Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.
KAMATI ya siasa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Ruvuma, imeitaka serikali
kupitia Wakala wake wa barabara (TANROADS) mkoani humo kusimamia kikamilifu ujenzi
wa daraja la mto Ruhuhu, lililopo wilayani Nyasa mkoani hapa na kumuhimiza mkandarasi
anayejenga daraja hilo akamilishe ujenzi wake kwa wakati na viwango vinavyokubalika.
Aidha kampuni ya ujenzi Lukolo Construction Limited ndiyo
inayofanya kazi ya ujenzi wa daraja hilo, ambapo Wajumbe wa Kamati hiyo walitembelea juzi kuona maendeleo ya mradi huo, ambao
upo katika kata ya Lituhi wilayani humo mpakani mwa mkoa wa Ruvuma na wilaya ya
Ludewa mkoa wa Njombe.
Mjumbe mmoja ambaye ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Ruvuma, Oddo
Mwisho alisema kuwa serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imejipanga
kikamilifu kwa kuhakikisha kwamba, inaondoa kero zilizopo kwa wananchi wake
wanaoishi katika maeneo hayo ndio maana inajenga daraja hilo hivyo mkandarasi
huyo anapaswa kufanya jitihada kuhakikisha ujenzi huo unakamilika ndani ya
mkataba husika.
Napegwa Kiseko ambaye ni Mhandisi mshauri ujenzi wa daraja
hilo aliiambia Kamati hiyo ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi kwamba mradi huo ujenzi
wake unafadhiliwa kwa asilimia mia moja na serikali ya Tanzania.
“Daraja hili linalojengwa hapa, lipo umbali wa kilometa 84
kutoka kijiji cha Kitai wilaya ya Mbinga ambako kuna barabara kuu ya kiwango
cha lami, tutahakikisha tunasimamia na kushauri kwa umakini mkubwa ili liweze
kukamilika kwa viwango vinavyokubalika na wananchi waweze kuanza kulitumia”,
alisema Kiseko.