgLzBvG0IEX36PSIAexQHHbm1O3UZW4XUHmybCaOa_ILQFMTzgK3mloNyZmwn99NOQ39XQOx4Ifd-Js4naFVNZDgoVzRBnhfUWUtTT9nvkXW8/s1600/Police1.jpg

 
Na Muhidin Amri,
Ruvuma.

BAADHI ya askari polisi kituo kikuu Mbinga mjini, wamemtuhumu Mkuu wa polisi wa wilaya hiyo(OCD) Justine Joseph, kuwa ni mtu anayetumia madaraka yake vibaya kwa kuendesha manyanyaso dhidi ya askari wa vyeo vya chini na kumuomba Mkuu wa Jeshi hilo hapa nchini Said Mwema, kumchukulia hatua za kinidhamu.

Askari wengine ambao hakutaka majina yao yatajwe katika mtandao huu walisema ni vyema kama kuna uwezekano, ahamishwe na kupewa kituo kingine cha kazi kabla hali haijawa mbaya.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, askari hao wamelalamikia kuwa OCD huyo amekuwa hana ushirikiano na baadhi ya askari wenzake na wakati mwingine hutoa lugha za dharau, na hata  zisizopendeza kwao hali inayowavunja moyo wa kufanya kazi  katika wilaya hiyo.
Walisema iwapo jeshi litashindwa kumchukulia hatua za kinidhamu huenda kukatokea sintofahamu na hawatoweza kuvumilia vitendo vinavyoendelea kufanywa na afisa huyo ikiwemo hilo la kuwatolea lugha za kihuni ambazo walidai kuwa ni sawa na kuwadhalilisha.
Aidha wameshauri hata maafisa wengine katika wilaya hiyo wanatakiwa kuondoka kwani wameshakaa Mbinga kwa muda mrefu, hivyo ni vyema wakapelekwa katika maeneo mengine hapa nchini.
Walisema kitendo cha maofisa hao kukaa muda mrefu katika kituo cha Mbinga wamekwisha jenga mazoea makubwa na raia, hivyo huwafanya washindwe kutimiza majukumu yao ya kazi ipasavyo. 
Wamelalamikia wakidai kuwa OCD Justine  ni mtu ambaye hapendi kushirikisha wenzake wakiwemo maafisa wa ngazi ya chini  jambo linalomfanya kutengwa na kujikuta yuko pekee.

"Huyu mkuu wetu ni tatizo ni vyema sasa serikali ikaangalia upya namna ya kutatua tatizo hili lililopo sasa hapa Mbinga, vinginevyo viongozi wa ngazi ya juu wakiendelea kulifumbia macho askari tutashindwa kufanya kazi zetu ipasavyo", walisema askari hao.  
Kwa upande wake Mkuu huyo wa polisi wilaya ya Mbinga Justine Joseph alipohojiwa hivi karibuni ofisini kwake na mwandishi wa habari hizi  alikanusha tuhuma hizo na kuziita kuwa ni unafiki unaofanywa na askari wachache waliozoea kula rushwa hasa kwa waendesha pikipiki jambo ambalo yeye hataki kusikia katika uongozi wake.
“Hizi tuhuma sio za kweli, zinafanywa na baadhi ya askari wangu hasa wale wala rushwa, nimekwisha elekeza wakikamata pikipiki waje na faini hapa au mmiliki wake sio kuleta pikipiki hatuna eneo la kupaki kwani hizi tulizonazo ni nyingi na hatuna sehemu ya kuzipeleka”, alisema Justine.
Naye Kamanda wa polisi mkoa wa Ruvuma Deusdedith Nsimeki alikiri kuwepo kwa malalamiko  hayo ya askari wa vyeo vya chini kituo cha Mbinga mjini, dhidi ya OCD wao na kuahidi kuwa atashughulikia tuhuma hizo ili kupata ukweli wa jambo hilo.
"Askari hatufanyi mambo kwa kukurupuka lazima tufanye uchunguzi  ili tujiridhishe, unajua ukishakuwa kiongozi unatakiwa kuwa makini  hasa  katika maamuzi ili usifanye mambo kwa kumuonea mtu, lazima utende haki kila wakati”, alisema Nsimeki.

No comments: