Thursday, July 11, 2013

WANANCHI WA MBINGA WATAKIWA KUSHIRIKI KIKAMILIFU KATIKA SHUGHULI ZA KIMAENDELEO

Gaudence Kayombo, Mbunge wa jimbo la Mbinga.





















Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WITO  umetolewa kwa wananchi katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na  kutoa mawazo yao mapya ambayo yataijenga upya wilaya hiyo na kuendeleza shughuli za kiuchumi kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

Pia wametakiwa kuwa mstari wa mbele na kuacha malalamiko yasiyokuwa na manufaa kwao kwani hayatasaidia kuongeza  uzalishaji  au kuleta maendeleo katika jamii hivyo endapo watafanya hivyo  wanaweza kuirudisha nyuma wilaya hiyo ambayo ni tegemeo kubwa kwa uchumi mkoani Ruvuma.

Kauli hiyo ilitolewa na Mbunge wa jimbo la Mbinga Gaudence Kayombo wakati alipokuwa akizungumza katika kikao cha dharula cha baraza la Madiwani kilichoketi kwenye ukumbi wa jumba la maendeleo uliopo mjini hapa.

Kayombo alisema kila mmoja anaowajibu  mkubwa kutoa mawazo au michango mbalimbali  kwa viongozi na watumishi wa halmashauri ya wilaya hiyo, ili wasaidiane katika kuijenga wilaya badala ya jukumu hilo kuliacha kwa watu wachache huku akisisitiza viongozi kutanua wigo  katika kuwahudumia wananchi na kuacha tabia ya kujifanya Miungu watu.


Vilevile Mbunge huyo amewakumbusha  watumishi na wataalamu wote katika halmashauri hiyo kutimiza wajibu wao katika kushauri na kujenga ubunifu kwa kubuni hata vyanzo vya mapato ambavyo vitasaidia kupata fedha za kutosha ambazo zitawahudumia wananchi katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo.

Kadhalika alisisitiza kuyahudumia makundi mbalimbali maalum yenye kuhitaji mahitaji muhimu katika kuishi, kama vile walemavu, wajane, vijana na  yale mengine ambayo yanahitaji kujinasua katika kuondokana na lindi la umasikini unaowakabili miongoni mwao.

Alisema kwa muda mrefu makundi hayo yamesahaulika hivyo muda umefika kwa viongozi kuyaangalia kwa lengo la kutaka kuyapunguzia mzigo wa matatizo waliyonayo na sio kuyaacha pekee.

Amewaagiza madiwani kuwa mstari wa mbele katika mapambano  dhidi ya umasikini na kwenda kuongeza umakini katika usimamizi na ufuatiliaji wa fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo vijijini, ili fedha zinazopelekwa na serikali huko ziweze kufanya kazi iliyokusudiwa.

Kayombo amewasihi wanaporudi katika maeneo yao kwenda kuwashirikisha wananchi kwa kila jambo la maendeleo na  wawe wabunifu.

No comments: