Monday, July 22, 2013

PADRE WA KANISA KATOLIKI SEMINARI PERAMIHO JIMBO LA SONGEA ASWEKWA MAHABUSU KWA TUHUMA ZA UTAPELI

IGP Said Mwema.


















Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

PADRE wa Kanisa Katoliki Xavery Kazimoto Komba, amekamatwa na kuwekwa mahabusu katika kituo kikuu cha polisi wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, kwa tuhuma ya kuwatapeli wakulima kahawa yenye thamani ya shilingi milioni 95.

Habari zinaeleza kuwa mchungaji huyo ambaye ni wa Seminari kuu Peramiho jimbo la Songea, amesota mahabusu kwa siku tatu ambapo anadaiwa kuchukua kahawa ya wakulima hao na kutokomea nayo kusikojulikana.

Komba anatuhumiwa kukusanya kahawa kilo 25,000 yenye thamani ya fedha hizo, katika vikundi vitano vya wakulima, msimu wa mavuno wa mwaka 2012 na 2013 kwa lengo la kwenda kuuza na baadaye aweze kurejesha malipo halali ya wakulima hao.

Vikundi ambavyo alikusanya kahawa na kutokomea nayo bila kurejesha malipo yao ni Lutondo, Muungano Lituru, Jaribio Lunoro, kipando na Otmary vilivyopo wilayani Mbinga.

Imeelezwa kuwa Padre huyo amekuwa akifanya biashara ya zao hilo kupitia kampuni yake ya Songea network, lakini cha kushangaza baada ya kukusanya kahawa ya vikundi hivyo, hadi leo hii hajarejesha fedha hizo kwa wakulima wa vikundi hivyo.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma Deusdedith Nsimeki, amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kwamba alieleza kuwa yupo bado mahabusu wakati wowote kuanzia leo atafikishwa Mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika, ambao unafanywa na kitengo cha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) wilayani Mbinga.

Nsimeki alisema anafanyiwa uchunguzi chini ya kifungu kikuu namba 15 cha sheria ya kuzuia na kupambana rushwa cha mwaka 2007.

Hata hivyo alipotafutwa Kamanda wa TAKUKURU mkoani Ruvuma Daud Masiko, ili aweze kutolea ufafanuzi juu ya tukio hilo hakuweza kupatikana na simu yake ilikuwa ikiita muda mrefu bila kupokelewa.

No comments: