Tuesday, July 16, 2013

SERIKALI KUBORESHA VIWANDA VYA KUBANGULIA KOROSHO NCHINI

Watoto wakichambua korosho.

















Na Steven Augustino,

Tunduru.

SERIKALI imeahidi kufanya uchunguzi wa kina katika viwanda 10 vilivyo jengwa kwa ajili ya kubangulia korosho za wakulima nchini, ikiwa ni juhudi ya kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa kero ya kukosekana kwa soko la uhakika la zao hilo.

Sambamba na ahadi hiyo ya serikali pia imewahakikishia wakulima wanaozalisha zao hilo kote nchini,  kuwa itatoa fedha katika kipindi cha miezi miwiIi ijayo  baada ya utafiti huo kufanyika,  ili kuviwezesha viwanda hivyo kununuaa mitambo mipya ya kisasa ambayo itarahisisha kazi ya ubanguaji wa korosho.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mizengo Pinda alisema hayo wakati akizungumza na wananchi wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, na kuongeza kuwa serikali imebaini kuwa kuna changamoto lukuki ambazo wakulima wa zao la korosho wamekuwa wakikabiliana nazo na kurudisha nyuma maendeleo yao.  

Pia alieleza kuwa serikali imebaini kuwa utaratibu wa kutumia stakabadhi ghalani ambao uliwekwa kwa ajili ya kuwalipa fedha zao wakulima wa zao hilo katika awamu tatu kutoonesha mafanikio na hata ukiachwa uendelee kwa muda mrefu hautawaletea tija wakulima hao.


Aidha katika hotuba hiyo pia Waziri pinda akaeleza kuwa katika kuonesha kuwa maamuzi hayo siyo nguvu ya soda, alisema kuwa serikali imejipanga kutoa fedha katika viwanda hivyo na kuviwezesha kununua vyenyewe korosho kutoka kwa wakulima ili kukata mirija ya unyonyaji kwa kuwaondoa wakulima hao katika mikono ya wanyonyaji.

Katika taarifa hiyo Waziri huyo alisisitiza kwamba kufuatia hali hiyo tayari serikali imekwisha unda kikosi kazi cha watu watano kitakachosimamiwa na Katibu mkuu wa kutoka katika Ofisi yake, na kwamba kazi ya kwanza itakuwa ni kupita katika viwanda hivyo  na kuchunguza kwa kina matatizo yanayokwamisha visiweze kuendelea.

Hata hivyo Pinda ambaye alikuwa akihutubia wananchi katika uwanja wa Tunduru mjini, alisema fedha zitakazotolewa na serikali katika kukuza maendeleo ya viwanda hivyo, zitaelekezwa zaidi katika ununuaji wa mitambo mipya ya kubangulia korosho za wakulima.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda leo ameondoka wilayani Tunduru, akiendelea na ziara yake mkoani Ruvuma akielekea sasa wilayani Namtumbo.  

No comments: