Thursday, July 4, 2013

MAMENEJA WANAOSIMAMIA MITAMBO YA KUKOBOA KAHAWA MBIVU VIJIJINI WILAYANI MBINGA, WATAKIWA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAO IPASAVYO ILI KUBORESHA KIWANGO CHA UBORA WA KAHAWA WILAYANI HUMO


Mtaalamu wa mimea na udongo Kaminyoge Mhamerd wa Kampuni ya Sustainable Harvest, kutoka wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro ambayo hujishughulisha na uboreshaji wa zao la Kahawa, akitoa mafunzio juu namna ya uendeshaji kwa ufanisi wa mitambo ya kukoblea kahawa kwa Mameneja wa vikundi vinavyozalisha kahawa bora wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, mafunzo ambayo yamefanyika kwenye ukumbi wa Kilicafe uliopo mjini hapa.


Kaminyoge Mhamerd akiwaelekeza Mameneja mitambo juu ya kahawa inayostahili kupokelewa mtamboni mara baada ya kuchumwa kutoka shambani.


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

VIONGOZI wanaosimamia mitambo ya kukoboa kahawa vijijini, wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kuwa makini katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi ili kuweza kuongeza ubora, wa uzalishaji wa  kahawa wilayani humo.

Sambamba na hilo Mameneja waliopo katika mitambo hiyo ambao ndio wasimamizi wakuu juu ya uendeshaji wa mitambo, hivyo nao wameshauriwa 
kufanya kazi kwa ukaribu na wakulima wanaozalisha zao hilo.

Rai hiyo imetolewa na mtaalamu wa mimea na udongo Kaminyoge Mhamerd wa Kampuni ya Sustainable Harvest, kutoka wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro ambayo hujishughulisha na uboreshaji wa zao la Kahawa, katika mafunzo ya siku moja yaliyoshirikisha Mameneja wa mitambo ya kukobolea kahawa wilayani Mbinga, ambayo yamefanyika kwenye ukumbi wa Kilicafe uliopo mjini hapa.


Alifafanua kuwa Mameneja hao wasipozingatia majukumu yao ipasavyo, ubadhirifu katika mitambo hiyo unaweza ukatokea na kusababisha kuua vyama vya ushirika na vikundi ambavyo hupeleka kahawa mbichi katika mitambo hiyo, kwa ajili ya kukobolewa.

“Ndugu zangu uwazi kati ya mameneja na wahasibu wa mitambo inatakiwa uzingatiwe ili kuepukana na vitendo vya wizi wa kahawa, jengeni ushirikiano na uaminifu tuweze kuendeleza ubora wa zao hili”, alisisitiza Kaminyoge.

Aidha aliongeza kuwa uhai wa vikundi katika mitambo ni makusanyo ya kahawa bora, na watendaji wa vikundi husika kufanya kazi kwa kutumia ubunifu wa hali ya juu, ili kuepukana na malalamiko yasiyokuwa ya lazima miongoni mwa jamii.

Pia alieleza kwamba vibarua wanaofanya kazi mitamboni inatakiwa wasimamiwe kikamilifu kwa kuhakikisha wanafanya kazi kwa muda waliopangiwa, na kwamba Meneja aliyekuwa katika mtambo husika kila siku ahakikishe anapofunga kituo cha mtambo anatakiwa awe anafanya kikao na wasaidizi wake, kwa kutoa taarifa za utendaji wa kazi iliyofanyika kwa siku nzima.

Pamoja na mambo mengine Mameneja walioshiriki katika mafunzo hayo walitoka katika vikundi vinavyozalisha kahawa bora wilayani Mbinga, ambavyo ni Unango, Lumeme, Jikwamue, Chemichemi, Mikalanga, Bagamoyo, Jitahidi na Ukombozi.


No comments: