Saturday, July 13, 2013

WANANCHI WAMPORA ASKARI SMG NA RISASI 30


IGP Said Mwema. 

























Na Mwandishi wetu,
Singida.

BAADHI ya wananchi mkoani Singida wamempora askari polisi bunduki aina ya Sub Machine Gun (SMG) na risasi zake 30 baada ya kumshambulia askari huyo, kwa mawe na fimbo.

Kutokana na tukio hilo watu 18 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kupora silaha hiyo na risasi na bunduki hiyo ambayo ina namba za usajili 14300650.

Kamanda wa Polisi mkoani Singida, Geofrey  Kamwela alisema tukio hilo lilitokea majira ya saa 11:15, askari aliporwa silaha hiyo katika kijiji cha Milade, kata ya Iguguno, tarafa ya Kinyangiri wilayani Mkalama.


Kamanda Kamwela alifafanua kwamba askari wawili walikwenda kwenye kijiji hicho kwa lengo la kuchukua ng'ombe watano kama ushahidi ambao waliokuwa wameibwa katika kijiji cha jirani cha Mukulu wilayani Iramba.

Alisema kwamba baada ya ng'ombe hao kuibwa wananchi walifanikiwa kuwakamata pamoja na kumkamata mtuhumiwa Ramadhan Mohamed katika kijiji cha Milade na kumpeleka kwenye kituo kidogo cha polisi cha Iguguno.

Ng'ombe hao ni mali ya Samwel Mlata  (71) mkazi wa kijiji cha Mukulu. 

Lakini katika jambo la kushangaza polisi hao walipokwenda kwenye kijiji cha Milade, hawakuwakuta ng'ombe hao.

Baada ya kutowakuta askari hao na uongozi wa kijiji waliwafuatilia ng'ombe hao ili wakiwapata wawarejeshe mpaka kituo cha polisi kwa ajili ya kufuata taratibu.

Lakini baada ya kufanikiwa kuwapata ng'ombe hao wananchi waligoma kuwaachia ng'ombe hao.

Wakati wakiendelea na majadiliano mwananchi mmoja alimrukia askari wenye silaha katika miguu yake na kumwangusha chini na wananchi wengine walimshambulia kwa mawe na fimbo na kuangusha silaha chini.

Mwisho, wananchi walichukua silaha na ng'ombe na kuondoka. 

No comments: