Saturday, March 11, 2017

CWT YASAIDIA WATOTO WALEMAVU SONGEA

Na Julius Konala,        
Songea.

KATIKA kuadhimisha siku ya Wanawake duniani, Chama Cha Walimu (CWT) kitengo cha wanawake Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma kimetoa msaada wa vitu mbalimbali kwa watoto wenye ulemavu ambao wana matatizo ya kusikia (Viziwi) katika shule ya msingi maalum ya Mtakatifu Vincent Ruhuwiko iliyopo mjini hapa.

Msaada huo ulitolewa jana shuleni hapo na Mwenyekiti wa CWT kitengo cha wanawake Manispaa ya Songea, Zabiuna Nchimbi ambapo alidai kuwa wameamua kufanya hivyo baada ya kuguswa na tatizo hilo linalowakabili watoto hao wenye ulemavu wa kusikia.

Nchimbi alitaja msaada uliotolewa kwa ajili ya watoto hao kuwa ni viatu, nguo, mafuta ya kupaka, chumvi pamoja na sabuni za kufulia huku akidai kuwa kufanikiwa kwa zoezi hilo kumetokana na kuchangishana walimu wenyewe.


Awali akizungumza kabla ya kukabidhi msaada huo, Mwenyekiti huyo alisema kuwa walimu hao wanatambua changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo watoto hao wenye ulemavu wa kusikia, ndio maana wakaamua kuchangishana vitu hivyo kwa lengo la kusaidia watoto hao ambapo ametoa rai kwa taasisi mbalimbali kuona umuhimu wa kutembelea shuleni hapo kwa ajili ya kuendelea kuwasaidia.

Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mtakatifu Vincent Ruhuwiko Sista Anna Mgaya, amekishukuru Chama hicho cha walimu kitengo cha wanawake Manispaa ya Songea kwa msaada wao kwa madai kuwa imedhihirisha ni jinsi gani wanavyowajali na kuwathamini watoto wenye ulemavu.

Mgaya alisema kuwa watoto hao wenye ulemavu wa kusikia wanatakiwa kuthaminiwa na kwamba katika shule hiyo wapo watoto pia wenye vipaji mbalimbali ambapo baadhi yao wamefanikiwa kufika mpaka elimu ya juu na vyuo vya ufundi.


Hata hivyo Mwalimu mkuu huyo aliongeza kwa kusema kuwa changamoto kubwa wanayokumbana nayo watoto hao ni baadhi ya madaktari na watumishi mbalimbali, kushindwa kuwasiliana nao kwa alama pindi wanapougua na kufuatilia huduma nyingine maofisini hivyo ametoa wito kwa jamii kujifunza lugha za alama kwa lengo la kuwarahisishia kupata huduma kwa urahisi watoto hao.

No comments: