Saturday, July 13, 2013

WADAU WA KAHAWA WILAYANI MBINGA WAASWA KUZINGATIA TARATIBU ZA UNUNUAJI WA ZAO LA KAHAWA, MKUU WA WILAYA ASISITIZA ATAKAYEKIUKA KUKIONA CHA MTEMAKUNI

Upande wa kulia Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga akisisitiza jambo katika kikao cha Wadau wa kahawa kilichofanyika mjini hapa, katikati kutoka kulia ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Allanus Ngahi na kushoto ni Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Hussein Issa. (Picha na Kassian Nyandindi)




Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

MAKAMPUNI yanayojishughulisha na ununuaji wa kahawa katika msimu wa mwaka huu wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, yameaswa kufuata taratibu zilizowekwa katika mchakato wa utekelezaji wa zoezi hilo wilayani humo.

Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga alitoa agizo hilo katika kikao cha Wadau wa zao hilo kilichoketi jana Julai 12 mwaka huu, kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa.

“Nawaasa tufuate taratibu zilizowekwa, tusiwakope wakulima kahawa ninachohitaji hapa tuwalipe fedha zao taslimu, atakayekiuka hili tusije tukaonana wabaya”, alisisitiza Ngaga.

Sambamba na hilo Ngaga alisema hataki kuona biashara ya Magoma ikiendelea kufanyika wilayani Mbinga, na endapo atalibaini hilo yupo tayari kumchukulia hatua za kisheria mfanyabiashara ambaye atahusika kufanya hivyo.

Alisema biashara za mtindo huo hazina tija kwa mkulima wa kahawa, badala yake zimekuwa zikirudisha nyuma  maendeleo ya mkulima husika.


Kadhalika Mkuu huyo wa wilaya alitangaza bei ya kununua kahawa wilayani Mbinga, ambapo alisisitiza kwamba mtu yeyote asinunue kahawa mbivu chini ya bei ya shilingi 500 kwa kilo moja.

 Vilevile kwa upande wa kahawa kavu ambayo imekobolewa kwenye mitambo, inunuliwe kwa shilingi 2533 na kwa ile ambayo imekobolewa nyumbani kwa mkulima(Home Parchment) inunuliwe kwa shilingi 1900 kulingana na bei elekezi, iliyotolewa na Bodi ya kahawa Tanzania(TCB).

Ngaga aliongeza kuwa uchumi wa wilaya ya Mbinga kwa asilimia 80 unategemea zao la kahawa, hivyo uongozi wa wilaya hiyo unasisitiza wadau wa kahawa kuzingatia kanuni au sheria zilizowekwa katika kuliendeleza zao hilo, ili liweze kuwa endelevu kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Pamoja na mambo mengine Ngaga alifungua rasmi msimu wa kununua zao hilo wilayani humo, na kwamba hivi sasa makampuni yote yaliyokubaliwa kufanya biashara ya zao hilo wilayani Mbinga, sasa ni ruksa kupita kwa wakulima vijijini kununua kahawa.

No comments: