Monday, July 15, 2013

PINDA: BARABARA YA KUTOKA NAMTUMBO TUNDURU KUJENGWA OKTOBA MWAKA HUU

Waziri mkuu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mizengo Pinda.



Na Dustan Ndunguru,
Tunduru.

WAZIRI mkuu Mizengo Pinda amesema kazi ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Namtumbo hadi Tunduru ,yenye urefu wa kilometa 193 itaanza Oktoba mwaka huu ambapo kukamilika kwake kutasaidia wananchi waepuke kero mbalimbali wanazokabiliana nazo kwa sasa.

Akiongea mara baada ya kukagua ujenzi wa chuo cha ualimu Kiuma kilichopo katika kijiji cha Milonde tarafa ya Matemanga wilayani humo, na ambacho kinamilikiwa na taasisi ya Dkt. Matomora alisema ujenzi wa barabara hiyo kimsingi ungekuwa unaendelea vizuri lakini ulikwamishwa na mkandarasi aliyepewa kazi hiyo awali Progressive kutoka India.

Alisema serikali inalifahamu tatizo hilo kubwa kwa wananchi wa mkoa huo hususani katika wilaya za Namtumbo na Tunduru hasa baada ya mkandarasi huyo kusuasua kuijenga barabara hiyo kwa wakati na kwamba kutokana na hilo kampuni hiyo imenyang'anywa kazi hiyo na kupewa mtu mwingine ambaye atafanya kazi hiyo kwa uaminifu.


"Naomba wananchi msiwe na wasiwasi serikali yenu itahakikisha barabara kutoka Namtumbo hadi Tunduru inakamilika kwa kiwango cha lami kama ilivyopangwa,naomba msiwasikilize wale ambao wanapita huku na kuwadanganya kuwa serikali imewasahau", alisema Pinda.

Kwa mujibu wa waziri mkuu fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo zipo na kwamba pia barabara kutoka Tunduru hadi Mangaka yenye urefu wa kilometa 140 itajengwa kwa kiwango cha lami, ambapo kukamilika kwa ujenzi wa barabara hizo kutapelekea wananchi wa wilaya hiyo kuongeza hata uzalishaji wa mazao mbalimbali ya biashara kutokana na ukweli kwamba watakuwa na uhakika wa kusafirisha kiurahisi kwenda kwenye masoko.

Katika hatua nyingine Pinda alisema serikali itaendelea kutambua michango mbalimbali inayotolewa na taasisi binafsi, ikiwemo katika sekta ya elimu kwani jukumu la kuwaelimisha watanzania ni la wote na kwamba kuiachia serikali pekee ni kuitwisha mzigo.

Akizungumza mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa chuo cha ualimu Kiuma ambacho kwa mwaka wa kwanza baada ya kukamilika kitachukua wanafunzi 300 wa diploma ya ualimu, alisema kujengwa kwa chuo hicho ni mfano mzuri wa kuigwa kutokana na ukweli kwamba wahitimu wake watasaidia kuondoa changamoto ya uhaba wa walimu kwa shule za msingi na sekondari hapa nchini.

Pinda aliwataka watu binafsi na taasisi zote nchini kuendelea kushirikiana na serikali yao katika kuwaletea maendeleo watanzania na kwamba kamwe wasiwaunge mkono wale wote ambao, siku zote wamekuwa wakibeza kila linalofanywa na serikali kwa wananchi wake.

Kuhusu zao la korosho alisema ili kuepukana na tatizo la ukosefu wa soko la uhakika mipango inafanyika ili badala ya kuwategemea wanunuzi binafsi kununua kwa wakulima kiwanda cha kubangua zao hilo kipewe jukumu la kununua moja kwa moja kwa wakulima jambo ambalo litapelekea wakulima waondokane na adha wanayoipata sasa.

Alisema wakulima hawapaswi kukata tamaa ya kuendelea kuitunza miti ya mikorosho kwani serikali yao ipo imara kuhakikisha hali hiyo ambayo ilijitokeza inakwisha na kwamba wataalamu wa kilimo waendelee kutoa elimu kwa wakulima ili hatimaye waweze kuzalisha mazao bora ambayo yatapelekea wapate bei nzuri sokoni.

Alisisitiza juu ya kuimarisha mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani ambapo kwa kufanya hivyo mkulima atakuwa na uhakika wa kupata mkopo wakati huo mazao yake yapo ghalani yakisubiri bei nzuri na kwamba wakulima wenyewe wajiunge pamoja na kuanzisha vikundi na kuimarisha vyama vyao vya ushirika hali ambayo itawafanya wauze mazao yao kwa pamoja.


No comments: