Wednesday, July 31, 2013

MAHAKAMA KUINGILIA KATI MGAWANYO WA MALI MBINGA, MADIWANI WASEMA HAWAKUBALIANI NA MCHAKATO WA UGAWAJI

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Hussein Ngaga akijibu hoja za madiwani katika kikao kilichoketi leo mjini hapa katika ukumbi wa Jumba la maendeleo, ambapo madiwani hao walisitisha mara moja mgawanyo wa mali kati ya wilaya hiyo na wilaya mpya ya Nyasa, kutokana na kubaini kuna mbinu chafu zimetumika katika mgawanyo huo.

Baadhi ya madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, wakimsikiliza kwa umakini Mkurugenzi wao wakati alipokuwa akijibu hoja zao za msingi, ambazo ziliwasilishwa katika kikao hicho cha baraza la madiwani kilichoketi leo mjini hapa.                                          (Picha zote na Kassian Nyandindi)


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida Baraza la Madiwani, Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, limesitisha zoezi la mgawanyo wa mali kati ya wilaya hiyo na wilaya mpya ya Nyasa, kutokana na zoezi hilo kuonekana kuingiliwa na vitendo vinavyoashiria kuwepo kwa upendeleo wa upande mmoja, na wenye kulenga njia za siri na ujanja ujanja.

Aidha usitishaji huo umefuatia Madiwani hao kubaini kuwa aliyekuwa Mkurugenzi wa wilaya ya Mbinga Shaibu Nnunduma, ametumia mbinu za ujanja katika kutengeneza makabidhiano(Handing Over) kwa Mkurugenzi mpya wa wilaya hiyo Hussein Ngaga, ambayo yanalenga asilimia kubwa ya mali zilizopo Mbinga zipelekwe Nyasa.

Hali hiyo imejitokeza leo katika kikao cha baraza hilo kilichoketi kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa, kikao ambacho ni cha kawaida chenye kulenga kujadili maendeleo mbalimbali ya wilaya hiyo.

Mbunge wa Jimbo la Mbinga, Gaudence Kayombo akichangia hoja katika kikao hicho alisema, endapo uongozi wa wilaya hiyo na mkoa huo kwa ujumla utaendelea kulifumbia macho suala la mgawanyo halali wa mali za halmashauri za wilaya ya Mbinga na Nyasa, baraza la madiwani la wilaya ya Mbinga lipo tayari suala hili kulifikisha mahakamani ili haki iweze kupatikana.

Alisema jambo hili hata yeye binafsi linamsikitisha kwa jinsi lilivyofanyika, hivyo hakubaliani nalo na sasa tayari amekwisha ongea hata na uongozi wa makao makuu ya Tawala za mikoa na serikali za mitaa(TAMISEMI) ili waweze kuja na kulifanyia kazi.

“Kuhusu mgawanyo huu wa mali hata mimi unanisikitisha, nimeongea na mkoa na TAMISEMI wamesema wanakuja kushughulikia suala hili, na kwa kweli nasema jambo hili linaonesha kuna ujanja ujanja umefanyika na sisi kama madiwani wa Mbinga, hatutakubali kuona linaendelea”, alisema Kayombo.

Mbunge huyo alisisitiza akisema, mali hizo ni vyema zigawanywe kwa uwiano ulio sawa, huku akiongeza kuwa pasipo kufanya hivyo itakuwa ni ulafi ambao unadhihirisha wazi kwamba, mtu mmoja anataka kujilimbikizia mali nyingi wakati Mbinga nayo inabidi isonge mbele kimaendeleo.


Kadhalika Diwani wa Kata ya Utiri Hyasint Ndunguru, naye alinyoshea kidole suala hilo alisema, kuna siri kubwa imejificha juu zoezi hilo la mgawanyo wa mali huku akieleza kuwa kamati ya mgawanyo wa mali anamashaka nayo haikutenda haki wakati ilipoketi ikifanya mchakato wa zoezi hilo.

“Mheshimiwa mwenyekiti, mimi binafsi ninamashaka katika ugawaji wa mali hizi, magari mengi wameyachukua lakini cha kushangaza madeni wametutupia sisi peke yetu huku Mbinga tuyalipe na wao wasiyalipe, mimi siwezi kuunga mkono jambo hili, vizuri lifanyiwe kazi upya kwa kufuata taratibu nzuri”, alisema Ndunguru.

Naye Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Allanus Ngahi aliunga mkono kwa kusema kuanzia sasa wanasitisha kazi ya mgawanyo wa mali kati ya wilaya hizo mbili, (Mbinga na Nyasa) hadi kamati husika itakapoketi na kuridhia uhalali wa mgawanyo huo.

Pamoja na mambo mengine, hoja hii ya mgawanyo wa mali katika baraza hilo la Madiwani la halmashauri ya wilaya ya Mbinga ililetwa na madiwani hao katika baraza hilo, ikiwa katika mfumo wa hoja binafsi ili iweze kujadiliwa na kusitishwa mara moja kwa mgawanyo huo hadi hapo baadaye Kamati husika, itakapoketi na kufanya tena upembuzi yakinifu juu ya mgawanyo wenye uwiano sawa ambao hautaweza kuleta mtafaruku miongoni mwa madiwani wa wilaya ya Mbinga na Nyasa.

No comments: