Tangaza Biashara yako nasi kwa Matangazo ya aina mbalimbali, Mawasiliano zaidi piga simu namba 0762 578960
Wednesday, October 28, 2015
MEYA MANISPAA YA SONGEA ASHINDWA KUTETEA KITI CHAKE
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
ALIYEKUWA Mstahiki Meya wa Halmashauri
ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, Charles Mhagama katika kipindi kilichopita
ameshindwa kutetea kiti chake cha udiwani kata ya Matogoro kupitia tiketi ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Manispaa hiyo, baada ya mgombea udiwani wa kata
hiyo kutoka Chama cha Wananchi (CUF) Alawi Kawelea, kuibuka mshindi.
Msimamizi wa uchaguzi Jimbo la
Songea, Raphael Kimari alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake
alisema CCM kimefanikiwa kushinda kata 16, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
kimeshinda kata 4 na CUF kimeshinda kata 1 ambapo jimbo hilo lina jumla ya kata
21.
Charles Mhagama. |
Kimari aliwataja washindi wa Chama
Cha Mapinduzi na kata zao kwenye mabano, kuwa ni Oddo Mbunda (Mjimwema), Festo
Mlelwa (Seedfarm), Mshawej Hassan (Subira), Maurus Lungu (Mletele), Yobo Mapunda
(Lilambo), Lotari Mbawala (Mshangano), Cresensia Kapinga (Ndilimalitembo) na
Osmund Kapinga wa kutoka kata ya Mwengemshindo.
Aliwataja wengine kuwa ni Wilbart
Mahundi (Ruhuwiko), Ismail Aziz (Misufini), Shaib Kitete (Mjini), Hussein
Abukadi (Majengo), George Oddo (Lizaboni), Golden Sanga (Bombambili), Izack
Lutengano (Msamala) na Mussa Mwakaja kata ya Mateka.
Tuesday, October 27, 2015
TUNDURU SONGEA CCM YAZIDI KUNG'ANG'ANIA MAJIMBO YAKE
Na Steven Augustino,
Ruvuma.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) katika wilaya ya Tunduru na Songea
mkoani Ruvuma, kimeendelea kung’ang’ania majimbo yake na kata kwa ujumla baada
ya wagombea wake kwa nafasi ya diwani, ubunge na rais kuongoza kwa kura nyingi.
Wakitangaza kwa nyakati tofauti wasimamizi wa uchaguzi katika
majimbo ya Tunduru Kusini, Kaskazini na Songea walisema kuwa wagombea wa chama
hicho ndio walioibuka kidedea katika matokeo ya uchaguzi huo, uliofanyika
Oktoba 25 mwaka huu.
Wilayani Tunduru msimamizi wa uchaguzi, Mkurugenzi mtendaji wa
Halmashauri ya wilaya hiyo, Tinna Sekambo aliwatangaza Daimu Mpakate kupitia
Chama Cha Mapinduzi kuwa mshindi wa nafasi ya ubunge, jimbo la Tunduru Kusini
baada ya kupata kura 27,486.
Monday, October 26, 2015
MANYANYA AIBUKA KIDEDEA JIMBO LA NYASA
Injinia Stella Manyanya |
Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.
TAARIFA zilizotufikia hivi punde Jimbo la Nyasa lililopo wilayani
Nyasa mkoa wa Ruvuma, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaendelea kuongoza na
kupeperusha bendera yake kwa nafasi ya kiti cha udiwani, ubunge na rais dhidi
ya vyama vya upinzani.
Mkurugenzi msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo, Jabir
Shekimweri amezungumza na mwandishi wa habari hizi na kueleza kwamba kwa nafasi
ya udiwani, mpaka sasa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeweza
kuchukua kata mbili kati ya 18 zilizopo wilayani humo na matokeo kwa ngazi hiyo
ya udiwani, bado yanapokelewa kutoka katika kata mbalimbali.
Alisema jimbo la Nyasa lina idadi ya wapiga kura 70,766 na
kwamba waliojitokeza kupiga kura walikuwa 45,838.
CCM MBINGA YAIBUKA KIDEDEA MATOKEO YA UCHAGUZI YATANGAZWA
Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,
kimeibuka kidedea baada ya wagombea wake kwa nafasi ya diwani, ubunge na rais
kuongoza kwa kura nyingi katika vituo vyake vya kupigia kura.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wetu umebaini kuwa Jimbo la
Mbinga mjini na vijijini uchaguzi ulifanyika kwa amani na utulivu, huku
wananchi ambao ni wapiga kura wakijitokeza kwa wingi kupiga kura katika vituo
husika.
Matokeo yametangazwa leo majira ya mchana, katika kituo cha utafiti
wa zao la kahawa TaCRI – Ugano kilichopo Mbinga mjini ambako Wakurugenzi wa Tume
ya uchaguzi katika majimbo hayo, waliweka kambi huko wakifanya kazi ya
kujumlisha matokeo ya wagombea.
Akitangaza matokeo kwa jimbo la Mbinga mjini, Mkurugenzi msimamizi
wa uchaguzi Oscar Yapesa alisema kuwa jimbo hilo lina idadi ya wapiga kura
61,833 likiwa na kata 19 na vituo vya kupigia kura 165 na kwamba waliojitokeza
kupiga kura walikuwa 42,706, kura halali 41,442.
UCHAGUZI JIMBO LA MBINGA MJINI NA VIJIJINI WAENDESHWA KWA AMANI NA UTULIVU MATOKEO KUTANGAZWA LEO
Na Kassian
Nyandindi,
Ruvuma.
HALI ya uchaguzi katika Jimbo la Mbinga mjini na vijijini
mkoani Ruvuma, limeendeshwa kwa amani na utulivu, huku wananchi ambao ni wapiga
kura wakijitokeza kwa wingi kupiga kura.
Mwandishi wetu ambaye ametembelea katika maeneo mbalimbali ya
vituo vya kupigia kura, ameshuhudia hali ikiwa shwari licha ya kuwepo kwa changamoto
ndogo ndogo wakati zoezi hilo linaendeshwa.
Changamoto hizo ni kwamba baadhi ya wafuasi wa vyama vya
siasa, ambao wanadaiwa kutoka vyama vya upinzani, walikuwa wakionekana katika
vituo wakifanya kampeni na kupiga kelele.
Hali hiyo imeshuhudiwa katika kata ya Mpepai na Mbangamao jimbo la Mbinga mjini,
ambapo askari wa kikosi cha kutuliza ghasia, walikwenda huko na kufanikiwa
kuzima kelele hizo.
Saturday, October 24, 2015
ASKARI MAGEREZA WAFARIKI BAADA YA KUPATA AJALI
Na Kassian Nandindi,
Songea.
ASKARI wawili wa Jeshi la magereza, gereza la mifugo la
Majimaji lililopo wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wamefariki dunia baada ya
pikipiki waliyokuwa wanasafiria kuacha njia na kupinduka.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela |
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Mihayo Msikhela aliwataja
askari hao waliopoteza maisha kuwa ni B 7303(Wader) Oscar Henry (29) na B 5361
CPL Geofrey Mwambigija (26) wote ni askari wa gereza hilo.
Alisema siku hiyo ya tukio, kwenye barabara inayotoka Tunduru
kwenda Masasi pikipiki isiyofahamika namba za usajili ambayo ilikuwa
ikiendeshwa na B 7303(Wader) Oscar Henry ikiwa kwenye mwendo kasi ilianguka na
kusababisha vifo vyao.
WATAWANYWA KWA MABOMU YA MACHOZI BAADA YA KULETA VURUGU
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
KUNDI la watu linalodaiwa kuwa ni la wafuasi wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) limevamia eneo la soko la wakulima
lililopo Mbinga mjini mkoani Ruvuma, na kung’oa kisha kuchana bendera 50 za Chama
Cha Mapinduzi (CCM) zenye thamani ya shilingi 200,000 kutokana na chuki za
kisiasa zilizopo wilayani humo.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake, Kamanda wa Polisi
mkoani humo, Mihayo Msikhela alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya
asubuhi huko wilayani Mbinga.
Alifafanua kuwa inadaiwa siku hiyo ya tukio, kundi hilo lilikwenda
kwenye eneo hilo na kufanya vurugu kisha kungo’a milingoti iliyowekwa bendera
na kuzichana jambo ambalo lilisababisha kuwepo kwa vurugu kubwa kati ya wafuasi
wa CHADEMA na wa CCM.
Friday, October 23, 2015
MWAMBUNGU: PIGENI KURA NA KURUDI NYUMBANI
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu. |
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
YAKIWA yamebaki masaa machache Watanzania kushiriki katika kinyang’anyiro
cha uchaguzi mkuu, Serikali mkoani Ruvuma imewataka wananchi wake mkoani humo,
Oktoba 25 mwaka huu kushiriki kikamilifu kupiga kura katika kituo husika
walichojiandikisha na mara baada ya kukamilisha zoezi hilo, waondoke na kurudi
nyumbani.
Mkuu wa mkoa huo, Said Mwambungu alisema hayo leo alipokuwa
akizungumza na madereva wa pikipiki maarufu kwa jina la Yeboyebo, katika ukumbi
wa Songea Club uliopo mjini hapa.
“Nawasihi sana, mkisha piga kura ondokeni katika eneo la
kituo na kuwaacha mawakala wa vyama husika wakilinda kura zenu”, alisema
Mwambungu.
TUNDURU KASKAZINI KUMCHAGUA MANJOLO
Na Steven Augustino,
Tunduru.
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, baadhi ya vijana wa Chama cha
Mapinduzi (CCM) katika Jimbo la Tunduru Kaskazini wilayani Tunduru mkoa wa
Ruvuma, wameanzisha utaratibu wa kupita nyumba kwa nyumba ili kumsaidia kufanya
kampeni mgombea ubunge, kupitia tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF) Manjolo
Kambili ambaye anaungwa mkono na UKAWA.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwa masharti ya kutotajwa
majina yao walisema, walisema kuwa maamuzi hayo wameyachukua baada ya kubaini
kuwa mgombea ubunge aliyeteuliwa kupeperusha bendera ya Chama Cha Mapinduzi,
Mhandisi Ramo Makani kuwa hawamtaki.
Walisema wamelazimika kuingia katika mapambano hayo, ili
kuhakikisha kuwa mgombea huyo wa CCM, anang'olewa kupitia Sanduku la kura katika
uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Wednesday, October 21, 2015
AMTWANGA NA MCHI KICHWANI NA KUSABABISHA MAUAJI
Na Steven Augustino,
Tunduru.
MKAZI mmoja wa kitongoji cha Makombe kijiji cha Milonde kata
ya Matemanga wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, Mohamed Mawazo (43) anashikiliwa
na Polisi kwa tuhuma ya mauaji.
Taarifa za tukio hilo, zinasema kuwa mtuhumiwa huyo
anashikiliwa akidaiwa kumuua Zuberi Issa kutokana na kipigo alichokipata kutoka
kwa mtuhumiwa huyo ambaye alimpiga kwa kutumia mchi wa kutwangia, kutokana na wivu
wa kimapenzi.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Revocatus Malimi. |
Kwa mujibu wa taarifa hizo, mtuhumiwa huyo alifanya kosa hilo
kwa kumtwanga nao kichwani kitendo ambacho kilimsababishia kufikwa na mauti.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Revocatus Malimi alisema
kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa Oktoba 16 mwaka huu.
Alisema baada ya mtuhumiwa huyo kufanya shambulizi hilo,
alikwenda kuripoti kwa Mwenyekiti wa kitongoji cha Makombe, Said Mussa huku
akitamba kuwa tayari amekwisha mpiga mtu aliyekuwa anamtuhumu kwamba anatembea
na mke wake, ambaye ni miongoni mwa wake zake watatu.
ASKARI WAASWA KUTOTUMIA NGUVU WAKATI WA UCHAGUZI
Na Steven Augustino,
Tunduru.
ASKARI ambao watashiriki katika jukumu la kulinda amani na
utulivu, siku utakapofanyika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu, wametakiwa
kupunguza matumizi ya nguvu zisizokuwa za lazima katika uchaguzi huo.
Mkuu wa Polisi wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Nicolaus
Mwakasanga alisema hayo alipokuwa akifungua juzi mafunzo elekezi yaliyoshirikisha
askari polisi, magereza, uhamiaji na mgambo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa
Hospitali ya wilaya hiyo mjini hapa.
Mwakasanga alisema kuwa lengo la mafunzo hayo, ni kuweza
kufanikisha na kuhakikisha kwamba uchaguzi huo unakwenda salama.
Tuesday, October 20, 2015
WAUGUZI WATAKIWA KUZINGATIA MAADILI YAO
Na Muhidin Amri,
Songea.
MKURUGENZI mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Songea
vijijini mkoani Ruvuma, Sixbert Kaijage amewataka Wauguzi wanaofanya kazi ndani
ya halmashauri hiyo kujituma na kutekeleza majukumu ya kazi zao ipasavyo,
ili waweze kuboresha huduma husika kwa jamii, jambo ambalo litawafanya waweze
kuepukana na malalamiko yasiyokuwa ya lazima.
Alisema kufanya hivyo kutasaidia wilaya hiyo, kusonga
mbele kimaendeleo kwa haraka zaidi, na wananchi kufanya shughuli zao wakiwa na
afya nzuri.
Kaijage alisema hayo mwishoni mwa wiki alipokuwa katika
kijiji cha Lundusi, mji mdogo wa Peramiho, wakati alipokuwa akizungumza na
wakazi wa kijiji cha Maposeni wilayani humo kuhusiana na serikali
ilivyojipanga kukabiliana na changamoto mbalimbali, za kiutendaji kwa watumishi
wa halmashauri hiyo.
Saturday, October 17, 2015
MAMIA WAMUAGA MBUNGE DEO FILIKUNJOMBE NYUMBANI KWAKE KIJICHI DAR ES SALAAM
Waombolezaji
wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Ludewa,
Deogratias Filikunjombe wakati wa ibada ya kuuaga iliyofanyika nyumbani
kwake Kijichi Dar es Salaam leo mchana.
Majeneza
yenye miili ya aliyekuwa Mbunge wa Ludewa, Deogratias Filikunjombe na
ndugu zake, Plasdus Ngabuma na Casablanga Haule yakiwa yamewekwa mbele
wakati wa ibada ya kuiombea iliyofanyika nyumbani kwa mbunge huyo
Kijichi Dar es Salaam leo, kabla ya kusafirishwa kwenda Ludewa kwa
mazishi.
Mjane wa Deo Filikunjombe, Sarah (katikati) akisaidiwa na jamaa zake wakati wa ibada hiyo.
Waombolezaji wakiwa kwenye ibada hiyo.
Padri Maxmillian Wambura, kutoka Parokia ya Mtakatifu Wote Kiluvya akiyamwagia mafuta ya baraka majeneza hayo.
Waombolezaji wakiwa katika ibada hiyo.
Waombolezaji wakiwa wamebeba jeneza la Plasdus Haule.
Familia ya Filikunjombe ikiwa katika ibada hiyo.
Waombolezaji wakiwa kwenye ibada hiyo.
Nyumba
ya Filikunjombe ambayo inadaiwa amekaa wiki mbili tangu ahamie baada ya
kukamilika ujenzi wake 'Hakika tumuache mungu aitwe mungu"
(Imeandaliwa na mtandao wa habari za jamii.com)
Friday, October 16, 2015
TUNDURU WAISHUKURU SERIKALI AWAMU YA NNE
Na Steven Augustino,
Tunduru.
WANUFAIKA katika mradi wa uhawilishaji fedha, kaya maskini wilayani
Tunduru mkoa wa Ruvuma, ambao unatekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii
Tanzania (TASAF) awamu ya tatu, wameishukuru serikali ya awamu ya nne kwa
kubuni na kuwapelekea mradi huo.
Aidha wanufaika hao, wametaja baadhi ya miradi ambayo
wameianzisha na kuanza kuwaletea maendeleo katika maisha yao baada ya kupokea fedha
kutoka TASAF kuwa ni ufugaji wa mbuzi, kondoo, kuku, kanga, bata, matibabu
pamoja na kununua vifaa vya ujenzi wa nyumba zao.
Wananchi hao walitoa shukrani hizo, walipokuwa kwenye
mahojiano maalum na mwandishi wetu ambaye alitembelea vijiji vya Mbesa, Nalasi,
Mchoteka, Tunduru mjini na Namasakata wilayani humo.
BREAKING NEWS: MGOMBEA UBUNGE DEO FILIKUNJOMBE AFARIKI DUNIA KATIKA AJALI YA CHOPA
Mbunge wa Ludewa mkoani Njombe, Deo Filikunjombe aliyevaa shati la kijani enzi ya uhai wake akishiriki na wananchi wake katika shughuli mbalimbali za maendeleo Jimbo la Ludewa. |
ALIYEKUWA Mbunge wa Jimbo la Ludewa mkoani Njombe na mgombea
wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Deo Filikunjombe
(Pichani) amefariki dunia wakati akielekea kwenye jimbo lake akitokea jijini
Dar es Salaam, akiwa kwenye Chopa iliyoanguka jana katika hifadhi ya wanyama ya
Selous iliyopo mkoani Morogoro.
Jeshi la Polisi limethibitisha kutokea kwa ajali hiyo, na kwamba
hakuna mtu aliyepona katika ajali hiyo.
Thursday, October 15, 2015
WATAKIWA KUTUNZA SHAHADA ZAO ZA KUPIGIA KURA
Na Muhidin Amri,
Namtumbo.
MGOMBEA nafasi ya ubunge Jimbo la Namtumbo mkoani Ruvuma, kwa
tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mhandisi Edwin Ngonyani, amewakumbusha
wananchi wa jimbo hilo, kutunza shahada zao za kupigia kura na kuchagua viongozi
watakaowaletea maendeleo.
Aidha amewataka kuwakataa wagombea wanaotumia kiasi kikubwa
cha fedha kuwahonga wapiga kura, ili waweze kuwachagua katika uchaguzi mkuu
unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Ngonyani alisema kitendo hicho ni cha aibu na fedheha, hivyo
kiongozi anayepatikana kwa mfumo huo akishachaguliwa hushindwa kutimiza ahadi alizotoa
kwa wananchi wake, badala yake hutumia nafasi yake aliyonayo kuliingiza Taifa
kwenye matatizo makubwa na kuwafanya wananchi anaowaongoza kuwa maskini.
UWT RUVUMA YA WAASA WANACHAMA WAKE
Na Muhidin Amri,
Songea.
KATIBU wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) mkoani
Ruvuma, Chiku Masanja amewataka wanawake wa mkoa huo, kuwaunga mkono wanawake
wenzao waliojitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kupitia chama
hicho.
Alisema wanawake wakipata nafasi za uongozi, itakuwa rahisi
kwao kuwatetea wanawake wenzao katika vikao mbalimbali vya maamuzi hasa vile vya
baraza la madiwani, ubunge na kupata fursa ya kushiriki kikamilifu katika shughuli
ambazo zitawawezesha wajikwamue
kiuchumi.
Chiku aliyasema hayo jana, wakati alipokuwa
akizungumza na Jumuiya ya wanawake, kata ya Misufini Manispaa ya Songea mkoani
humo kwenye ukumbi wa CCM tawi la mjini, kwa lengo la kujadili masuala
mbalimbali ya maendeleo ya umoja wao sambamba na kuwakumbusha juu ya wajibu wa
kila mwanamke kushiriki kikamilifu kupiga kura katika uchaguzi mkuu, Oktoba 25
mwaka huu katika eneo lake analoishi.
Tuesday, October 13, 2015
MARTIN MSUHA CHAGUO LA WANAMBINGA VIJIJINI APANIA KUWALETEA MAENDELEO WANANCHI WAKE
Na Kassian Nyandindi,
OKTOBA 25 mwaka huu, ni siku maalum ambayo Watanzania
wataweka historia kubwa ya kuwachagua viongozi wao watakaoweza kuwaongoza
katika kipindi cha miaka mitano ambao ni diwani, mbunge na rais kwa kuvihusisha
vyama mbalimbali vya siasa ambavyo vimesajiliwa kisheria hapa nchini.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni chama ambacho kimeendelea
kuiongoza nchi hii, baada ya kushinda uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2010,
ambapo uchaguzi huo ulivishirikisha vyama vya upinzani au vyama rafiki kama
inavyoelezwa na baadhi ya makada wa chama.
Tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi hapa nchini, Julai
2 mwaka 1992, CCM ni chama ambacho Watanzania wengi wanakiamini na kukichagua
kiendelee kushika dola kwa miaka mingi sasa.
Watanzania hao katika vipindi vyote vya chaguzi zilizopita,
waliamua kwa dhati kuwachagua wagombea waliotokana na chama hicho baada ya
kuridhishwa na sera zake, ambazo zinalenga kuwaletea maendeleo.
Katika makala haya Mwandishi wetu, anapenda kuelezea juu ya
nafasi ya Ubunge ni moja kati ya nafasi nyeti ambayo wananchi watakuwa na haki
ya kuchagua kama vile katiba ya nchi yetu inavyotaka, ambapo wakati ukifika
upigaji wa kura utafanyika katika majimbo mbalimbali ya uchaguzi na kupatikana
kiongozi ambaye atawaongoza wananchi wake katika eneo husika.
CUF TUNDURU YALAANI KUCHANWA MABANGO YA MGOMBEA WAKE
Na Steven Augustino,
Tunduru.
CHAMA cha Wananchi (CUF) wilaya
ya Tunduru mkoani Ruvuma, kimelaani vikali kitendo cha
kuchanwa mabango ya mgombea wake wa udiwani kata ya Mlingoti Mashariki,
Mohamed Nyoni.
Kwa mujibu wa taarifa za tukio hilo, zinaeleza kuwa zaidi ya
mabango 300 yamechanwa na vijana wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) na kwamba mabango hayo, yalikuwa yamebandikwa katika maeneo
mbalimbali ya kata hiyo.
Sambamba na kuchanwa kwa mabango hayo, pia taarifa hizo
zinasema kuwa watu hao walichana mabango ya mgombea wao wa
ubunge jimbo la Tunduru Kaskazini, anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya
Wananchi (UKAWA) Manjolo Kambili.
MGOMBEA UBUNGE TUNDURU KUSINI AFANANISHWA NA JEMBE
Na Steven Augustino,
Tunduru.
WAPENZI na wakereketwa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la
Tunduru Kusini mkoani Ruvuma, wamemfananisha mgombea ubunge wa jimbo hilo, Daimu
Mpakate kuwa ni sawa na jembe na pembejeo za kilimo, ambavyo
wamekuwa wakivitabikia kwa muda mrefu jimboni mwao.
Wananchi wenye bendera za chama hicho, walikuwa na
mabango yenye kubeba ujumbe wa aina mbalimbali ambao ulikuwa
ukimuunga mkono mgombea huyo, huku wakiimba nyimbo za
kumpongeza kuchaguliwa kwake, kuwa mgombea wa ubunge kwa tiketi ya chama hicho.
Hayo yalibainishwa kwa vitendo kutokana na wananchi hao, pale
walipojitokeza kwa wingi huku wakiwa wameinua mabango hayo ambayo yalikuwa
na ujumbe wakumpa moyo mgombea, kwamba watamchagua kwa kumpatia kura zaidi ya asilimia
zaidi ya 80.
NALICHO: JENGENI UWEZO KWA WATUMISHI WAJIENDELEZE KIMASOMO
Na Muhidin Amri,
Namtumbo.
SERIKALI wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma, imeziagiza idara
na taasisi za serikali wilayani humo, kuhakikisha zinawajengea uwezo watumishi
wao kwa kuwapatia nafasi ya kwenda kujiendeleza kimasomo, ili
kupunguza tatizo sugu la wataalamu wa kada mbalimbali ikiwa ni lengo la kuongeza
ufanisi mahali pa kazi.
Mbali na hilo, wakuu wa idara husika wametakiwa kuwasimamia
na kufuatilia kwa karibu watumishi wazembe ambao wanafanya kazi zao kwa mazoea,
kitendo ambacho kinasababisha kutokea
malalamiko ya hapa na pale kutoka kwa wananchi.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa wilaya hiyo, Chande Nalicho
alipokuwa akizungumza na wakuu wake wa idara katika Halmashauri hiyo na kukemea
tabia ya baadhi ya watumishi, kukwamisha kwa makusudi mipango mbalimbali ya
maendeleo inayotekelezwa na serikali kwa manufaa ya jamii.
TASAF NAMTUMBO YASEMA BAADHI YA WANASIASA WANAPOTOSHA WANANCHI
Na Muhidin
Amri,
Ruvuma.
OFISA ushauri na ufuatiliaji, Mfuko wa Maendeleo ya
Jamii (TASAF) hapa nchini wilaya ya Namtumbo mkoani
Ruvuma, Edson Kagaruki amekanusha taarifa
za upotoshaji zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa wilayani humo, kwamba mfuko
huo unafanya kazi ya kuhawilisha fedha kwenda kaya maskini, kwa lengo la
kukisaidia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kiweze kushinda katika uchaguzi mkuu
utakaofanyika, Oktoba 25 mwaka huu.
Kufuatia maneno hayo, Ofisa huyo wa TASAF wilayani humo amewataka wanasiasa hao kuacha
porojo hizo na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali, katika
kupambana na umaskini hapa nchini.
Aidha amewakumbusha kutumia majukwaa ya kisiasa, kueleza sera
zao na sio kuwapotosha wananchi kwa mambo ambayo hayana msingi, jambo ambalo linaweza
kuchochea uhasama katika jamii.
Monday, October 12, 2015
VITUO 216 JIMBO LA PERAMIHO KUTUMIKA KUPIGIA KURA
Mlemavu asiyeeona akisoma mfano wa karatasi ya kupigia kura, wakati wa mkutano kati ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Watu wenye ulemavu. |
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
JUMLA ya vituo 216 vimetengwa katika jimbo la Peramiho,
lililopo katika Halmashauri ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, kwa ajili ya
kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu ambao unatarajiwa kufanyika Oktoba, 25 mwaka
huu.
Akizungumza na mwandishi wetu, kwa niaba ya msimamizi mkuu wa
uchaguzi wa jimbo hilo Sixbert Valentine, Ofisa uchaguzi wa Halmashauri ya
wilaya ya Songea Furaha Mwangakala, alisema kuwa maandalizi kwa ajili ya
uchaguzi huo yamekamilika.
Mwangakala alifafanua kuwa katika kila kituo ndani ya Jimbo
hilo, kutakuwa na wapiga kura 450 kwa lengo la kupunguza msongamano na kutoa
fursa kwa wananchi wote ambao wamejiandikisha, waweze kupiga kura bila kupata usumbufu
wa aina yoyote ile.
Alisema kuwa, kufuatia zoezi hilo jumla ya watu 67,334 kwa Jimbo
la Peramiho wenye sifa ya kupiga kura wamejiandikisha, miongoni mwao yakiwemo
makundi mbalimbali ya wazee, vijana, wanawake kwa wanaume ili waweze kutumia
haki yao ya msingi kuwachagua viongozi wao.
MANJORO KUMBWAGA RAMO TUNDURU KASKAZINI
Na Steven Augustino,
Tunduru.
WAKATI kampeni za Uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika Oktoba
25 mwaka huu zikiendelea kushika kasi sehemu mbalimbali hapa nchini, mgombea
ubunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini kupitia tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF)
na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) Manjoro Kambili, amesema
ataendelea kujiwekea mikakati ya kuhakikisha kwamba anajipatia ushindi mnono na
kujinyakulia jimbo hilo, ili aweze kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Jimbo hilo kwa sasa mgombea huyo, anapambana na Mhandisi Ramo
Makani ambaye anapeperusha bendera kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hayo yamebainika kufuatia uchunguzi uliofanywa na mwandishi
wa habari hizi, ambapo taarifa zinaonesha kuwa Kambili amechukua maamuzi
hayo kutokana na kuwepo kwa mgogoro mkubwa miongoni mwa wanachama wa CCM ambao
unafukuta chini kwa chini, huku kukiwa na kundi kubwa lililoanza kujitokeza na
kumuunga mkono mgombea huyo wa UKAWA.
AUAWA NA TEMBO AKIWA SHAMBANI
Na Steven Augustino,
Tunduru.
MKAZI mmoja ambaye ni wa kijiji cha Kalulu, wilayani Tunduru
mkoa wa Ruvuma, Said Athuman (42) amefariki dunia baada ya kushambuliwa na
Tembo, wakati akiwa shambani kwake.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, walisema kuwa tukio
hilo lilitokea Septemba 29 mwaka huu, majira ya jioni baada ya kundi la Tembo kujitokeza
na kumvamia.
Alifa Abdalah Said ambaye ni Kaka wa marehemu huyo, alisema
chanzo cha tukio hilo kilitokana na maafisa wa idara ya wanyama pori ambao
wanalinda wanyama katika kituo cha hifadhi Kalulu kilichopo kwenye hifadhi ya
taifa ya Selous, walikuwa wakiwafukuza Tembo hao katika maeneo waliyokuwepo,
ndipo walikimbilia shambani huko na kusababisha mauaji.
MAMBO MAZURI TUNDURU WAIBUKA KIDEDEA
Na Steven Augustino,
Tunduru.
TIMU ya soka, Mambo Mazuri FC ya Tunduru mjini mkoani Ruvuma,
imeibuka kidedea kupitia ligi ya Polisi Jamii, baada ya
kuwafunga mahasimu wao, Vampire FC magoli manne kwa matatu katika
mchezo mkali, uliorindima kwenye uwanja wa Chama Cha Mapinduzi mjini hapa.
Kutokana na matokeo hayo, Vampire FC imeambulia nafasi ya
pili na mshindi wa tatu katika mashindano hayo ikachukuliwa na Jobe FC.
Kulingana na maelekezo yaliyotolewa na Mratibu wa mashindano
hayo, Inspector Songelael Jwagu mshindi wa kwanza katika mashindano
hayo atazawadiwa kikombe, seti moja ya jezi na mpira mmoja wa miguu.
Friday, October 9, 2015
DED TUNDURU ACHUKIZWA WANANCHI KUUZIWA MAENEO YA MAKABURI
Na Steven Augustino,
Tunduru.
HALMASHAURI ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, imewataka wananchi
wake kuzingatia taratibu husika, hasa pale wanapohitaji kununua maeneo ya viwanja
kwa ajili ya kujenga nyumba au kuweka makazi yao ya kudumu.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo, Tinna Sekambo alitoa
rai hiyo Ofisini kwake alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu, na akatumia
nafasi hiyo kuwataka kutoa ushirikiano pale wanapoona wanatapeliwa na wajanja
wachache ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Sekambo alifafanu kuwa, tahadhali hiyo ameitoa kufuatia
kuwepo kwa taarifa za kuibuka kwa kundi la matapeli wilayani humo, ambao
wamekuwa wakiwauzia watu viwanja na kuwapatia hati bandia.
Alisema kufutia hali hiyo, Ofisi yake inafanya uchunguzi kwa
kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kuweza kuwabaini na kuwachukulia hatua za
kisheria haraka iwezekanavyo, kabla ya wananchi hawajapata hasara kubwa.
POLISI WATOA ONYO SIKU YA UCHAGUZI MKUU
Na Muhidin Amri,
Songea.
JESHI la Polisi mkoani
Ruvuma limesema kwamba, halitakuwa tayari kuona amani na utulivu vikivurugwa
hasa katika kipindi hiki cha kampeni na kuelekea siku ya kupiga kura, kutokana
na sababu za itikadi za kisiasa.
Kauli hiyo imetolewa jana na Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Revocatus Malimi alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake kuhusiana na hali ya usalama ya wananchi, kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika oktoba 25 mwaka huu.
Malimi alisema Jeshi hilo limejiandaa vya kutosha kuhakikisha kwamba, uchaguzi wa mwaka huu unaendeshwa kwa amani na utulivu, katika maeneo mbalimbali mkoani humo mpaka siku ya mwisho ya upigaji kura.
Tuesday, October 6, 2015
PICHA YA WIKI: MKUU WA WILAYA MBINGA AKIFURAHIA TEKINOLOJIA YA MAJIKO SANIFU YA KUPIKIA
POLISI NA JWTZ WAFANIKIWA KUHARIBU MABOMU MAWILI
Na Mwandishi wetu,
Songea.
JESHI la Polisi mkoani
Ruvuma, kwa kushirikiana na askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ)
wamefanikiwa kuharibu mabomu mawili, yaliyokutwa katika Kijiji cha
Ngwinde kata ya Litola, wilayani Namtumbo mkoani humo.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Revocutus Malimi alisema kuwa mabomu hayo yaliharibiwa ili yasiweze kuleta madhara katika jamii, ambapo moja liliharibiwa majira ya saa nne asubuhi na la pili saa sita mchana.
Alisema kuwa
katika mabomu hayo, moja lilikuwa aina ya Motor lenye ukubwa wa mm. 82 ambalo
lilikutwa chini ya mti na la pili ni la kurusha kwa Roketi (RPG) lenye
ukubwa wa mm. 122 ambalo lilichimbiwa chini ya ardhi.
WASHIKILIWA KWA KOSA LA KUJIANDIKISHA MARA MBILI KATIKA BVR
Revocatus Malimi, kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma. |
Na Muhidin Amri,
Ruvuma.
JESHI la Polisi
mkoani Ruvuma, linawashikilia watu 18 kwa kosa la kujiandikisha zaidi ya
mara mbili katika daftari la kudumu la wapiga kura, kwa njia ya
kielektroniki (BVR).
Kukamatwa kwa watu
hao, kumetokana na ushirikiano kati ya Jeshi hilo na taasisi nyingine
zinazohusika na uandikishaji huo.
Kaimu Kamanda wa
Polisi wa mkoa huo, Revocutus Malimi alisema kwamba watu hao wamekamatwa kutoka
maeneo mbalimbali ya mkoa huo, hata hivyo bado wanaendelea kuwatafuta
wengine ambao wanadaiwa nao kujiandikisha zaidi ya mara moja katika daftari
hilo.
Sunday, October 4, 2015
WANAFUNZI SEKONDARI AGUSTIVO MBINGA WAFUNDWA
Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
WANAFUNZI wanaohitimu masomo ya kidato cha nne wilaya ya
Mbinga mkoa wa Ruvuma, wameshauriwa kutojiingiza kwenye masuala ya anasa kama
vile vitendo vya kimapenzi, ambavyo husababisha kukatisha ndoto ya kujiendeleza
kimasomo katika maisha yao.
Aidha wakati wote wametakiwa kuonesha dhamira ya kusonga mbele, kwa kujikita zaidi kwenye malengo ya kuongeza elimu kwa faida
ya maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
Ushauri huo ulitolewa jana na Khalid Kingi, ambaye ni Katibu
msaidizi wa Umoja wa Vijana Chama Cha Mapinduzi Taifa (UVCCM) katika mahafali
ya kidato cha nne shule ya sekondari Agustivo iliyopo mjini hapa, ambapo katika
sherehe hizo alikuwa akimwakilisha mgeni rasmi Katibu Mkuu UVCCM Taifa, Sixtus
Mapunda.
“Ndugu zangu mnahitimu masomo yenu katika kipindi ambacho
kina changamoto nyingi, natoa wito kwenu na kwa wengine hapa wilayani ambao
wanahitimu kidato cha nne kama ninyi, huko muendako mkapambane na changamoto za
ulimwengu huu kwa kuweka malengo ya kuongeza elimu, na kuacha tabia ya
kufikiria maisha ya mtaani ambayo yatawafanya mwisho wa siku mjiingize kwenye
makundi mabaya”, alisema Kingi.
MGOMBEA URAIS ACT ASEMA MAENDELEO YALIYOPO YANATOKANA NA JITIHADA ZA VYAMA VYA UPINZANI
Anna Mghwira mgombea urais kwa tiketi ya chama cha ACT Wazalendo, akiwa katika moja ya mikutano yake ya kampeni hapa nchini. |
Na Steven
Augustino,
Tunduru.
WANANCHI wilayani
Tunduru mkoa wa Ruvuma, wameshauriwa kufanya mabadiliko kwa kuchagua wagombea
kutoka vyama vya upinzani ifikapo Oktoba 25 mwaka huu, ili waweze kuwaletea
maendeleo yenye kasi ya ajabu kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.
Mgombea urais,
Jamuhuri ya muungano wa Tanzania kwa tiketi ya chama cha ACT Wazalendo, Anna
Mghwira alisema hayo alipokuwa akizungumza na maelfu ya wananchi ambao
walijitokeza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika viwanja vya Baraza la Idd
mjini hapa.
Aidha mgombea
huyo alipokuwa akizungumza na wananchi hao, aliahidi kuunda serikali ya umoja
wa kitaifa akidai kwamba lengo lake kuondoa chokochoko zilizopo, na mitafaruku
ambayo baadaye inaweza kuleta mapigano (Vita) miongoni mwa jamii.
UHAMIAJI RUVUMA WATOA ONYO
Na Mwandishi
wetu,
Songea.
IDARA ya
uhamiaji mkoa wa Ruvuma, imewaonya watu wasiokuwa raia wa
Tanzania kutojihusisha kwa namna yoyote ile katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa
kufanyika Oktoba 25 mwaka huu, na endapo watafanya hivyo watakuwa wamekiuka
sheria za nchi.
Mbali na hilo
imeelezwa kuwa kushiriki katika uchaguzi huo kwa mtu asiyekuwa raia wa
Tanzania, kunaweza kusababisha taifa kupata viongozi wabovu wasiokuwa na
uchungu wa kuleta maendeleo kwa Watanzania.
Ofisa uhamiaji wa
mkoa huo, Hilgaty Shauri alitoa rai hiyo alipokuwa akizungumza na vyombo
mbalimbali vya habari mjini songea.
SERIKALI KUENDELEA KUBORESHA SEKTA YA AFYA
Na Muhidin Amri,
Namatumbo.
SERIKALI imesema,
itaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za wauguzi, madaktari
na kuboresha miundombinu mbalimbali ili kuwavutia watumishi wa
idara ya afya, kupenda kufanya kazi wakiwa katika mazingira mazuri na
waweze kutekeleza majukumu ya kazi zao kwa ufanisi zaidi.
Kauli hiyo ilitolewa
na Mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Chande Nalicho alipokuwa akifungua
mkutano wa mwaka wa uchaguzi kwa viongozi wa chama cha wauguzi mkoani
humo, uliofanyika kwenye ukumbi wa Faraja uliopo mjini hapa.
Mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Chande Nalicho. |
Alifafanua kuwa
serikali inatambua matatizo yanayowakabili wafanyakazi wa idara hiyo, ambapo
itaendelea kuboresha mazingira yao ikiwemo pia mishahara na maeneo ya kufanyia
kazi zao.
Mkuu huyo wa wilaya
aliongeza kuwa bado serikali inaendelea kuajiri watumishi wengi mwaka hadi
mwaka, sambamba na ujenzi wa vituo vya afya, zahanati na hospitali ili kukidhi
mahitaji husika ya watanzania kwa kila mkoa, wilaya, kata na vijiji
ikiwa ni lengo kwamba wananchi wake waweze kupata huduma ya matibabu kwa
urahisi.
NGAGA: MWALIMU ATAKAYEKUWA MTOVU WA NIDHAMU ATACHUKULIWA HATUA
Na Muhidin Amri,
Ruvuma.
WALIMU nchini
wametakiwa kukataa kugeuzwa wapiga debe na kuwa madalali wa vyama
vya siasa, badala yake wazingatie majukumu yao ya kazi kwa kuongeza
juhudi ya ufundishaji watoto darasani, hatua ambayo itasaidia kuwaongezea uelewa
wanafunzi na kukuza taaluma hapa nchini.
Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi ngaga alisema hayo, mwishoni mwa wiki alipokuwa akifungua kikao cha siku tatu kwa wakuu wa shule za sekondari kutoka mikoa mitatu ya nyanda za juu kusini Ruvuma, Njombe na Iringa kilichofanyika kwenye ukumbi wa Kanisa katoliki uliopo mjini hapa.
Mbali na hilo, pia amewaonya walimu hao kutotumia maeneo ya shule kufanyia kampeni wanasiasa kwa sababu maeneo hayo, sio rasmi kwa ajili ya shughuli hizo huku akisisitiza kwamba tabia hiyo inawanyima fursa watoto, kupata haki yao ya msingi.
HII NI KERO NA AIBU KWA MANISPAA YA SONGEA
Friday, October 2, 2015
MWANAFUNZI SHULE YA MSINGI MAHELA MBINGA AOMBA MSAADA AKATIBIWE INDIA
MAELEZO YA PICHA HII:
Huyu ni mtoto Yasin Ngonyani mwenye umri wa miaka 13, ambaye ni mwanafunzi wa darasa la sita shule ya msingi Mahela wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, anaomba msaada wa kuweza kufanikiwa kwenda nchini India kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya oparesheni ya mguu wake ambao unamsumbua kwa muda mrefu sasa.
Kwa mujibu wa Madaktari ambao wamemfanyia uchunguzi wa awali, gharama za matibabu yake ni shilingi milioni 17, hivyo yeyote atakayeguswa na tatizo hilo ambaye yupo tayari kumsaidia kuweza kufanikisha matibabu ya mguu huo, anaweza kuwasiliana na mzazi wake kwa simu namba; 0763 - 770387 au 07 - 12345831.
Hata hivyo kwa mawasiliano zaidi unaweza kupiga simu namba; 0754 - 236443 kwa Ofisa ustawi jamii, Davina Maketa hapa wilayani Mbinga ambaye ndiye anafuatilia kwa karibu na kushughulikia matibabu ya mtoto huyo.
KUTOA NI MOYO SIO UTAJIRI !!
Subscribe to:
Posts (Atom)